Katibu mkuu Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano anayeshughulikia Ujenzi Arch. Elius Mwakalinga akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na mradi wa ujenzi wa nyumba za makazi (Magomeni kota,) jijini Dar es Salaam ambapo amesema kuwa mradi huo utapokea kaya 656 na tayari umekamilika kwa asilimia 88, jijini Dar es Salaam.


Meneja mradi wa nyumba za makazi (Magomeni kota,) unaotekelezwa jijini Dar es Salaam Arch. Benard Mayemba (wa pili kushoto) akieleza mchakato wa uendelezaji wa mradi huo na kusema kuwa, mradi huo umetengewa maeneo maalumu yakiwemo maduka kwa wakazi wa eneo hilo, katikati ni Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano anayeshughulikia Ujenzi Arch. Elius Mwakalinga.


Muonekano wa nyumba za makazi (Magomeni Kota,) jijini Dar es Salaam

Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam.

KATIBU Mkuu Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano anayeshughulikia Sekta ya Ujenzi, Arch. Elius Mwakalinga  Novemba 30, 2020 amefanya ziara na kukagua maendeleo ya mradi wa ujenzi wa nyumba za makazi wa Magomeni Kota jijini Dar es Salaam. Katika ziara hiyo Arch. Mwakalinga amepitia na kuona maendeleo mbalimbali yanayoendelea katika mradi huo ikiwa ni pamoja na kujiridhisha na utekelezaji wa maelekezo aliyoyatoa alipotembelea Oktoba 20, 2020.

Akizungumza na Uongozi wa TBA ambao ni Wakandarasi na Washauri Elekezi wa mradi huo,  Arch. Mwakalinga amesema kuwa alipotembelea Oktoba 20, 2020 maendeleo ya mradi yalikuwa ni asilimia 81 lakini kwa sasa ujenzi huo umefikia kiwango cha asilimia 88. Vilevile ameipongeza TBA kwa kuzingatia maelekezo yake aliyoyatoa pamoja na kuonesha ubunifu kwa kujenga majengo ya kupokelea wageni, na majengo ya maduka ambayo yatatoa huduma kwa wakazi hao wa Magomeni Kota.

Aidha,  ameagiza TBA kupitia Idara ya Miliki kuweka Afisa  katika eneo la mradi huo kuanzia sasa kwa ajili ya kupokea maoni mbalimbali kutoka kwa wateja ambao wangependa kuuziwa au kupangishwa nyumba hizo na kufanya tathmini ambayo itasaidia kutambua mahitaji ya soko kwa nyumba nyingine zitakazojengwa mkabala na majengo ambayo yanaendelea kujengwa. 

Pia  ameongelea ubunifu unaoendelea katika mji wa Serikali awamu ya pili pamoja na ukarabati wa nyumba unaoendelea katika mikoa ya Dodoma na Dar es Salaam.

Mradi wa ujenzi wa nyumba za Magomeni Kota utakapokamilika unatarajiwa kutoa makazi kwa kaya 656.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...