Kaimu Askofu wa kanisa la Mlima wa Moto Rose Mgeta (wa pili kushoto) akizungumza na waumini wa kanisa hilo mara baada ya kutangazwa kushika nafasi ya uongozi katika nafasi hiyo kulia kwake ni mchungaji Paul Kuria kutoka nchini Kenya na kushoto kwake ni Askofu Yohana Masinga kutoka Dodoma na anayefuatia ni mtoto wa marehemu Mama Getrude Rwakatare Dkt. Rose Rwakatare leo jijini Dar es Salaam. 
Kaimu Askofu wa kanisa la Mlima wa Moto Rose Mgeta (katikati) akiongoza maombi mara baada ya kutajwa kuwa kiongozi wa kanisa hilo ambapo ameomba ushirikiano kutoka kwa waumini wa kanisa hilo, kulia kwake ni mchungaji. Paul Kuria kutoka nchini Kenya na kushoto ni Askofu Yohana Masinga kutoka Dodoma, leo Mikocheni B, Jijini Dar es Salaam. 
Kaimu Askofu wa Kanisa la Mlima wa Moto lililopo Mikocheni B jijini Dar es Salaam Rose Mgeta(wa tatu kushoto) akiwa na wachungaji viongozi na familia ya marehemu Askofu Getrude Rwakatare, wakikata utepe kuzindua maombi maalumu ya siku 13 kuanzia leo yajulikanayo kama Shilo kanisani hapo, leo jijini Dar es Salaam.


*Ni kaimu Askofu Rose Mgeta, aomba ushirikiano na kumuenzi kwa vitendo Askofu Rwakatare.

Na Leandra Gabriel, Michuzi TV

BAADA ya kanisa la Mlima wa Moto kumpoteza muasisi na Askofu wa kanisa hilo Mama Getrude Rwakatare aliyefariki dunia Aprili 20 mwaka huu, leo Desemba 6 kanisa hilo limemtangaza Rose Mgeta aliyekuwa mchungaji kiongozi wa kanisa hilo kuwa kaimu Askofu wa makanisa hayo huku taratibu za kumpatia kofia ya uaskofu kamili zikiendelea.

Akizungumza wakati wa ibada ya jumapili leo, mwakilishi wa viongozi na wachungaji wa makanisa ya Mlima wa Moto Apostle. Dickson Mashima amesema kuwa baada ya mbeba maono kulala usingizi wa milele, kwa kushirikiana na familia wakaona ni vyema kuwa na mtu wa kuendeleza maono hayo, na kwa nafasi hiyo aliyekuwa mchungaji kiongozi Rose Mgeta atakuwa kaimu Askofu wa makanisa yote ya Mlima wa Moto.

Amesema, makanisa hayo kwa sasa yana kaimu Askofu na baadaye mipango kamili itafanyika ili kumfanya kuwa Askofu kamili na kuwaomba waumini na viongozi wote kushirikiana naye.

Akizungumza mara baada ya kupewa jukumu la kubeba maono hayo Kaimu Askofu mteule Rose Mgeta amewashukuru waumini na familia ya Rwakatare kwa kuonesha ushirikiano katika kipindi kigumu cha kumpoteza Askofu Rwakatare na kujitoa kwa moyo katika kuendeleza maono yake.

"Kazi ya Mungu si mchezo, unaajiriwa na tajiri usiyemuona na ukikosea anakuadhibu...naombeni maombi yenu, ushirikiano na kufanya kazi kwa umoja." Amesema.

Amesema watoto wa Askofu Rwakatare wapo bega kwa bega kwa kuwa wana mzigo wa mama yao katika kuendeleza maono yake ambayo yamegusa wengi kwa namna mbalimbali.

Baadhi ya waumini wa kanisa hilo wamehaidi kuendelea kuyaenzi mema na maono yaliyoanzishwa na muasisi wa kanisa hilo na kuahidi ushirikiano zaidi kwa Kaimu Askofu mteule Rose Mgeta katika kujenga Taifa la Mungu.

Hafla hiyo iliyoenda sambamba na ufunguzi wa  maombi maalumu ya siku 13 kuanzia leo yajulikanayo kama Shilo kanisani hapo na yamehudhuriwa na maaskofu na wachungaji kutoka ndani na nje ya nchi akiwemo mchungaji Paul Kuria kutoka nchini Kenya.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...