Na. Bebi Kapenya

WAKALA wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) umeendelea kusimamia na kufanya ukarabati wa miundombinu ya barabara na madaraja katika maeneo mbalimbali Halmashauri ya Manispaa ya Lindi mkoani Lindi.

Meneja wa TARURA Halmashauri ya Manispaa ya Lindi, Mhandisi Lusekelo Mwakyami alisema kuwa wameshakamilisha ujenzi wa barabara kwa kiwango cha Lami Kilomita 6.2 kwa gharama ya Shilingi Bilioni 7.1 na Kilomita nyingine 1.8 za barabara zinaendelea kufanyiwa matengenezo kwa kiwango cha Lami ambapo miradi yote hiyo inafadhiliwa na Benki ya Dunia kupitia Mpango wa Kuzijengea Uwezo Halmashauri mbalimbali nchini mpango ambao kwa sasa unasimamiwa na TARURA.

“Tunatekeleza miradi yetu kwa kulenga maeneo ya kiuchumi na kijamii kama vile vituo vya afya, shule na maeneno ya biashara ili kuboresha mazingira ya kuishi na kukuza uchumi wa wananchi”, alisema Mhandisi Mwakyami.

Mhandisi huyo alieleza kuwa mbali na kutekeleza miradi inayofadhiliwa na Benki ya Dunia, pia wametekeleza miradi mingine ya barabara iliyo chini ya Mfuko wa Barabara kwa kujenga Barabara ya Nkurumah yenye urefu wa Mita 450 kwa kiwango cha lami ambayo imeshakamilika na kuwekewa taa, Barabara ya Amani yenye urefu wa Mita 500 na Barabara ya Resthouse yenye urefu wa Mita 700 zote zikiwa kwa kiwango cha lami.

Aidha, Meneja huyo aliongeza kuwa miradi mingine wanayoendelea kuitekeleza ni ujenzi wa barabara yenye urefu wa Km 1.3 kutumia gharama nafuu Shilingi Milioni 767 ambayo bado kuwekewa tabaka la lami, mifereji na taa, ujenzi wa Barabara ya Wailes Km 2.5 kwa kiwango cha lami inayoelekea Ofisi ya Mkuu wa Mkoa kwa gharama ya Shilingi Bilioni 1.4 na pia wana mpango wa kujenga barabara nyingine ya Mita 700 kwa kiwango cha lami kwa gharama nafuu inayopita nyuma ya soko katika manispaa ya Lindi ujenzi unaotarajia kuanza hivi karibuni na ukarabati utachukua miezi 6.

Naye, Aisha Yusuph Mshana Mkazi wa Lindi ameipongeza TARURA kwa kuboresha barabara za mitaa na kuweka taa za barabarani kwani zimeweza kutoa hamasa kwa wananchi kushiriki shughuli za biashara hadi nyakati za usiku na kuwaongezea kipato.

‘’Kwa sasa Mji wetu umependeza, barabara zimejengwa kwa miundombinu ya kisasa kabisa ikiwemo taa za barabarani na hii imesaidia tunafanya biashara zetu hadi usiku kwasababu ya mwanga wa taa na pia ajali zimepungua wakati wa usiku kwasababu iwapo kutatokea gari limepata tatizo una uwezo wa kuliona”, alisema Bi. Aisha.

Naye, Bw. Juma Costa Mkazi wa Lindi ameishukuru Serikali kwa kuboresha barabara hizo ambapo hapo awali walikuwa wanapata shida ya vumbi na matope lakini kwasasa shida hiyo imepungua, pia ameiomba Serikali kufanya matengenezo ya mara kwa mara na kurekebisha baadhi ya taa za barabarani kwa wakati pale inapobidi ili kuwezesha upatikanaji wa huduma wakati wote.

Muonekano wa Barabara ya Makongoro kwa kiwango cha Lami yenye urefu wa Kilomita 1.7 iliyopo Kata ya Makumbi Halmashauri ya Manispaa ya Lindi mkoani Lindi.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...