Mwanasheria kutoka Ofisi Kuu ya Mashitaka Beatrice Mpembo kutoka Ofisi ya Mwendesha Mshtaka Mkuu (DPP), akizungumza wakati wa mjadala kuhusu namna ya kuwasaidia waathiriwa wa matatizo ya vitendo vya ukatili wa kijinsia iliyoandaliwa na Shirika la Wanawake katika Sheria na Maendeleo Afrika  (WiLDAF). Kushoto ni Hakimu Mfawidhi Mahakama ya Ilala, Martha Mpanze. Kulia ni daktari wa kituo cha ukatili wa kijinsia katika hospitali ya Amana, Margret Ibobo na  Koplo Kuluthum kutoka Jeshi la Polisi.
Mkurugenzi wa Shirika la Wanawake katika Sheria na Maendeleo (WiLDAF), Anne Kulaya akizungumza kwenye mkutano wa kusaidia waathirika wa vitendo vya ukatili wa kijinsia uliofanyika jana jijini Dar es Salaam. Wengine ni maofisa kutoka taasisi mbalimbali waliokuwa wakijibu maswali kutoka kwa washiriki wa mjadala huo.

Balozi wa Ireland nchini, Adrian Fitzgerald akiwa kwenye picha ya    pamoja na viongozi wa Shirika la Wanawake katika Sheria na Maendeleo Afrika  (WiLDAF) mara baada ya kufungua mafunzo ya siku mbili kuhusu namna ya kuwasaidia waathiriwa wa vitendo vya ukatili wa kijinsia ikiwemo ubakaji.

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

BAADHI ya wadau wameshauri wawepo madaktari maalum wa kushughulikia kesi za ubakaji na ukatili wa kijinsia watakaopewa mafunzo maalum na ulinzi ili wawe huru kutoa ushahidi mahakani

Ushauri huo ulitolewa na washiriki wa kongamano la mwendelezo wa siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia kuhusu namna ya kuwasaidia waathiriwa wa vitendo vya ukatili

Kongamano hilo liliandaliwa na Shirika la Wanawake katika Sheria na Maendeleo Afrika (WiLDAF) na kushirikisha maofisa kutoka Ofisi ya Mwendesha Mshtaka Mkuu wa Serikali DPP, Mahakimu Wafawidhi, Jeshi la Polisi, madaktari na wadau wa taasisi zisizo za kiserikali (Ngo’s.)

Grolia Bartazari kutoka Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS), alisema utaratibu wa sasa wa kila daktari kushughulikia mashauri ya ubakaji unasababisha kesi hizo kuchukua muda mrefu kumalizika kutokana na wengi kuzikacha.

Alisema ili kesi hizo ziwe nyepesi na zisikilizwe kwa haraka watengwe madaktari watakaopewa mafunzo maalum kuhusu namna ya kujaza fomu namba tatu (PF3) na namna ya kutetea ushahidi wao wanapoitwa mahakamani.

“Madakatri hawa watawajibika kwasababu hili ndilo litakuwa jukumu lao la msingi tofauti na sasa ambapo kila mtu anahusishwa, tukifanya hivyo tutasaidia hizi kesi ziishe haraka kwasababu zikichelewa kunatoa mwanya wa  uchakachuaji wa ushahidi,” alisema Grolia.

Mshiriki mwingine, Selemani Yusuf aliunga mkono hoja hiyo akisema kuwa baadhi ya madaktari wanakimbia kesi za ubakaji kutokana na kuchukua muda mrefu kusikilizwa.

Alisema kuahirishwa kwa kesi mara kwa mara kumekuwa kukiwachosha madaktari wanapoitwa kwenda kutoa ushahidi wao kuhusu vipimo walivyofanya kwa mwathiriwa.

“Unakuta daktari anaitwa mahakamani anaenda asubuhi lakini mpaka saa nane hajaitwa kwenye kesi na mwishowe anaambiwa kwamba kesi imeahirishwa sasa ndiyo sababu wengi hawataki kabisa kuona PF3,” alisema.

Dk. Rahina Ali wa Kituo cha Afya Kigamboni alisema madaktari wengi hawapendi kuhudumia wagonjwa wanaokwenda na PF3 kwa hofu ya usumbufu watakaoupata wa kwenda kutoa ushahidi wao mahakamani.

“Kwanza hatuna ulinzi, sisi ni tofauti kabisa na polisi kwasababu wao angalau wanaogopwa na wengine wana silaha sasa sisi madaktari tuna na sindano tu hivyo kuna haja ya kuwawekea mazingira mazuri madaktari,” alishauri.

“Tatizo lingine linalowafanya madaktari kuona kesi za namna hii ni kero ni tatizo la nenda rudi mahakamani…unaenda mahakama ya Temeke kutoa ushahidi kesi inaahirishwa kila wakati unaitwa mahakama ya Kisutu unakuta yale yale sasa inakuchukua muda mrefu kushinda mahakamani ndiyo maana hawazipendi,” alisema.

Gema Akilimali ambaye ni mwanachama wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), alishauri kesi za ukatili wa kijinsia ikiwemo ubakaji zipewe kipaumbele ili zikamilike kwa wakati.

Alisema kama polisi wanakerwa na vitendo vya ukatili wa kijinsia basi wanapaswa kuharakisha kukamilisha ushahidi wa kesi hizo ili wahusika wachukuliwe hatua badala ya mashauri hayo kukaa mahakamani miaka na miaka.

“”Lakini kuna ushahidi mwingine siyo wa kutafuta, unakuta mhusika kakutwa eneo la tukio na mwenyewe amekiri kuhusika lakini utashangaa kuona kesi hiyo inachukua muda mrefu na ukiuliza unaambiwa upelelezi bado unaendelea inashangaza sana,” alisema Gema.

Alisema hata vitendo vya rushwa mahakamani, polisi na kwenye mfumo mzima kimekuwa kikwazo kikubwa kwa kesi za ukatili wa kijinsia kumalizwa mapema na wakati mwingine ndugu kuhadaiwa na kuyamaliza nje ya mahakama.

“Inasikitisha sana wakati mwingine mke anaamua kumlinda mume wake aliyembaka binti yake kisa kulinda ndoa sasa jamii ielimishwe tuachane na huo utamaduni wa kulinda ndoa kwa namna hiyo kwani alipobaka hakujua kwamba anandoa,” alihoji Gema.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...