Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Hassan Abbasi, amewataka wafanyakazi wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) kuendelea kuwa wabunifu na kubuni mambo makubwa yatakayotekelezwa na Serikali katika shirika hilo.

Dkt. Abbasi ameyasema hayo leo jijini Dar es Salaam alipomwakilisha Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe Innocent Bashungwa, katika ufunguzi wa kikao cha Baraza la Wafanyakazi la TBC.

"Serikali imetimiza na itaendelea kutumiza wajibu wake kwenu; miaka mitano iliyopita hamkuwa mnapata fedha za uendeshaji na zile za miradi, leo serikali imewongezea na juzi tu mmeletewa hela zote za maendeleo kwa bajeti ya mwaka huu, kikao hiki lazima kisiwe cha malalamiko tena, kiwe sasa cha kufanya dhukuru kuhusu TBC inapaa kwenda wapi huko tuendako," alisema Dkt. Abbasi.

Alitumia fursa hiyo pia kuwapa maagizo sita wajumbe wa Baraza hilo ikiwemo kutaka kuona mipango mikubwa na yenye ubunifu katika Shirika hilo kuhakikisha linatimiza wajibu wake na kusisitiza mipango hiyo kila mfanyakazi ashiriki kuitekeleza.

Alisisitiza: "Mwanafalsafa mmoja amewahi kusema inachukua muda na kiasi kile kile cha nguvu yako kuwaza mambo makubwa au kuwaza mambo madogo yasiyo na tija. Kwa sababu hiyo nawaomba msipoteze muda kuwaza mambo madogo madogo na kuendekeza ulalamishi na majungu. Leteni mipango mikubwa na sisi Serikali tutashirikiana nanyi kuitekeleza."

Awali Mkurugenzi Mkuu wa TBC, Dkt. Ayub Rioba alieleza kuwa mkutano huo unalenga kuwapatia wajumbe hao, pamoja na mambo mengine, mada kuhusu uboreshaji wa ufanisi na kuleta mabadiliko katika taasisi hiyo kongwe ya Serikali.



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...