Na Said Mwishehe, Michuzi TV

MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kelevya nchini imeendelea na mikakati ya kukomesha biashara ya dawa hizo kwa kutumia mbinu mbalimbali ambazo zipo kwa mujibu wa Sheria.
Kwa sehemu kubwa Mamlaka hiyo imefanikiwa kwani takwimu zilizopo za kitaifa na kimataifa zinaonesha kwa sasa uingizaji, usambazaji na utumiaji wa dawa za kulevya nchini Tanzania umepungua kwa kiasi kikubwa sana ikilingaishwa na miaka ya huko nyuma.


Chini ya Kamishna Generali wa Mamlaka hiyo James Kaji pamoja na makamishna wengine wasaidizi walioko katika idara mbalimbali za mamlaka hiyo wamekuwa wakifanya kazi kubwa na nzuri katika mapambano dhidi ya biashara ya dawa za kulevya.Wanastahili kila aina ya pongezi.


Hata hivyo umefika wakati kwa jamii ya Watanzania kila mmoja kuona anao wajibu wa kushirkiana na Mamlaka hiyo pamoja na wadau wengine kukomesha biashara ya dawa za kulevya ambayo madhara yake ni makubwa zaidi kwa jamii inayotuzunguka kuliko faida zake.


Kwa mujibu wa tafiti ambazo zimefanywa na Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya zimebaini madhara makubwa ambayo yanapatikana kutokana na biashara ya dawa za kulevya nchini.
Katika mahojiano maalumu na Michuzi Blog, Kamishna Msaidizi wa Kinga na Tiba katika Mamlaka hiyo Dk.Cassian Nyandindi anafafanua kwa kina kuhusu biashara ya dawa za kulevya , matumizi ya dawa za kulevya na jinsi inavyoleta madhara ya kiafya, kijamii, kiuchumi, kisiasa na kimazingira na Kidiplomasia.


Akifafanua zaidi kuhusu madhara ya kiafya amesema matumizi ya dawa za kulevya husababisha magonjwa mbalimbali yakiwemo ya akili, uraibu, moyo, ini na mapafu. Pia matumizi hayo hayo pia huchangia kuenea kwa maambukizi ya VVU, virusi vya homa ya ini na kifua kikuu(TB) miongoni mwa watumiaji na jamii kwa ujumla. 


Aidha, matumizi hayo yanaweza kufanya mishipa ya damu kusinyaa na inapotokea hali hiyo kwenye ubongo husababisha shinikizo la damu na kiharusi. "Dawa za kulevya hupunguza kumbukumbu, uwezo wa kufikiri na kufanya maamuzi sahihi. Matumizi ya kiwango kikubwa cha dawa za kulevya kuliko alichozoea mtumiaji, husababisha vifo vya ghafla hasa kwa wajidunga.


"Watumiaji wa dawa za kulevya hasa wanawake wajawazito wamekuwa wakijifungua watoto wenye uraibu wa dawa za kulevya na waliodumaa kimwili na kiakili. Madhara mengine ya kiafya ni pamoja na saratani, kupunguza nguvu za kiume, sonona, kukosa usingizi, kukosa hamu ya kula, kuoza meno, vidonda kwenye mfumo wa chakula na mara nyingine vifo.


"Kwa ujumla matumizi ya dawa zakulevya hupunguza umri wa kuishi wa mtumiaji kutokana na maradhi, uhalifu au kuzidisha dawa anayotumia,"amesema Dk.Nyandindi huk akitumia mifano mingi rahisi ya kuelezea madhara yanayopatikana kutokana na matumizi ya dawa za kulevya.


Wakati kwa upande wa kijamii, anasema matumizi ya dawa za kulevya husababisha kukithiri kwa vitendo vya kihalifu katika jamii kama wizi, ukahaba, utapeli na uporaji ambayo hufanyika ili kupata fedha za kununulia dawa hizo. Kwa wafanyabiashara wa dawa za kulevya hulinda biashara zao kwa kutoa rushwa kubwa hivyo kuzuia kufikishwa kwenye vyombo vya dola au vyombo hivyo kutotenda haki, hali inayosababisha tatizo la dawa za kulevya kuongezeka kwenye jamii. 

Ameongeza wauzaji wa dawa za kulevya wana kawaida ya kujihusisha na biashara nyingine haramu kama biashara ya binadamu ambapo huwaweka watu rehani (bondi).Pia wafanyabiashara wa dawa za kulevya huweza kuvuruga usalama kwa kufadhili vita na ugaidi. 


Aidha amesema mahusiano katika familia huvurugika ambapo ndoa huvunjika na watoto hutelekezwa na iwapo mtoto ni mtumiaji huacha au hufukuzwa shule, hufukuzwa nyumbani na kuishi kwenye magheto ambako hubobea kwenye matumizi ya dawa za kulevya na uhalifu. 


"Mtakumbuka kuna familia moja ya kitanzania ilikamatwa nchini China miaka ya nyuma kidogo kwa tuhuma za kukutwa na dawa za kulevya, ambapo baba na mama walifungwa na mtoto akarudishwa nchini Tanzania.Huo ni moja ya mfano wa jinsi dawa za kulevya zinavyovuruga mahusiano ya kifamilia.Kuna familia baba anatumia dawa za kulevya na mama hatumia na matokeo yake nyumba inakuwa ya kupigana mapanga tu,"amesema.


Madhara mengine kwenye jamii ni kuongezeka kwa maambukizi ya VVU, homa ya ini na kifua kikuu katika jamii kutoka kwa watumiaji ambao huwa na kiwango kikubwa cha maambukizi ya maradhi hayo. "Unyanyapaa kwa watumiaji husababisha wakose haki zao za kifamilia na kijamii na hata pale wanapoacha matumizi ya dawa za kulevya familia zao au waajiri hushindwa kuwakubali".
Kwa upande wa kiuchumi, Dk.Nyandindi amesema matumizi ya dawa za kulevya hudhoofisha afya za watumiaji na kupunguza ufanisi wao kazini au kwenye masomo na wale ambao hawana ajira kutoweza kupata ajira kutokana na kuathiriwa na dawa za kulevya (Uraibu).


Hivyo kuleta umaskini kwake mtumiaji, jamii yake na taifa kwa ujumla. Pia biashara wa dawa za kulevya husababisha mfumuko wa bei na kuondoa mizania ya ushindani wa kibiashara kwa kuwa uwezo wa kununua bidhaa kwa bei ya juu kuliko bei ya kawaida ya soko hivyo kuwakosesha wengine fursa na kuongeza pengo la kipato kati yao na wananchi wa kawaida hali inayosababisha umaskini. 


"Dawa za kulevya huambatana na utakatishaji wa fedha haramu zinazotokana na biashara hiyo ambapo madhara yake ni pamoja na kuhamisha nguvu ya kifedha kutoka kwenye Serikali, masoko na wananchi na kwenda kwa wahalifu ambao ni wafanyabiashara wa dawa za kulevya. Pia utakatishaji fedha huathiri taasisi za kifedha kama vile benki pale mhalifu anapoamua kutoa fedha zake kwa mkupuo ambapo mara nyingi huwa ni kiasi kikubwa na hivyo kuiacha taasisi ya kifedha ikiyumba na kuzorotesha ukuaji wa uchumi.


"Jamii na Serikali huingia gharama zisizo za lazima kwa ajili ya ukamataji, matibabu ya waraibu, kutoa elimu ya kupunguza matumizi ya dawa za kulevya na kutunza wafungwa gerezani badala ya kuelekeza rasilimali hizo kwenye maendeleo hivyo kurudisha nyuma jitihada za kukuza uchumi wa nchi,"amesema. 


Kuhusu madhara ya kimazingira, amesema kilimo cha bangi na mirungi hufanyika katika maeneo yasiyofikika kirahisi kama vile kwenye milima, misitu na kwenye vyanzo vya maji na hivyo kusababisha kukauka kwa vya vyanzo vya maji, ukame, mmomonyoko wa ardhi na kutoweka kwa baadhi ya viumbe hai na uoto wa asili. 


Ameongeza kwamba uharibifu huo umejidhihirisha katika baadhi ya safu za milima ya Uluguru, Usambara, Udzungwa, Upare na maeneo ya Arumeru. Aidha, watumiaji dawa za kulevya ambao wamekuwa wakitumia njia ya kujidunga wamekuwa wakitupa ovyo mabomba ya sindano yaliyotumika kwenye majalala, vichochoro, viwanja vya michezo, fukwe na vituo vya daladala hivyo kuiweka jamii kwenye hatari ya kupata maambukizi ya magonjwa yanayoambukiza kwa njia ya damu kama VVU na homa ya ini. 


"Katika eneo la kidiplomasia , nako nifafanue kidogo, kuna nchi ambazo mtanzania akienda anapekuliwa kiasi cha kuwa kero na sababu utakuta kuna mtanzania huenda aliwahi kukamatwa na dawa za kulevya,"amesema Dk.Nyandindi.


Hata hivyo amesema pamoja na madhara hayo na mengine Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya kwa kushirikiana na wadau wengine imeendelea kutoa elimu kuhusu madhara ya dawa za kulevya katika makundi mbalimbali ya kijamii ili jamii isijihusishe na matumizi ya dawa hizo.
Ambapo elimu hiyo hutolewa kupitia vyombo vya habari, machapisho, maadhimisho ya kitaifa, semina na makongamano." Upunguzaji wa madhara yanayosababishwa na matumizi na biashara ya dawa za kulevya ni nguzo ya tatu kati ya nguzo kuu nne za kudhibiti na kupambana na tatizo hilo. Nguzo hii inalenga kupunguza madhara yatokanayo na matumizi ya dawa za kulevya ikiwemo uraibu, maambukizi ya VVU, homa ya Ini, Kifua Kikuu.


"Magonjwa ya afya ya akili na kupunguza usugu kwa dawa za kufubaza virusi vya UKIMWI na kifua kikuu pamoja na unyanyapaa kwa watumiaji wa dawa za kulevya. Hivyo kupitia nguzo hii waathirika wa dawa za kulevya wanapata fursa ya kupata tiba ya uraibu na matatizo mengine ya kiafya, sambamba na kuwaunganisha katika jamii na familia zao.Mamlaka kwa kushirikiana na wadau mbalimbali iliendelea kutoa elimu na tiba kwa waathirika wa matumizi ya dawa za kulevya ili kupunguza madhara kwenye jamii.


" Aidha, Mamlaka imekuwa ikifanya usimamizi shirikishi kwa vituo vya kutolea huduma za afya, asasi za kiraia na vikundi mbalimbali vinavyojihusisha na mapambano dhidi ya dawa za kulevya.Tumekuwa tukitoa Tiba ya Methadone ambayo ni maalum kwa ajili ya kuwatibu waraibu wa dawa za kulevya aina ya afyuni pamoja na matatizo mengine ya afya yanayoambatana na uraibu wa dawa hizo,"amesema.


Jitihada nyingine ambazo zimeendelea kuchukuliwa a Mamlaka hiyo ni kuendelea kuanzisha vituo vya afya vya kutolea huduma ya methadone ambayo inahusisha tiba ya uraibu wa dawa za jamii ya afyuni hasa heroin pamoja na magonjwa shirikishi kama vile VVU, Homa ya Ini na Kifua Kikuu.
"Waraibu katika vituo hivyo hupata tiba ya magonjwa ya zinaa na elimu ya uzazi, magonjwa ya akili pamoja na magonjwa yoyote ambayo yangeweza kutibiwa katika kituo chochote cha afya cha Serikali. Hadi Desemba, 2019 Serikali ilifanikiwa kufungua jumla ya vituo sita vya kutolea huduma ya Dawa ya Methadone nchini. 


"Vituo vitatu viko katika mkoa wa Dar es Salaam katika hospitali za rufaa za mikoa za Mwananyamala, Temeke na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili. Vituo vingine vitatu vipo katika mikoa ya Mwanza, Mbeya na Dodoma,"amesema.

Akizungumzia makundi ya dawa za kulevya baada ya kuona madhara yake,Dk.Nyandindi amesema hivi "Dawa za kulevya ni kemikali ambazo mtu akizitumia huathiri mfumo wa fahamu na hasa ubongo, kiasi kwamba anakuwa na shida katika hisia, fikra na tabia.


"Kwa hiyo ubongo unaathirika na ukiathirika vitu vitatu ndio huonekana moja kwa moja, hisia huwa na matatizo, fikra inakuwa inaleta shida lakini anakuwa na tabia ambayo haikubaliki katika jamii inayomzunguka.Ukimuangalia muathirika wa dawa za kulevya mara nyingi kinachoonekana ni tabia yake imebadilika, huenda utamuona anakokota makopo, anapiga watu, anakuwa mwizi , mchafu, anatumia lugha ambazo si za kawaida.


"Kwa hiyo jamii inaona tu mabadiliko hayo lakini kiuhalisia dawa zinakuwa zimeathiri ubongo kiasi kuanzia hisia, fikra zake zinamtuma tofauti.Dawa za kulevya ndio zinabadilisha mambo matatu na tabia anazozifanya hazikubali katika jamii,"amesema.


Aidha amesema kitalaamu wanaangalia makundi ya dawa za kulevya katika mitazamo miwili, kuna waoziangalia kwa kuziweka katika makundi kulingana na uzalishaji ambapo kuna makundi makubwa matatu.Kundi la kwanza dawa za kulevya halisia zinazotokana na mazao kama bangi na mirungi.
"Kundi la pili dawa za kulevya ambazo zinachanganya kemikali na mazao halisia na kisha kupata dawa za kulevya na kundi la tatu ni dawa za kulevya zinazotengenezwa kiwandani kwa kemikali ambazo zenyewe hazina mimea bali ni kemikali za viwandani peke yake.


"Lakini kuna aina nyingine ya kugawa makundi ya dawa za kulevya kwa kuangalia hivi huyu mtu akitumia dawa za kulevya madhara yake yanakuaje? Hivyo tunaziangalia kwa jinsi zinazovyoleta madhara mwilini na hapo kuna makundi matatu.Kundi la kwanza ni Kupumbaza, kundi pili la Vichagamshi, na kundi la tatu la Vileta njozi, sasa katika haya makundi matatu kwenye vipumbaza ina maana mtu anapokuwa ametumia dawa za kulevya zinakwenda kuathiri mifumo yote ya mwili, inapumbazika, inakwenda kufanya kazi chini ya kiwango. 


"Mfano sisi katika hali ya kawaida tunapumua kati ya mara 16 na 20 kwa dakika moja, kwa hiyo anayetumia kipumbaza atakuwa anapumua chini ya 16.Mifano yake ukienda kwenye kituo cha daladala ukamkuta teja ambaye ametumia dawa kupumbaza itakuwa rahisi kumjua, atakuwa amezubaa, hata kama anapiga debe matamshi yake atakuwa anayatamka kiuteja uteja maana zile dawa zinakuwa zimempumbaza.


"Kundi la Vichangamshi, hizi mtu akitumia ile mifumo yote ya mwili inakuwa inafanya kazi kuliko kawaida na hapa mifano mizuri ni kwa mtu anayetumia Cocaine na mirungi na huyu mifumo yote ya mwili inakuwa juu, kwa mfano nilisema kupumua inakuwa kati ya 16 kwa 20 kwa dakika huyu atakuwa anapumza zaidi,"amefafanua.


Wakati kndi la Vileta chonzi, ni zile dawa ambazo mtu akizitumia anaanza kupata hisia pasipo na uhalisia."Mtu anaweza kukaa hapa akajikuta anapata hisia tofauti na uhalisia , wakati tunajifunza somo la Baiolojia tulijifunza milango mitano ya fahamu ambayo ni Kuona, Kusikia, Kunusa, Ladha na Kugusa.


"Kwa hiyo yeye anapata hisia tofauti na uhalisia, anaweza kukaa peke yake akaanza kupiga kilele akidai anamuona Simba na hao mara nyingi ni wale wanaovuta bangi.Anaweza kusema anasikia sauti ya babu yake na anamtaja kwa jina kabisa na anaweza kwenda chooni hatoki kumbe ile harufu anayoipata kwake anaona raha,"amesema Dk.Nyandindi.



Kamishna Msaidizi wa Kinga na Tiba kutoka Mamlaka ya Kudhibiti na Kupmbana na dawa za kulevya Cassian Nyandindi akifafanua jambo wakati akielezea madhara yanayotokana na matumizi ya dawa za kulevya

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 1 mpaka sasa

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...