Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-Tamisemi,  Selemani Jafo ameiagiza Mikoa ambayo Halmashauri zake zimekusanya mapato chini ya asilimia 50 kufanya tathmini na kuweka mikakati madhubuti katika ukusanyaji wa mapato katika vipindi vilivyosalia.

Waziri Jafo ameyasema hayo leo wakati akitoa taarifa ya ukusanyaji wa mapato ya ndani ya halmashauri kwa kipindi cha robo ya pili ya mwaka wa fedha 2020/21 kwa kujumuisha taarifa ya mapato yanayotokana na vyanzo vya ndani vya Halmashauri kuanzia Julai hadi Desemba, 2020.

Waziri Jafo amesema wakurugenzi wa Halmshauri  zote ambazo hazijafikia asilimia 50 ya makisio kwa kipindi hiki cha nusu mwaka wanatakiwa kujitathmini na kuweka mikakati mizuri ya kufikia malengo  katika ukusanyaji wa mapato.

Ameendelea kusisitiza kuwa kila Halmashauri kuendelea kutumia kwa usahihi mifumo ya kielektroniki ya ukusanyaji wa mapato ya ndani na mifumo ya uhasibu ili kutoa taarifa kwa kufuata matakwa ya kisheria na kuzingatia viwango vya Kimataifa vya Uhasibu katika Sekta za Umma (IPSAS).

Akizungumzia ukusanyaji wa Mapato hayo Waziri Jafo ameeleza kwa mwaka  wa fedha 2020/21 Halmashauri zilipanga kukusanya Shilingi Bilioni 814.96 kutoka kwenye vyanzo vyake vya ndani katika kipindi cha Julai, 2020 hadi Desemba, 2020 Halmashauri  zimeweza kukusanya  jumla ya shilingi bilioni 381.27 sawa na  asilimia 47.

Amefafanua kuwa taarifa za mapato ya vyanzo vya ndani vya Halmashauri katika kipindi cha Julai - Desemba, 2020 imeonesha uwepo wa ongezeko la mapato yaliyokusanywa kuwa ni shilingi bilioni 24.5 ikilinganishwa na kiasi kilichokusanywa katika kipindi kama hicho cha Julai - Desemba, 2019 sawa na ongezeko la asilimia 7.

Waziri Jafo ameongeza kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Masasi imeongoza kwa kukusanya mapato kwa asilimia 88 ya makisio yake ya mwaka wakati Halmashauri za Wilaya za Kishapu na Longido zikiwa za  mwisho kwa kukusanya chini ya asilimia 20 ya makisio yake ya mwaka.

Katika kuzipima Halmashauri zote kwa kigezo cha wingi wa mapato (pato ghafi), Halmashauri ya Manispaa ya Ilala imekusanya mapato mengi zaidi kuliko Halmashauri zote kwa kukusanya shilingi bilioni 30.67 na Halmashauri ya Wilaya ya Itilima imekusanya mapato kidogo kuliko Halmashauri zote kwa kukusanya Shilingi Milioni 324.89.

Hata hivyo katika ukusanyaji wa mapato ya Halmashauri Kimkoa kwa kuzingatia asilimia ya makusanyo Waziri Jafo amebainisha kuwa Mkoa wa Katavi umefanya vizuri katika ukusanyaji wa mapato ya ndani ambapo umekusanya kwa wastani wa asilimia 62 ya makisio ya mwaka ya Halmashauri za Mkoa huo wakati Mkoa wa mwisho kwa kigezo hicho ni Mkoa wa Simiyu ambao umekusanya wastani wa asilimia 36 ya makisio ya mwaka ya Halmashauri za Mkoa huo.

Katika hatua nyingine Waziri Jafo ameweka wazi Ukusanyaji wa Mapato ya Ndani ya Halmashauri Kimkoa kwa Kuzingatia Wingi wa Mapato kuwa Mkoa wa Dar es Salaam umefanya vizuri kwa kigezo cha wingi wa mapato   ambapo imekusanya kiasi cha Shilingi Bilioni 89.13 huku Mkoa wa mwisho katika wingi wa mapato ni Mkoa wa Rukwa ambao umekusanya Shilingi Bilioni 4.07.

 Vile vile Ukusanyaji wa mapato kwa Halmashauri kwa Kuzingatia aina ya Halmashauri kwa Kigezo cha asilimia ya makusanyo ukilinganisha na makisio  ya mwaka Waziri Jafo amesema kwa upande wa Majiji Halmashauri ya Jiji la Mwanza imeongoza kwa kukusanya mapato kwa asilimia 50 ya makisio yake ya mwaka na Halmashauri ya Jiji la Dodoma imekuwa ya mwisho katika kundi hili ambapo imekusanya kwa asilimia 39 ya makisio yake ya mwaka.

Halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni imeongoza kundi la Halmashauri za Manispaa ambayo imekusanya asilimia 69 ya makisio yake na Katika kundi hilo Halmashauri ya Manispaa ya Singida imekuwa ya mwisho ambapo imekusanya kwa asilimia 29 ya makisio yake ya mwaka.  

“Kwa kundi la Halmashauri za Miji , Halmashauri ya Mji wa Kahama imeongoza kwa kukusanya kwa asilimia 67 ya makisio ya mapato ya ndani kwa mwaka wa fedha 2020/21 ambapo Halmashauri ya Mji wa Bariadi imekuwa ya mwisho kwa kukusanya asilimia 23 ya makisio ya mapato ya ndani kwa mwaka wa fedha 2020/21” amesema Waziri Jafo

 Aidha, kwa upande wa Halmashauri za Wilaya amesema Halmashauri ya Wilaya ya Masasi imeongoza kwa kukusanya asilimia 88 ya makisio ya mapato ya ndani huku Halmashauri za Wilaya za Kishapu na Longido zimekuwa za mwisho katika kundi hilo kwa kukusanya chini ya asilimia 20 ya makisio ya mapato ya ndani kwa mwaka wa Fedha 2020/21.

“Halmashauri ya Jiji la Dodoma imeongoza kwa kundi la Halmashauri za Majiji kwa kigezo cha wingi wa mapato kwa kukusanya Shilingi bilioni 18.53 na Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam imekuwa ya mwisho katika kundi hili ambapo imekusanya Shilingi bilioni 5.66.” ameeleza Waziri Jafo

Kwa kuongezea Waziri Jafo amesema kwa upande wa Halmashauri za Manispaa,Manispaa ya Ilala imeongoza kwa kukusanya Shilingi bilioni 30.70 na Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma/Ujiji imekuwa ya mwisho katika kundi hili ambapo imekusanya Shilingi Milioni 834.53,

Huku katika kundi la Halmashauri ya Wilaya, Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze imeongoza kwa kukusanya mapato mengi ambapo imekusanya Shilingi Bilioni 4.78. Aidha, Halmashauri ya Wilaya ya Itilima imekuwa ya mwisho katika kundi hili ambapo imekusanya Shilingi Milioni 324.89.

 Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-Tamisemi,  Selemani Jafo

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...