Mbunge wa jimbo la Bumbuli Mkoani Tanga , January Makamba amezishauri taasisi za fedha nchini kuonyesha azma yao ya kuwasaidia wakulima wadogo kwa kuwapa mikopo kwa haki na kwa vitendo ili kuendeleza kilimo nchini.

Akitaja mambo  hayo muhimu manne ambayo alisema yanapaswa kufuatwa ili kufanikisha kilimo cha mkonge na mazao mengine nchini, katika Mkutano wa Wadau wa Zao la Mkonge uliofanyika Tanga, Makamba alisema kuwa ni dhahiri kuwa bila uwezeshaji kifedha hakuwezi kuwa na maendeleo ya maana katika kilimo.

Alisema taasisi za fedha hazitumii haki zinavyotathmini tahadhari katika kutoa mikopo kwa kilimo na kutoa riba kubwa kwa wakulima.

“Kuna tofauti kati ya mtu akienda kuomba mkopo kwa ajili ya kununua mazao akauze nje na mkulima ambaye anataka kulima na aanze kulipa mkopo huo baada ya miaka mitatu,” alisema.

Makamba alisema lazima taasisi ziweze kumtathimini kwa haki mkulima ambaye anachukua mkopo huku akiwa hajui kama mvua itanyesha au la na kama atavuna kama anavyotarajia.

Alisema kuwa taasisi za fedha hazijui kilimo na akazishauri kuandaa watu maalum kuja kujifunza zao la mkonge na kuzitaka kuwa tayari kubadilisha zao la mkonge kuwa 'development financing'. “Nia na azma za watu benki zisiwe za maneno,” alishauri.

Pia Makamba alizungumzia juu ya umuhimu wa serikali kugharamia huduma za ugani katika mkonge ili kufanikisha kilimo hicho.

Alisema kuwa ujuzi katika zao husika ni sharti muhimu katika kuendeleza zao mazao ya kilimo na huduma za ugani ni sehemu muhimu ya sharti la ujuzi katika kilimo. “Kilimo ni sayansi na ndiyo maana serikali inawekeza katika utafiti hivyo kuna umuhimu wa serikali kuwawezesha wakulima kupitia huduma za ugani,”alisema.

Mbunge huyo pia alizungumzia masharti mengine ya kuendeleza zao la mkonge kuwa  ni pamoja haja ya kuwahikishia wakulima soko la uhakika ikiwa pia haja ya wakulima hao kuwa na sauti katika soko hilo na bei ya zao.

Makamba pia alitaja suala la utawala bora katika zao hilo jambo ambalo alisema kuwa serikali imekwisha lishughulikia kikamilifu.

Akizungumzia kuhusu malengo, alishauri kuwa serikali kuweka malengo katika mapato kutokana na mauzo badala ya kusisitiza kuongeza wingi wa uzalishaji kwa kusisitiza juu ya kuongeza thamani na ubora pamoja na kuzalisha bidhaa zitokanazo na mkonge badala ya singa pekee.

Alitoa mfano wa Mexico ambayo alisema kuwa imeweza kupata fedha nyingi kutokana na kuzalisha mazao mengine yatakanayo na mkonge kama kinywaji cha Tequila ingawa uzalishaji wao mkubwa.

Alisema kuwa mwaka jana walipa Dola la Kimarekani 2.6 billioni kutokana na mauzo tequila ingawa haipo miongoni mwa wazalishaji watano bora duniani. Alisema kuwa soko la tequila duniani sasa hivi ni dola za kimarekani Bilioni 5 na hadi kufikia mwaka 2025 litafika dola Bilioni 6.7. “Kama tukiweza kupata hata asilimia moja ya soko hilo tutakuwa tumefanikiwa sana,” alisema.

Kwa upande wake Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, akijibu hoja  kuhusu huduma za ugani, alisema kuwa uzoefu unaonyesha kuwa maofisa ugani waliopo hawana taaluma kuhusu zao la mkonge na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (TARI) kwa maagizo ya Wizara ya Kilimo imeanza kutoa taaluma ya zao hilo kuhusu namna ya kuanzisha, kutambua mabadiliko mbalimbali ya zao hilo na namna mkulima atakavyosimamia zao hilo.

Alisema kuwa serikali itahakikisha kuwa kila sehemu inayolimwa mkonge inakuwa na afisa ugani anayeshughulikia zao hilo.

Kuhusu uhakika wa soko alisema kuwa serikali inashughulikia hilo lakini akasema kwa masikitiko kuwa baadhi ya watu waliomo katika sekta hiyo ndiyo walioshiriki katika kuwafanya watu wengine waache kulima mkonge.

Alisema kuwa kumekuwa na makato mengi na akaahidi kuwa serikali imejipanga kusimamia kuhakikisha kuwa mkulima anapata bei anayostahili.

Alisema kuhusu utawala serikali inaendelea kuimarisha Bodi ya Mkonge ambayo alisema sasa hivi inafanya kazi kwa sheria ya zamani na akaahidi kushughulikia suala hilo.

 Alizitaka taasisi za fedha kufanya mambo ambayo walikubaliana wakati wa mazungumzo yao ili kuendeleza zao hilo.

Alizitaka taasisi kuwafuata wakulima kule walipo badala ya kuwangojea waje kwao.

 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...