Kikosi cha Zimamoto na Uokozi Zanzibar kwa kushirikiana na Viongozi, Wafanyakazi wa Mahoteli na Wananchi wa maeneo jirani wamefanikiwa kuuzima moto mkubwa uliozuka usiku wa  Manane na kuteketeza baadhi ya Majengo ya Hoteli za Ocean Paradise na Tui Blue Bahari zilizopo Pwani Mchangani Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Askari wa Kikosi hicho kutoka Vituo vya Mahonda na Kigunda walifika eneo hilo ndani ya muda wa Dakika 18 baada ya kuibuka tukio hilo liloripotiwa kuanza kutokea majira ya saa 8.33 za Usiku.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla akiambatana na Viongozi tofauti wa Serikali na Wadau wa Sekta ya Utalii walifika eneo hilo la tukio kujionea hali halisi ya hasara iliyotokana na janga hilo pamoja na kuwapa pole Viongozi na Wafanyakazi wa Ocean Paradise na Tui Blue Bahari kwa vile ni wadau wakubwa katika kuchangia Pato la Taifa.

Akitoa Taarifa za awali kuhusiana na tukio hilo Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja Mh. Ayoub Mohamed Mahmoud alisema Wageni wote waliokuwemo kwenye Hoteli hizo mbili wako salama wakati Moto huo ulipoanza kuibuka katika Jengo la Ufundi la Hoteli ya Ocean Paradise.

Naye Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mh. Leila Mohamed Mussa alisema Wageni 208 wa Hoteli ya Ocean Paradise yenye Wafanyakazi 170 na Wageni 129 wa Hoteli ya Tui Blue Bahari yenye Wafanyakazi 300 Wazawa wamehamishiwa Hoteli za Jirani.

Kwa upande wao wakielezea faraja walioipata ndani ya nyoyo zao kutokana na ujio wa Viongozi hao wa Serikali ikiwa ni njia ya kuwapa pole Meneja Mkuu wa Hoteli ya Tui Blue Bahari Bwana Reda Sweed na mwenzake wa Hoteli ya Ocean Paradise Bwana Burnt walisema ushirikiano wa pamoja uliofanikisha kukabiliana na janga hilo wataendelea kuukumbuka katika maisha yao ya baadae.

Imetolewa na Kitengo cha Habari (OMPR)
Januari 16, 2021.

 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...