Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Askofu Mteule wa Kanisa la Kiinjili la  Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, Rev. Dkt. Msafiri Joseph Mbilu, Januari 16, 2021 Ofisini kwake Mlimwa jijini Dodoma. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na uongozi mpya wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, Januari 16, 2021 Ofisini kwake Mlimwa jijini Dodoma. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwa katika picha ya pamoja na uongozi mpya wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, Januari 16, 2021 Ofisini kwake Mlimwa jijini Dodoma. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

**************************************************

 WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameutaka uongozi mpya wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Kaskazini Mashariki inayomiliki chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Sebastian Kolowa (SEKOMU) ukamilishe mahitaji ambayo yataiwezesha Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) kukiruhusu chuo hicho kuendelea na udahili.

Ametoa kauli hiyo leo (Jumamosi, Januari 16, 2021) wakati alipokutana Askofu Mteule wa Dayosisi hiyo Mchungaji Dkt. Msafiri Mbilu pamoja na viongozi wengine wapya waliochaguliwa. Kikao hicho kimefanyika katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Mlimwa.

Waziri Mkuu ameyasema hayo baada ya Askofu Dkt. Mbilu kuiomba Serikali iusaidie uongozi wa Dayosisi hiyo katika kukiwezesha chuo hicho kufunguliwa na kuruhusiwa kufanya udahili. Mwaka 2018 TCU ilikisitishia chuo hicho kufanya masomo na udahili wa wanafunzi katika ngazi zote za masomo baada ya kukosa vigezo.

“Kamilisheni mahitaji yatakayokifanya chuo chenu kiweze kuendelea kufanya udahili. Taarifa niliyonayo ni kwamba TCU walishakuja kukutana nanyi na kufanya ukaguzi, walitoa mahitaji kadhaa ambayo mnapaswa kuyakamilisha na nimesikia mmeridhia na kazi hiyo inaendelea.”

Mbali na maagizo hayo, pia Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kuwashukuru viongozi wa dini nchini kutokana na mchango mkubwa wanaoendelea kuutoa kwa Taifa. “Viongozi wa dini ni watu muhimu sana, nchi imetulia na ina amani, hivyo kuwa kimbilio kwa waliokosa amani makwao.”

Awali, Askofu Dkt. Mbilu alimweleza Waziri Mkuu kwamba Chuo Kikuu cha SEKOMU kimezuiliwa kufanya udahili kutokana na changamoto mbalimbali za kimfumo wa ndani ya Dayosisi na ndani ya chuo ikiwa ni pamoja na kuwa na viongozi wa kukaimu kwa muda mrefu jambo ambalo kwa sasa tayari limeshapatiwa ufumbuzi.

Alitaja changamoto nyingine kuwa ni madeni makubwa yakiwemo ya mishahara ya watumishi, ambapo tayari uongozi umeshaanza kulipa malimbikizo hayo na  wameweka mipango ya kumaliza kulipa madeni hayo. Pia, kiongozi huyo alisema chuo kimeshapata waalimu wa kutosha kwa ajili ya kufundisha wanafunzi mara kitakapofunguliwa.

Askofu Dkt. Mbilu alisema kabla ya kufungiwa Chuo Kikuu cha SEKOMU kilikuwa kinatoa elimu katika nyanja mbalimbali ikiwemo elimu maalumu ya kuwahudumia watu wenye ulemavu katika ngazi ya shahada na shahada ya uzamili, hivyo kimetoa wataalamu wengi.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...