Na Josephine Majura, Mwanza

MAMIA ya wazee wastaafu wanaolipwa pensheni zao na Wizara ya Fedha na Mipango (Hazina), wamejitokeza kuhakikiwa katika Mikoa ya Mwanza, Kagera na Geita, ikiwa ni mkakati wa Serikali wa kuhuisha taarifa za wastaafu hao.

Akizungumza Jijini Mwanza, Mratibu wa zoezi hilo ambaye pia ni Mhasibu Mkuu sehemu ya pensheni kutoka Idara ya Mhasibu Mkuu wa Serikali, Wizara ya Fedha na Mipango Bi. Scola Mafumba, amesema kuwa uhakiki huo umelenga kuhuisha taarifa za wastaafu hao na kuziweka kwenye mfumo wa kieletroniki.

 

Alieleza kuwa zoezi hilo lilianza rasmi tarehe 7 Desemba mwaka 2020 na linatarajiwa kukamilika mwezi Machi mwaka 2021 ambapo mpaka sasa wazee wastaafu katika mikoa 10 ya Tanzania bara wamehakikiwa na kwamba zoezi hilo litafanyika hadi Zanzibar.

 

“Baada ya hapa tutaelekea mikoa ya Shinyanga, Mara na Simiyu kuanzia tarehe 18 Januari, 2021 ambapo kazi tunayoifanya ni kuhakiki na kukusanya taarifa za wastaafu na kuziweka kitaalam ili kuboresha kanzidata ya wastaafu iliyoko Hazina” aliongeza Bi. Mafumba

 

Alisema kwamba zoezi hilo ni la lazima kwa wastaafu wote na kuongeza kuwa Wastaafu ambao hawatahakikiwa wataondolewa kwenye orodha ya malipo ya Pensheni kuanzia Aprili, 2021

 

Aidha, Bi. Mafumba aliwaasa wastaafu kujiepusha ama kujihadhari na matapeli wanaowarubuni kwamba watawasaidia kupata pensheni zao na kuwadai rushwa ambapo amesema huduma za wastaafu zinatolewa bure na Serikali.

 

“Kama kuna mstaafu anataka kupata taarifa zozote zinazohusu mafao yao tunawashauri wafike kwenye ofisi za Hazina Ndogo zilizoko mikoa yote nchini na kamwe wasikubali kutoa fedha zao kwa mtu yeyote kwa sababu huduma za wastaafu zinatolewa bure na Serikali” Alisisitiza Bi. Mafumba.

 

Kwa upande wao, Wazee Wastaafu wameipongeza Serikali kwa hatua wanayochukua ya kuwahakiki na kuboresha taarifa zao ambazo zitakuwa zikipatikana mahali popote kwa njia ya mtandao.

 

Aidha, wameiomba Serikali kuwaongezea pensheni wanayolipwa kila mwezi ili waweze kukabiliana na changamoto za maisha zinazowakabili ikiwemo afya.


Muuguzi Bi. Benta Ragita, akimpa usaidizi Mzee Mstaafu Theones Rutehagwa baada ya kuhakikiwa katika ukumbi wa Hamlashauri ya Jiji la Mwanza, ambapo uhakiki wa wastaafu wanaolipwa na Hazina linaendelea tangu tarehe 11 Januari na linatarajiwa kukamilika tarehe 15 januari, 2021 katika mikoa ya Mwanza Geita na Kagera.

Mtumishi wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bi. Mariana Mahwaya, akimhakiki Mzee Mstaafu Theones Rutehangwa, mkazi wa Mkoa wa Mwanza wakati wa zoezi la uhakiki wa wastaafu wanaolipwa pensheni moja kwa moja na Hazina, linafanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza.

Mtumishi wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Benard Mkude akimhakiki Mzee Mstaafu Ramadhani Simba, mkazi wa Mkoa wa Mwanza wakati wa zoezi la uhakiki wa wastaafu wanaolipwa pensheni moja kwa moja na Hazina, linafanyika katika ukumbi wa Hamlashauri ya Jiji la Mwanza.

 

Akina mama wastaafu wanaolipwa pensheni zao na Hazina, Bi. Sophia Matondo (kulia) na Bi. Mary Ngussa wakihakiki nyaraka zao wakati walipojitokeza kuhakikiwa na maafisa wa Wizara ya Fedha na Mipango katika Ukumbi wa Hamlashauri ya Jiji la Mwanza kwenye zoezi la kuwahakiki wastaafu hao linalofanyika nchi nzima kwa nyakati tofauti

Baadhi ya wazee wastaafu wanaolipwa pensheni zao moja kwa moja na Wizara ya Fedha na Mipango (Hazina) wakisubiri kuhakikiwa katika ukumbi wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza.

Msimamizi wa zoezi la Uhakiki wa Wazee Wastaafu wanaolipwa pensheni zao na Hazina ambaye ni Mhasibu Mkuu Sehemu ya Pensheni Idara ya Mhasibu Mkuu wa Serikali Wizara ya Fedha na Mipango Bi. Scola Mafumba akimpa maelekezo afisa uhakiki kutoka wizarani Bw. Leonard Mbelwa. Katika ukumbi wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza.

Msimamizi wa zoezi la Uhakiki wa Wazee Wastaafu wanaolipwa pensheni zao na Hazina ambaye ni Mhasibu Mkuu Sehemu ya Pensheni Idara ya Mhasibu Mkuu wa Serikali Wizara ya Fedha na Mipango Bi. Scola Mafumba akikagua nyaraka za mmoja wa wastaafu waliojitokeza kuhakikiwa katika ukumbi wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza

Msimamizi wa zoezi la Uhakiki wa Wazee Wastaafu wanaolipwa pensheni zao na Hazina ambaye ni Mhasibu Mkuu Sehemu ya Pensheni Idara ya Mhasibu Mkuu wa Serikali Wizara ya Fedha na Mipango Bi. Scola Mafumba akikagua nyaraka za mmoja wa wastaafu waliojitokeza kuhakikiwa katika ukumbi wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza

(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Wizara ya Fedha na Mipango Mwanza)

 

 

Baadhi ya wazee wastaafu wanaolipwa pensheni zao moja kwa moja na Wizara ya Fedha na Mipango (Hazina) wakisubiri kuhakikiwa katika ukumbi wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza.


Ukumbi wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza ambapo zoezi la uhakiki wa wastaafu wanaolipwa pensheni moja kwa moja na Hazina, linafanyika likihusisha mikoa ya Mwanza, Kagera na Geita, zoezi lililoanza tarehe 11 hadi 15 Januari, 2021.

 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...