Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji Mhandisi Nadhifa S.Kemikimba amezindua Mradi maji wenye Gharama ya Tshs 318,888,222/= kwa jitihada za Serikali kwa kushirikiana na Shirika la Water Mission Tanzania  pamoja na Wananchi wa Kijiji cha Ikombo .

Taarifa  iliyosomwa na Meneja wa RUWASA Wilaya ya Chamwino Mhandisi Christina Msengi imesema mradi huo ulilenga kuwapatia Maji safi na salama wananchi wa Kijiji hicho  ili kuepuka adha ya kutembea umbali mrefu kufuata huduma hiyo.

Kukamilika kwa Mradi huo ni jitihada  za Serikali ya Awamu ya tano chini ya Mhe.Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kupitia RUWASA kuchimba kisima kirefu kwa Tsh 25,000,000 katika bajeti ya 2017/2018, Shirika la Water Mission Tanzania likajenga miundombinu ya usambazaji Maji ya mradi huu kwa gharama ya Tsh. 288,726,222 na Mchango wa Wananchi kuwa Tsh 5,162,000.

"Kwa sasa mradi huu unahudumia watu wapatao 4,047 kati ya 4172  sawa na asilimia  97%. ya kijiji chote, aidha kisima hicho kina uwezo wa kutoa lita 23,400 kwa saa na kuendeshwa kwa mfumo wa nishati ya jua licha ya kuwa na mfumo wenye uwezo wa kutumia Nishati ya Umeme na Upepo (Multipurpose)" Mhandisi Christina. 

Akizungumza kwa niaba ya Shirika hilo, Mkurugenzi wa Shirika la Water Mission Tanzania  Benjamin Filskow alisema mradi huo ni alama ya mahusiano baina ya Serikali ya Tanzania, Shirika Water Mission na wananchi wa Kijiji cha Ikombo, akaeleza umuhimu wa kuilinda mradi huo na kuikumbusha Jumuiya ya Watumiaji Maji kuwa na matumizi mazuri ya fedha inayopatikana katika mradi huo na  akatoa pongezi kwa Wilaya ya Chamwino kusimamia Vizuri miradi ya Maji. 

Mapema kabla ya kumkaribisha  Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji (Mgeni Rasmi), Remidius Emmanuel Afisa Tarafa Itiso ambaye katika tukio hilo alimwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Chamwino Mhe.Vumilia Nyamoga pamoja na kutoa shukrani kwa Shirika la Water Mission, kiongozi huyo alisema Serikali haitasita kuwachukulia hatua kali wale wote watakaojaribu kuharibu miundombinu  ya Maji na akaahidi kupokea maelekezo yote kutoka kwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji kupitia tukio hilo, akamaliza kwa kufikisha salaam za Mbunge wa Jimbo hilo Mhe. Deogratius Ndejembi ambaye Maji imekuwa ni sehemu ya kipaumbele chake.

Akitoa hotuba yake kwa Wananchi wa Kijiji cha Ikombo kabla ya kuzindua rasmi mradi huo, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji Mhandisi Nadhifa alisema kutekelezwa kwa miradi hiyo ni sehemu ya kutimiza malengo ya Serikali ya Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kupitia Sekta ya Maji upande wa Vijijini na  kwamba ifikapo Mwaka 2025 tunatakiwa tuwe tumehudumia wananchi kwa zaidi ya Asimilia 95 (lengo la kitaifa), akasisitiza mpango huo ni kwa maeneo yote, na hivyo viongozi ngazi zote watekeleza mpango huo kupitia maeneo yao.

Aliwashukuru sana Water Mission kwa kuendelea kutoa ushirikiano katika Sekta hii muhimu ya maji na kuwapongeza Wananchi wa Ikombo kwa kuupokea vizuri mradi huo pamoja na kushiriki kikamillifu kuchangia nguvu  kazi  na kwa kufanya hivyo wananchi hao wameelewa malengo na nia  ya Mhe. Rais Dkt. Magufuli. 

" Ni lazima kuwa na mipango endelevu ya kuhifadhi mradi huu, mtunze miundombinu, makusanyo mpate taarifa zake na RUWASA muwe karibu kukagua taarifa hizo, mpange miradi ya maendeleo kutokana na mradi huu wa maji" Mhandisi Nadhifa

Alipongeza hatua ya Shirika la Water Mission kutoa mafunzo kwa Vijana kijijini hapo juu ya namna kuendesha mitambo ya kusukuma maji lakini akasisitiza iandaliwe miongozo maalum ya  matumizi ya mitambo hiyo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kijiji cha Ikombo  Juma Madeje alisema kukamilika kwa mradi huo kumewezesha wananchi wa Kijiji hicho kutumia muda mwingi katika shughuli za maendeleo tofauti na zamani kabla ya mradi huo na sasa wanapata Maji Safi na Salama.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji Mhandisi Nadhifa S. Kemikimba akizungumza na Wananchi wa Kijiji cha Ikombo, Wilayani Chamwino wakati wa Uzinduzi wa mradi wa Maji Kijijini hapo.
Mkurugenzi wa Shirika la Water Mission Tanzania Ndugu Benjamin Filskow akitoa salaam na ujumbe kutoka Shirika hilo wakati wa uzinduzi wa Mradi maji wenye Gharama ya Tshs 318,888,222/= uliofanikiwa kwa jitihada za Serikali kwa kushirikiana na Shirika la Water Mission Tanzania  pamoja na Wananchi wa Kijiji cha Ikombo .

Meneja wa RUWASA Wilaya ya Chamwino Mhandisi Christina Msengi akisoma Taarifa ya Mradi huo mbele ya Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji Mhandisi Nadhifa S. Kemikimba.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji Mhandisi Nadhifa S. Kemikimba (wa kwanza kutoka Kushoto)  akifurahi pamoja na wananchi wa Kijiji cha Ikombo, Wilayani Chamwino wakati wa uzinduzi wa mradi wa Maji Kijijini hapo, kushoto kwake ni AfisaTarafa Itiso Remidius Emmanuel aliyemwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Chamwino katika tukio hilo.Baadhi ya wananchi wakiwa kwenye hafla ya uzinduzi wa Mradi maji wenye Gharama ya Tshs 318,888,222/= uliofanikiwa kwa jitihada za Serikali kwa kushirikiana na Shirika la Water Mission Tanzania  pamoja na Wananchi wa Kijiji cha Ikombo .Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...