Akiongea mbele ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa wakati wa kikao cha
wadau wa Mkonge kilichofanyika jana Mkoani Tanga, Afisa Mkuu wa Wateja Binafsi
na Biashara wa Benki hiyo - Filbert Mponzi, alisema kuwa NMB itaendeleza
jitihada za kufufua zao hilo ambazo imezianza.
Alisema kuwa tangu serikali imeanza kulifufua zao hilo na Benki hiyo
imekuwa ikitoa ushirikiano ambapo imetoa zaidi ya Bilioni 1 kwa ajili ya
ununuzi wa matrekta 11 na trela 22 vifaa ambavyo vitapunguza
gharama ya uendeshaji na kuongeza tija na pato la wakulima wadogo wa mkonge.
Aidha aliongeza kuwa Benki hiyo imeendelea kutoa mikopo ya pembejeo na
uendelezaji wa mashamba ya Mkonge kwa wakulima wadogo, kati na wakubwa ili
kuongeza uzalishaji na mapato ambapo zaidi ya shilingi bilioni 6 zimeshatolewa
kwa wakulima wa mkonge.
Alisema kuwa NMB imefanikisha kufungua akaunti kwa wakulima zaidi ya
1,500 ambapo akaunti hizo zinajumuisha wakulima mmoja mmoja na wale
wanaozalisha kupitia Vyama vya Msingi.
“Uwepo wa akaunti hizi unajenga utamaduni wa wakulima kutumia huduma
za benki kwa usalama wa fedha zao na mazingira sahihi katika kupata huduma
zaidi ya kifedha ikiwemo Mikopo.” Alisema Mponzi.
"Mheshimiwa Waziri Mkuu ili kuendelea kuwajengea uwezo
wakulima wadogo na kupata mitaji NMB kupitia taasisi kanzu ya NMB Foundation
inaendelea kutoa mafunzo kwa wakulima kupitia vyama vya vya msingi na kikundi
ili kuimarisha utendaji na kuongeza soko." Alifafanua.
Mponzi alibainisha kuwa Benki ya NMB itaendeleza jitihada hizo,
ikiwemo kutoa mikopo mikubwa, midogo na ya kati ili kuhakikisha wakulima wa zao hilo wanazlisha kwa tija.
“NMB tutaendelea mikopo katika ngazi zote za uzalishaji wa zao la
mkonge, ikijumuisha mikopo ya muda mfupi na muda wa kati (yaani uwekezaji).
Mikopo hii inajumisha pembejeo, upanuzi na miundo mbinu ya mashamba, matrekta,
mashine za uchakataji wa mkonge, viwanda vya mkonge pamoja na huduma mbalimbali
katika sekta.” Alisema.
Akizungumza katika kikao hicho cha wadau wa zao la Mkonge, Waziri Mkuu
Kassim Majaliwa alisema kuwa mpaka kufikia mwaka 2025 Tanzania inatarajia
kuzalisha tani 120,000 za Mkonge kwa mwaka. Majaliwa alisema kuwa zao la Mkonge
ni miongoni mwa mazao ya biashara hapa nchini ambayo mikakati yake ilitekelezwa
vizuri itawezesha serikali kupata fedha za kigeni lakini pia kukuza pato la
mwananchi mmoja mmoja.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Kilimo Hussein Bashe alisema kuwa kwa
sasa Wizara tayari imeshatenga shilingi Bilioni 175 kwa ajili ya kufanya
utafiti ili kuzalisha mbegu bora na zenye gharama nafuu.
Bashe alisema kuwa Wizara imeweza kuandaa utaratibu wa hati ya dhamana
(LC) utakaowezesha wakulima wadogo kuchukua mkopo kwenye taasisi za fedha kwa
riba ya asilimia mbili tu.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...