MKUU wa Mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme
akizungumza kwenye Kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC,) amewaagiza Mamlaka
ya Usimamizi wa Wanyamapori (TAWA) kupeleka wanyama kwenye kisiwa cha Lundo
ziwa Nyasa wilaya ya Nyasa.
Mndeme amesisitiza kuwa
kupelekwa kwa wanyama katika kisiwa hicho,kutasaidia kuongeza vivutio kwa
watalii kwa lengo la kutangaza vivutio vya utalii vinavyopatikana wilaya ya
Nyasa ambayo imetangazwa kuwa kitovu cha utalii katika Mkoa wa Ruvuma.
Mkuu wa Mkoa pia
aliwaagiza wadau wa utalii na uhifadhi wakiwemo TAWA na TANAPA
kuchukua jukumu la kutoa elimu ya uhifadhi na utalii kwa wananchi hasa
wa Mkoa wa Ruvuma kuhusu umuhimu wa sekta ya utalii katika kuchochea uchumi.
Mndeme pia ameagiza
ushoroba na mapito ya wanyama katika Mkoa wa Ruvuma yaheshimiwe na kulindwa kwa
sababu ni moja ya rasilimali za nchi na ameagiza wananchi wote waliovamia
maeneo hayo waondolewe haraka.
Kufuatia maagizo hayo
wadau wa utalii mkoani Ruvuma wakiwemo TAWA,TANAPA na Wakala wa Huduma za
Misitu Tanzania(TFS) wameanza kuchukua hatua ikiwemo azma ya kuanzisha hifadhi
ya kufuga wanyamapori katika kisiwa cha Lundo,kifuga ndege katika kisiwa cha
Mbambabay(Zambia).
Mshauri wa Maliasili na
Utalii Mkoa wa Ruvuma Afrikanus Challe anasema wanatarajia kuanzisha hifadhi ya
Mbambabay ambayo inajumuisha visiwa vya Lundo,Mbambabay na milima ya
Mbamba,Tumbi na Ndengere wilayani Nyasa.
Challe anaitaja hifadhi
ya Mbambabay itakuwa na ukubwa wa eneo la hekta 597 na kwamba maeneo hayo
yanafaa kwa kufuga wanyamapori na ndege.
Hata hivyo anasema Kati
ya hekta hizo, mlima Mbamba una eneo lenye ukubwa wa hekta40,mlima Tumbi hekta
110,kisiwa Mbambabay chenye hekta 27,kitakuwa maalum kwa ufugaji wa ndege na
kisiwa cha Lundo chenye ukubwa wa hekta 20,TAWA inatarajia kupeleka wanyamapori
jamii ya swala.
“Milima na visiwa hivi
vimejaaliwa kuwa na uoto mzuri wa miombo,mawe yanayozunguka visiwa hivi na
milima kando kando ya ziwa yana hifadhi samaki adimu wa mapambo zaidi ya aina
400’’,anasisitiza Challe.
Kwa mujibu wa
Challe,eneo la hifadhi ya Mbambabay ni muhimu sana kwa upande wa Tanzania hususan katika matumizi ya shughuli za utalii
kama vile utalii wa kuvua samaki,kupiga mbizi,yatching,utalii wa kuendesha
mitumbwi na kuweka kambi kwenye fukwe.
Mtalaam huyo wa
uhifadhi anasema eneo hilo likihifadhiwa litatumika kwa ajili ya mazalia ya
samaki na hivyo kuongeza kipato kwa wananchi wanaotegemea shughuli za uvuvi.
“Mbambabay ikihifadhiwa
inaweza kuleta ushindani kibiashara hapa nchini kwa sababu katika nchi yetu
hakuna eneo linaloweza kutoa mchanganyiko mzuri wa huduma za kitalii kama
zitakazotolewa katika eneo hili’’,anasisitiza Challe.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...