Meneja wa Mamlaka ya mapato(TRA)Mkoa wa Ruvuma Amina Ndumbogani akionesha Tuzo Maalum waliyokabidhiwa na Mamlaka ya mapato Nchini kutokana na utendaji kazi mzuri wa watumishi wa mamlaka hiyo mkoa wa Ruvuma ambao umewezesha kuvuka lengo la kukusanya shilingi bilioni 8.6 kati ya lengo la kukusanya bilioni 7 katika kipindi cha miezi sita kwa mwaka wa fedha 2020/2021, kushoto ni meneja msaidizi Antipas Mrema.


Na Muhidin Amri, Songea

MAMLAKA ya mapato Nchini (TRA) mkoani Ruvuma, imefanikiwa  kukusanya kiasi cha shilingi bilioni 8.442 sawa na asilimia  109 kati ya lengo walilopewa
la  kukusanya shilingi bilioni 7.771  katika kipindi cha miezi sita
kutoka mwezi Julai hadi Desemba 2020.

Hayo yamesemwa na Kaimu Meneja wa Mamlaka hiyo mkoani humo Amina
Ndumbogani, wakati akitoa taarifa ya ukusanyaji wa mapato katika
kipindi cha nusu Mwaka wa fedha 2020/2021 kwa waandishi wa habari
ofisini kwake mjini Songea.

Amesema, katika mwaka wa fedha 2020/2021 TRA mkoani Ruvuma
imepewa lengo la kukusanya shilingi bilioni  15.639, lakini kutokana
na kazi nzuri iliyofanywa na watumishi wa mamlaka hiyo hadi kufika
Desemba 2020 wamefanikiwa kuvuka lengo kwa kukusanya shilingi bilioni
8.4 hivyo kuwa na matumaini ya kufika lengo la kukusanya shilingi
bilioni 15.6

Alisema, mbali na kazi nzuri iliyofanywa na watumishi pia mafanikio
hayo yametokana  na ushirikiano waliopata kutoka kwa  wadau wengine
wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa huo Christina Mndeme na wakuu wa Wilaya
tano za mkoa wa Ruvuma pamoja na kamati ya ulinzi na usalama ambayo ni
sehemu ya mafanikio hayo.

Alisema, anajivunia kuona  wadau mbalimbali  wakiongozwa na Mkuu wa
mkoa wa Ruvuma Chritina Mndeme,Wakuu wa wilaya za mkoa huo na
wafanyabiashara  walivyofanikisha malengo ya Mamlaka  hiyo kuvuka
malengo  katika kipindi cha nusu mwaka kutoka mwezi Julai hadi Desemba
2020.

Aidha alisema, kwa mwaka  huu wa fedha wameweka malengo mbalimbali
kama mkakati wa kukusanya shilingi bilioni 15 walizopewa ambayo ni
kupanua wigo kwa kuwatambua na kuwasajili wafanya biashara kwa  mfumo
wa mtandao, kupita  mlango kwa mlango ili kuwabaini walipa kodi na wale
wanaokwepa kulipa kodi na kuongeza nguvu kwa wafanyabiashara kuhusu
matumizi ya mashine za Efds.

Alisema, mbali na hilo mkakati mwingine ni  kuwafuatilia walipa kodi
wenye madeni  ili kulipa  madeni yao kwa wakati kabla ya hatua za
kisheria hazijachukuliwa dhidi yao.

“kazi ya kukusanya kodi ni ngumu sana, lakini kutokana na jitihada
kubwa zilizofanyika na wadau wengine kwa kweli ndiyo kwa kiasi kikubwa
waliofanikisha malengo hayo.” Alisema Amina.

Alisema, mamlaka ya mapato inaendelea kuwakumbusha wafanya biashara na wananchi wote kwa jumla  kuwa msingi wa makadirio ya kodi kwa haki ni
utunzaji sahihi wa kumbukumbu na ni wajibu na  kila mwenye sifa kulipa
kodi stahiki za Serikali.

Amina ameonya kuwa, mfanyabiashara yeyote atakayebainika kutotumia
vyema mashine za kielektroniki  katika biashara yake au kukaidi
kutimiza wajibu huo wa kisheria atakuwa ametenda kosa na atachukuliwa
hatua kali za kisheria.

Alisema, mfanyabiashara atakayekamatwa kwa kosa la  kutotumia mashine
za Efds adhabu yake ni faini  kuanzia milioni 3 na isiyozidi milioni
4.5  au kifungo cha miaka mitatu jela au vyote kwa pamoja kwa mujibu
wa sheria za usimamizi wa kodi ya mwaka 2015.

Pia, amewataka wanunuzi wote wa bidhaa mbalimbali kuhakikisha wanadai
risiti pindi wafanyapo manunuzi  kwani ni haki ya msingi na kisheria
kwa kila mnunuzi, na kutofanya hivyo ni kosa linaloweza kupelekea
kupata adhabu kali ikiwemo kutozwa faini kati ya shilingi 30,000 hadi
milioni 1.5.

Alisema, TRA inategemea sana ushirikiano kutoka kwa wadau wote  katika
suala zima la kukusanya mapato ya Serikali na kusisitiza,ni wajibu wa
kila mwananchi kuonyesha uzalendo kwa kulipa kodi ili kuisaidia
Serikali kutoa huduma bora na haraka zaidi.

Amina amesisitiza kuwa,  ni haki na lazima kwa mwananchi kudai risiti
sahihi kila anunuapo bidhaa au huduma pamoja na kutoa taarifa ya
upotevu wa mapato ili kuiwezesha mamlaka hiyo kutekeleza majukumu yake
kwa ufanisi katika kuwahudumia Watanzania.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...