Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu), Jenista Mhagama, Naibu wake, Patrobas Katambi na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Andrew Massawe, wakiwa katika kikao ambacho Taasisi chini ya Wizara ziliwasilisha taarifa kuhusu miundo na majukumu mbele ya Kamati ya Katiba na Sheria.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu), Jenista Mhagama, akifafanua jambo katika kikao cha Kamati ya Katiba na Sheria ambapo Taasisi chini ya Wizara yake ziliwasilisha taarifa kuhusu miundo na majukumu yao.
Kaimu Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda, akiwasilisha taarifa kuhusu muundo na majukumu ya Taasisi yake mbele ya Kamati ya Katiba na Sheria.

Wajumbe wa Kamati ya Katiba na Sheria wakifuatilia kikao ambacho Taasisi chini ya Wizara ya Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu ziliwasilisha taarifa kuhusu miundo na majukumu yao.

KAMATI ya Bunge ya Katiba na Sheria imeeleza kuridhishwa kwake na maboresho yaliyofanywa na Taasisi mbali mbali zilizopo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu-Kazi, Vijana, Ajira na wenye ulemavu katika kuwahudumia wananchi kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita.

Kauli hiyo ya Kamati imetolewa na Mwenyekiti wa kamati hiyo, Mohamed Mchengerwa, mara baada ya kuhitimisha kikao cha kamati hiyo kilichopokea na kujadili taarifa kuhusu miundo na majukumu ya Taaasisi mbali mbali chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu.

Mchengerwa amesema katika vikao hivyo wamekutana na wizara mbali mbali ikiwemo Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu) pamoja na Taasisi zake.

“Tumekuwa na mfululizo wa vikao vya kamati na tumekutana na Wizara na Taasisi mbali mbali ikiwemo Ofisi ya Waziri Mkuu kwa ajili ya kujadili muundo na majukumu ya ofisi hiyo. Kupitia taarifa zilizowasilishwa tumejionea namna ambavyo utendaji umeboreka ikilinganishwa na hali ilivyokuwa miaka mitano iliyopita (2015-2020) hivyo tunaipongeza Wizara na Taasisi zake kwa kazi nzuri ambayo imeendelea kufanyika,” alieleza Mwenyekiti wa Kamati.

Alifafanuwa kuwa kwasasa Taasisi nyingi zimejiimarisha ambapo alitolea mfano Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) na kueleza kuwa ni Taasisi ambayo imefanya kazi kubwa katika kuimarisha masuala ya Usalama na Afya mahali pa kazi hapa nchini kupitia uboreshaji wa mifumo yake ya utendaji. 

Kwa mujibu wa Kiongozi huyo wa Kamati ya Katiba na Sheria ambaye pia ni Mbunge wa Rufiji amesema walitumia kikao hicho kuweka mipango na mikakati ya kuendelea kuzishauri Taasisi wanazozisimamia namna bora zaidi ya kuendelea kuboresha utendaji wake.

Baadhi ya wajumbe wa Kamati hiyo wameipongeza Wizara inayoshughulikia Masuala ya Kazi chini ya Waziri Jenista Mhagama pamoja Taasisi husika ambazo ni Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA), Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) na Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA) kwa kufanya mageuzi makubwa katika mifumo na taratibu zake kiutendaji ambayo yamepelekea kuboresha huduma kwa wananchi.

“Leo tumepata mada nzuri sana kutoka kwa menejimenti ya OSHA kwasababu sote tunakwenda kazini ambako athari mbali mbali zitokanazo na mazingira ya kazi ambayo si rafiki zinaweza kutokea hivyo kupitia maelezo hayo tumeona njinsi ambavyo OSHA imejipanga kulinda nguvu kazi ya Taifa letu,” alisema Asha Abdallah Juma ambaye ni mjumbe wa Kamati ya Katiba na Sheria.

Kwa upande wake Yahaya Massare, Mjumbe wa Kamati ya Katiba na Sheria na Mbunge wa Manyoni Magharibi amesema hatua ya OSHA kufuta baadhi ya tozo zake ambazo zilionekana kuwa kero kwa wamiliki wengi wa sehemu za kazi, imepelekea mwitikio mkubwa wa wadau katika kutekeleza Sheria ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi ya mwaka 2003.

Vikao hivyo vya Kamati mbali mbali za kudumu za Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambavyo vilianza kufanyika tangu Januari 18, 2021, vinafanyika muda mfupi kabla ya kuanza rasmi kwa vikao vya Bunge la 11 ambavyo vinatarajiwa kuanza kufanyika kuanzia Februari 2, 2021.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...