Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akimkabidhi Hati ya Ardhi mkazi wa Mwanza Charles Maningu wakati wa zoezi la utoaji hati kwa wamiliki wa ardhi katika mkoa huo tarehe 26 Januari 2021.

 

Sehemu ya Watendaji wa sekta ya ardhi katika mkoa wa Mwanza wakimsikiliza Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula (hayupo pichani) wakati wa ziara ya kukagua utendaji kazi wa sekta ya ardhi na kuhamasisha ukusanyaji kodi ya pango la ardhi tarehe 26 Januari 2021.
Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana katika mkoa wa Mwanza Dkt Phillis Nyimbi akizungumza wakati wa kikao cha kazi baina ya Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Angeline Mabula (Katikati) na watendaji wa sekta ya ardhi katika mkoa huo wakati wa ziara ya kukagua utendaji kazi wa sekta ya ardhi na kuhamasisha ukusanyaji kodi ya pango la ardhi tarehe 26 Januari 2021. Kushoto ni Kaimu Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Mwanza Eliah Kamyanda.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe Dkt Angeline Mabula akiwa katika picha ya pamoja na wananchi wa mkoa wa Mwanza aliowakabidhi Hati za Ardhi wakati wa ziara ya kukagua utendaji kazi wa sekta ya ardhi na kuhamasisha ukusanyaji kodi ya pango la ardhi tarehe 26 Januari 2021. Wa pili kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Dkt Phillis Nyimbi na kulia ni Msajili wa Hati Msaidizi Ofisi ya Ardhi mkoa wa Mwanza Ivan Amurike.
Baadhi ya wananchi wa mkoa wa Mwanza wakikamilisha taratibu za kupatiwa Hati za Ardhi kabla ya kukabidhiwa na Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Mwanza wakati akiwa katika ziara ya siku moja katika mkoa huo tarehe 26 Januari 2021. (PICHA ZOTE NA MUNIR SHEMWETA WIZARA YA ARDHI.)


 

Na Munir Shemweta, WANMM MWANZA

 

NAIBU Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula amewaambia Watumishi wa Sekta ya Ardhi katika mkoa wa Mwanza kuwa, Wizara ya Ardhi itaanza kuwapima Wakuu wa Idara za Ardhi kwenye halmashauri kwa kuangalia utekelezaji wa majukumu yao ikiwemo ukusanyaji maduhuli ya serikali kupitia kodi ya pango la ardhi.

 

Dkt Mabula alitoa kauli hiyo tarehe 26 Januari 2021 jijini Mwanza wakati akizungumza na Wataalamu wa sekta ya ardhi katika mkoa huo akiwa katika ziara ya siku moja kukagua utendaji kazi wa sekta ya ardhi na kuhamasisha ukusanyaji maduhuli ya serikali kupitia kodi ya pango la ardhi.

 

Naibu Waziri wa Ardhi alisema, kwa sasa wizara inataka kuona ushindani katika ukusanyaji kodi ya pango la ardhi na wakuu wa idara wanalo jukumu kubwa la kuhakikisha fedha ya kodi ya ardhi inapatikana kwa watendaji hao kuzingatia sheria wakati wa kutekeleza majukumu yao.

 

"Naagiza watendaji wa sekta ya ardhi mkasimamie sheria hususan katika ukusanyaji kodi ya ardhi, nataka ushindani katika makusanyo ya kodi ya pango la ardhi na msimuonee mtu wakati wa utekelezaji majukumu yenu" alisema Dkt Mabula.

 

Aidha, Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Mabula aliwakumbusha watendaji wa sekta  kuhakikisha wanafikia malengo ya makusanyo ya kodi ya ardhi kwa kufuata sheria ikiwemo kuwafikisha kwenye Mabaraza ya Ardhi ya Nyumba na Wilaya wadaiwa sugu.

 

"Mkoa wa Mwanza hamjafanya vizuri katika makusanyo ya kodi ya ardhi, bado mko nyuma sana, asilimia 28 ya malengo na tunafikia nusu mwaka sasa ni ndogo sana na ni aibu kwa mkoa wakati mnadai takriban bilioni 70 nje" alisema Dkt Mabula.

 

Katika hatua nyingine, mkoa wa Mwanza katika kipindi cha mwezi Julai 2020 hadi Januari 22, 2021 umefanikiwa kutoa  jumla ya Hati za Ardhi 7,022.

 

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula alisema, wilaya inayoongoza kwa utoaji hati katika mkoa huo ni Ilemela iliyotoa Hati 3,212 ikifuatiwa na Jiji la Mwanza 2441, Magu 458, Misungwi Hati 336, Sengerema 216 na Ukerewe 203 huku wilaya ya Buchosa ikitoa jumla ya Hati  52.

 

Kwa mujibu wa Dkt Mabula, takwimu katika mkoa wa Mwanza zinaonesha kuongezeka kwa kasi ya utoaji Hati katika mkoa huo.

 

Hata hivyo, alisema pamoja na kuongezeka kwa kasi ya utoaji Hati bado muitikio wa uchukuaji hati kwa wamiliki umekuwa mdogo ukilinganisha na uandaaji hati na kutolea mfano wamiliki waliojitokeza kuchukua hati wakati wa zoezi la utoaji hati ni 22 huku idadi ya hati zilizoandaliwa ikiwa ni 142.

 

Naibu Waziri Mabula aliwataka wamiliki wa ardhi ambao hati zao zimekamilika kujitokeza kuzichukua na kuongeza kuwa, sasa wamiliki wamerahisishiwa utaratibu wa kupatiwa hati ambapo badala ya kuzifuata ofisi ya Msajili wa Hati Msaidizi mkoa wanapelekewa katika halmashauri zao. Kaimu Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Mwanza Eliah Kamyanda alisema ofisi yake imeanza kutekeleza suala hilo kwa kupanga siku maalum za kupeleka hati katika halmashauri husika.

 

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Dkt Phillis Nyimbi  ameishukuru wizara ya Ardhi kwa kujipanga katika kuhakikisha huduma katika sekta ya ardhi zinatolewa kwa ufanisi na kubainisha kuwa sasa katika wilaya yake kuna muitikio chanya wa wananchi kutaka kumilikishwa ardhi ukilinganisha na miaka ya nyuma.

 

"Wananchi wanapomilikishwa ardhi hata suala la ulipaji kodi ya pango la ardhi litafanyika kwa ufanisi kwa kuwa kumbukumbu za wamiliki zinafahamika" alisema Dkt Phillis Nyimbi.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...