WAZIRI JAFO ALIPA WIKI MBILI JIJI LA DODOMA KUFANYIA MABORESHO SHULE YA MSINGI NKUHUNGU

Charles James, Michuzi TV

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais-Tamisemi, Selemani Jafo ameliagiza Jiji la Dodoma chini ya Mkurugenzi wake Joseph Mafuru kuifanyia ukarabati Shule ya Msingi Nkuhungu pamoja na kuhakikisha inafikisha ufaulu wa asilimia 100 kwenye matokeo ya mitihani ya darasa la nne.

Jafo ametoa kauli hiyo leo jijini Dodoma wakati alipofanya ziara yake ya kukagua miundombinu ya shule hiyo pamoja na barabara ya Jamhuri na barabara ya Nkuhungu-Swai.

Kwenye barabara ya Jamhuri Waziri Jafo ameeleza kufurahishwa na ukamilikaji wa barabara hiyo ya kilomita moja iliyogharimu kiasi cha Sh Bilioni Moja huku akimuagiza Mratibu wa TARURA Mkoa wa Dodoma, Mhandisi Lusako Kilembe kuhakikisha barabara ya Nkuhungu Swai yenye ukubwa wa kilomita moja itayogharimu Sh Milioni 800 inakamilika ndani ya muda uliopangwa ambao ni Juni mwaka huu.

Akizungumza na viongozi wa Mkoa, Jiji, Walimu na Wanafunzi wa Shule ya Msingi Nkuhungu, Waziri Jafo ameuagiza uongozi wa Jiji la Dodoma kuhakikisha madarasa yote ambayo paa lake limeharibika kufanyia matengenezo huku pia akiagiza darasa la awali nalo kufanyiwa maboresho na kuwa la kisasa.

" Ninafurahishwa na kazi kubwa inayofanywa na Jiji la Dodoma lakini Mkurugenzi wa Jiji tenga angalau kiasi cha Sh Milioni 25 au 30 kwa ajili ya kufanyia matengenezo shule hii ambayo inabeba wanafunzi wengi sana, ninatoa wiki mbili hadi kazi iwe imekamilika hapa na mimi Februari 20 nitakuja tena kuikagua.

Nimeamua kuwa mlezi wa Shule hii hivyo ninataka iwe na muonekano wa kuvutia na kiwango chake cha ufaulu kiwe juu, matokeo ya darasa la nne ufaulu wake ni asilimia 91 ninataka iwe mwisho sasa kiwango kifikie asilimia 100 hivyo Jiji na uongozi wa Shule muangalie namna ya kuboresha ufaulu," Amesema Waziri Jafo.

Akitoa maelekezo yake kwenye miundombinu ya barabara, Waziri Jafo ameagiza TARURA kuhakikisha wanapanda miti ya matunda kwenye barabara zote nchini lengo likiwa ni kutunza mazingira lakini pia kupendezesha mandhari za barabara nchini.

" Nimeridhishwa na barabara ya Jamhuri kazi yake ni nzuri, lakini hii ya Nkuhungu Swai bado kasi yake siyo kubwa niwataka TARURA kuhakikisha mkandarasi anakamilisha kazi yake ndani ya muda uliopangwa bila kisingizio chochote.

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini, Anthony Mavunde ameahidi kutoa kiasi cha Sh Milioni 70 za mfuko wa Jimbo kwa ajili ya kununua madawati lengo likiwa ni kuondoa changamoto ya madawati kwenye shule za jiji la Dodoma na kuunga mkono juhudi za Rais Dk John Magufuli za kutoa elimu bila malipo.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-Tamisemi, Selemani Jafo akiagana na wanafunzi wa Shule ya Msingi Nkuhungu jijini Dodoma baada ya kumaliza kuongea nao alipofanya ziara ya kikazi shuleni hapo.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-Tamisemi, Selemani Jafo akizungumza na viongozi wa Mkoa wa Dodoma, Jiji la Dodoma, Walimu na Wanafunzi wa Shule ya Msingi Nkuhungu alipoitembelea shule hiyo leo.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk Binilith Mahenge akizungumza na wanafunzi wa Shule ya Msingi Nkuhungu leo wakati wa ziara ya Waziri Jafo shuleni hapo.
Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini, Anthony Mavunde akizungumza na wanafunzi wa Shule ya Msingi Nkuhungu jijini Dodoma wakati wa ziara ya Waziri wa Tamisemi, Selemani Jafo shuleni hapo leo.
Waziri wa Tamisemi, Selemani Jafo akiwasalimi wanafunzi wa darasa la awali Shule ya Msingi Nkuhungu alipoitembelea leo. Waziri Jafo ameagiza Jiji la Dodoma kufanyia matengenezo darasa hili.
Muenekano wa barabara ya Nkuhungu Swai inayojengwa kwa kiwango cha lami ambayo umefikia asilimia 10 ya ujenzi wake, Waziri Jafo ameagiza ikamilike ndani ya muda uliopangwa.
Waziri wa Tamisemi, Selemani Jafo akikagua barabara ya Jamhuri yenye urefu wa kilomita moja ambayo imekamilika na kugharimu kiasi cha Sh Bilioni Moja.
 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...