Muhidin Amri, Tunduru

HOSPITALI ya wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma, imezindua rasmi kampeni
ya kutokomeza maambukizi ya ugonjwa wa kifua kikuu mwaka 2021 kwa
kuanza kuwatumia wanachama wa chama cha Msalaba mwekundu(Red Cross)
kama mkakati wake utakaowezesha kupunguza maambukizi na kuwaibua watu wengi wanaougua ugonjwa huo.

Wanachama hao, wataungana na wataalam wa kitengo cha kifua kikuu na
ukoma wa Hospitali ya wilaya katika kutokomeza ugonjwa huo ambapo kwa
mkoa wa Ruvuma wilaya hiyo inaongoza kwa maambukizi makubwa ya kifua
kikuu.

Mratibu wa kifua kikuu na ukoma wa wilaya ya Tunduru Dkt Mkasange
Kihongole amesema, wameamua kuwatumia na kuwashirikisha wanachama wa Chama cha Msalaba Mwekundu  kutokana na umuhimu wao katika jamii kwa kuwapa mafunzo ambayo yatawasaidia kushiriki vyema katika mapambano ya ugonjwa huo.

“Uzinduzi wa mapambano ya kifua kikuu katika wilaya yetu kwa mwaka
2021 tumeanza na wanachama wa chama cha Msalaba Mwekundu kutokana na ukaribu wao na jamii, kwa hiyo tumelazimika kuwapa elimu kwa kuamini
kuwa tutaongeza kasi ya kuwaibua wagonjwa wengi zaidi wa kifua kikuu
katika wilaya yetu kama ilivyokuwa mwaka2020.”alisema.

Alisema, uzinduzi huo utakwenda sambamba na kufanya kampeni ya
kuelimisha na kuchunguza vimelea vya ugonjwa huo katika maeneo
mbalimbali ikiwemo taasisi za serikali,shule kwa shule, nyumba kwa
nyumba na kwenye vilinge vya waganga wa Tiba asili na tiba mbadala.

Dkt Mkasange alisema, wale watakaobainika kuwa na ugonjwa huo
wataanzishiwa dawa zinazotolewa bure katika zahanati,vituo vya Afya na
Hospitali zote na kuiomba jamii kushirikiana  katika kampeni ya mwaka
huu.

Kwa mujibu wa Dkt Mkasange,  kauli mbiu ya kampeni ya kifua kikuu
mwaka 2021 ni Tb katika wilaya ya Tunduru ni ya watu wote kwa  kila
mmoja ana wajibu kutokomeza ugonjwa huo.

Akizindua kampeni hiyo mwakilishi wa Mkuu wa wilaya ya Tunduru
Agostino Maneno, amewapongeza wanachama wa chama cha Msalaba Mwekundu kwa kukubali kuwa sehemu ya timu ya kampeni ya kutokomeza ugonjwa huo na kuwataka kwenda kushiriki kikamilifu katika kuwaibua wagonjwa wengi wa kifua kikuu.

Alisema, lengo la serikali siku zote ni kuboresha afya za wananchi
wake na kuwataka watendaji wa vijiji,mitaa na kata kuwapa ushirikiano
wanachama hao  pale wanapofika katika maeneo yao kwa ajili ya
kutekeleza  kazi hiyo  kwani wanakwenda kuongeza nguvu ya kuibua watu
wengi  na kuzuia kuongezeka kwa maambukizi ya kifua kikuu.

Maneno alisema, kimsingi kampeni yay a kutokomeza kifua kikuu sio ya
mtu mmoja  au kikundi fulani cha watu, bali kila mtu anawajibu wa
kushiriki kwa kuibua,kutokomeza na kuzuia  maambukizi ya ugonjwa huo
unaotajwa kati ya magonjwa 10 Duniani yanayoongoza kuuwa watu wengi.

Kwa upande wake Mganga Mkuu wa wilaya ya Tunduru Dkt Wendy Robert
alisema,  kuna mikakati mbalimbali ya kuibua wagonjwa wengi zaidi wa
kifua kikuu na mwaka huu wameanza kutoa elimu kwa wanachama wa Red
Cross na kuendelea kuwajengea uwezo makundi mbalimbali yakiwemo
Waganga wa tiba asili,watoa huduma ngazi ya jamii.

Alisema, mwaka huu nguvu kubwa itatumika katika kuibua wagonjwa wa
kifua kikuu hasa baada ya kuona katika wilaya hiyo kuna wagonjwa wengi
wa kifua kikuu.

Dkt Wendy alisema, mwaka jana mkakati ni kuwaibua wagonjwa 647,hata
hivyo kutokana na kazi nzuri  iliyofanywa na wataalam wa kitengo cha
kifua kikuu Hospitali ya wilaya na wadau wengine  kupitia kampeni
mbalimbali walifanikiwa kuibua watu 704.

Mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo  Salome Golihama alisema, kupitia
mafunzo hayo jamii itarajie kupata elimu kuhusu ugonjwa wa kifua kikuu
na watahakikisha wanashiriki vyema katika mapambano ya kutokomeza
ugonjwa huo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...