Na Mashaka Mhando, Mkinga

WAZIRI wa Mambo ya Ndani, George Simbachawene, ameipongeza Idara ya Uhamiaji kwa kujichangisha fedha zao mifukoni na kuanzisha chuo pamoja na mafunzo ya uongozi kwa maofisa wake.

Akifungua mafunzo hayo kwa askari 287 walioanza mafunzo mwezi huu katika Chuo hicho kipya, Simbachawene alisema ameshangaa kusikia kwamba uanzishwaji wa chuo hicho umetokana na fedha zilizochangwa na idara hiyo yenyewe.

"Kinachonifurahisha na kunishangaza ni namna ya idara ya Uhamiaji, mmekuwa wazalendo kwa kuchangisha fedha zilizoanza ujenzi wa chuo hiki, nakupongeza sana Kamishina Jenerali wa Uhamiaji, umefanya kazi nzuri, " alisema Waziri huyo.

Alisema kitendo kilichofanywa na Uhamiaji ni uzalendo wa hali ya juu unaopaswa kuigwa na idara nyingine kwani unaendeleza falsafa za Rais John Magufuli ambaye ni mzalendo namba moja.

"Lazima nishabikie huu uzalendo mliouonesha, nitausemea popote pale nitakapokwenda huu ni uzalendo uliotukuka, " alisema Waziri na kuaahidi kufikisha salamu kwa Waziri Mkuu Kasim Majalia.

Akizungumzia mafunzo yaliyoanza katika chuo hicho kinachoitwa Chuo cha Uhamiaji Boma Kichaka Miba, alisema yasaidie kujenga uweledi kwa maofisa uhamiaji, katika kupambana na uhamiaji haramu katika mipaka ya nchi.

Alisema kuna wimbi la wahamiaji wanaopita katika mipaka yetu kuelekea nchini Afrika Kusini akaelezea kwamba upitaji wao katika mipaka yao lazima kuna mawakala katika maeneo hayo.

Alisema wahamiaji hawawezi kujua njia za kupita katika maeneo ya nchi bila kuwa na wenyeji ambao ni mawakala wa kusafirisha wahamiaji hao.

"Wahamiaji wakipita Horohoro kisha wakaenda kukamatwa Morogoro, nitasafisha wote polisi na uhamiaji waliokuwa zamu, kwasababu hawawezi kupita bila kuwa na wakala, " alisema.

Waziri huyo ameahidi kusaidia kutatua changamoto zilizopo katika chuo hicho hasa suala la umeme ambapo alisema serikali haiwezi kushindwa kiasi cha shilingi milioni 66 zitakazogharamia mradi wa umeme hadi katika chuo hicho.

Awali Kamishina Generali wa Uhamiaji nchini Dkt Anna Peter Makakala alisema kambi hiyo ya uhamiaji ilianza kujengwa Julai 2020 na hadi ilipofikia imetumia kiasi cha shilingi milioni 140.

Alisema kati ya fedha hizo kiasi cha shilingi millioni 81 wamechangishana wenyewe na kiasi cha shilingi milioni 59 zimetoka kwa wadau wao ikiwemo saruji, mabati na vifaa vingine vya kujengea.

Dkt Makakala alisema kambi hiyo yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 300 kwa wakati mmoja, matarajio yao ni kuwa na kambi ambayo itaweza kuchukua wanafunzi 500 hapo baadae.

"Lengo la kujenga chuo chetu wenyewe ni kukidhi mahitaji ya Idara ya kutoa mafunzo kwa wakati kwa maofisa wake yatakayokuwa na manufaa ya kuongeza uwezo na kudhibiti suala la uhamiaji, " alisema Dkt Makakala.

Aliushukuru uongozi wa mkoa wa Tanga, kwa kuwapa ushirikiano uliowezesha kupatikana kwa chuo hicho na kwamba changamoto zilizopo wanashirikiana nao kuzitatua kama vile maji na umeme.

Kwa upande wake mkuu wa mkoa wa Tanga,  Martine Shigela alisema chuo hicho kitauweka mkoa wa Tanga katika ramani lakini pia  amewataka wananchi, kutumia uwepo wa chuo hicho kujinufaisha. 

Waziri wa mambo ya ndani George Simbachawene akizungumza wakati akifungua chuo hicho
Kamishina Generali wa Uhamiaji Dkt Anna Peter Makalala akizungumzia namna walivyoanza ujenzi wa chuo hicho kwa fedha zao za mifukoni
Waziri wa mambo ya ndani ya nchi, George Simbachawene akiweka jiwe la msingi jengo litakalokuwa la Utawala wa chuo hicho




Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...