Na Mwandishi Maalum (ORCI) - Dar es Salaam

Ubalozi wa Kenya nchini umeweka wazi nia yake ya kuongeza ushirikiano na Tanzania katika matibabu ya saratani kwa kuhakikisha diplomasia ya utamaduni na afya baina ya hizi nchi mbili unaimarishwa ikiwemo wananchi wa Kenya, kufika katika Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI).

Masuala hayo yamebainishwa na Balozi wa Kenya nchini Tanzania, Mhe. Balozi Dan Kazungu, alipofanya ziara katika Taasisi ya Saratani Ocean Road akiwa ameambatana na Afisa wa Ubalozi huo, Dr. Rosylne Angola.

Katika ziara hiyo, Balozi Kazungu amefanya kikao kifupi cha majadiliano ya kuimarisha ushirikiano na uongozi wa Taasisi ya Saratani Ocean Road akiwamo Mkurugenzi Mtendaji, Dkt. Julius Mwaiselage, Mkurugenzi wa Huduma za Kinga za Saratani, Dkt. Crispin Kahesa, na Mkurugenzi wa Mipango, Daudi Maneno.

"Ziara ililenga kubadilishana mawazo ya jinsi ya kuzidi kuboresha ushirikiano mzuri unaofanywa baina ya Serikali ya Kenya na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika maeneo mengi ikiwamo Sekta ya Afya," amesema Dk. Mwaiselage alipozungumza na waandishi wa Habari.

Ameongeza "Kama mnavyofahamu Serikali kupitia Taasisi ya Saratani Ocean Road imeboresha huduma zake mbali mbali ikiwemo za kuzuia saratani kwa kufanya chanjo za HPV na HBV pamoja na ugunduzi wa dalili za awali.

"Huduma za uchunguzi na matibabu ya saratani kwa kutumia mashine zenye teknolojia ya kisasa ambazo ni sawa na zile zinazopatikana nchi za Ulaya".

"Hii imeongeza idadi ya wagonjwa wanaotoka nchi za jirani ikiwemo Kenya kuja kupata huduma katika taasisi kutoka wagonjwa 24 mwaka 2017 hadi wagonjwa 128 mwaka 2020. Aidha, imesaidia kupunguza rufaa za wagonjwa kwenda nje ya nchi kutoka 164 mwaka 2014 hadi wagojwa watatu mwaka 2020," amebainisha.

Amesema katika kikao hicho walijadiliana jinsi ya kushirikiana katika shughuli za kijamii katika Taasisi na miongoni mwa shughuli waliyoridhia ni kuboresha mazingira kwa kupanda miti ikiwa ni sehemu ya kumuenzi Hayati Prof. Wangari Maathai aliyefariki Septemba 25, 2011 kwa saratani ya mlango wa kizazi.

"Prof. Wangari alitunikiwa nishani ya Nobel kwa jitihada za kutunza mazingira nchini Kenya na Afrika kwa ujumla. Prof Wangari alikuwa ni  mwanamke wa kwanza nchini Kenya kupata Shahada ya uzamivu (PhD) na alijikita sana katika kuhamasisha upandaji miti na utunzaji wa mazingira kupitia mpango wake wa Greenbelt movement," amebainisha.

Amesema shughuli hiyo ya upandaji wa miti imepangwa kufanyika April Mosi, mwaka huu katika viunga vya Taasisi ya Saratani Ocean Road ili pia kuadhimisha siku hiyo ambayo ni siku ya kuzaliwa hayati Prof Wangari Maathai".

Pichani kutokea  upande wa kushoto ni Mr.Daudi Maneno(Mkurugenzi wa Mipango), Anayefuata ni Dk. Julius Mwaiselage (Mkurugenzi Mtendaji ) , akifuatiwa na Mh.Dan Kazungu ( Balonzi wa Kenya nchini Tanzania), Mkurugenzi wa Huduma za Kinga za Saratani Ocean Road, Dk. Crispin Kahesa, anayefuata ni Dk.Rosylne Angola Afisa wa Ubalozi wa Kenya.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...