Mkutano wa 21 wa Wakuu wa Nchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki umepangwa kufanyika Jumamosi, 27 Februari, 2021 kwa njia ya mtandao (video conference).

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) amewaeleza waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuwa mkutano huo ni muhimu kwa sababu ya maamuzi ya msingi ya kuiwezesha jumuiya hiyo iweze kuendelea kufanya kazi zake.

“Jambo la kwanza ni uteuzi wa Katibu Mkuu mpya wa Jumuiya ya Afrika mashariki, kwa hiyo Wakuu wa nchi watamchagua Katibu Mkuu mpya siku hiyo,” Amesema Prof. Kabudi na kuongeza kuwa mkutano huo pia utafanya uteuzi wa Majaji wa Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki (The East African Court of Justice) kutokana na baadhi ya majaji kufikia umri wa kustaafu wa miaka 70, ambapo Tanzania imempendekeza jaji Yohane Masara kuwa jaji wa jopo la kwanza la mahakama ya Afrika Mashariki.

“Pamoja na kuteuliwa kwa majaji hao, pia Wakuu wa nchi watamteua Rais wa Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki (Judge President) pamoja na kumchagua Makamu wa Rais (Vice President) kwa ngazi ya Rufaa ya Mahakama hiyo, lakini katika ngazi ya awali Mkutano huo utamchagua Principla Judge wa Mahakama hiyo, kwa hiyo mtaona hizo ni baadhi ya shughuli zilizopelekea Wakuu wa nchi wakutane ili kuweza kufanya teuzi hizo muhimu ili shughuli za Jumuiya ya Afrika Mashariki ziweze kuendelea” Ameongeza Prof. Kabudi

Prof. Kabudi ameongeza kuwa Mkutano wa Wakuu wa Nchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki pia utajadili Muswaada ulipitishwa na Bunge la Afrika Mashariki kwa ajili ya kupata bajeti.

Mkutano huo utatanguliwa na mkutano wa 40 wa Kawaida wa Baraza la Mawaziri wa Afrika Mashariki utakaofanyika Alhamisi tarehe 25 Februari 2021 kwa ajili ya kuandaa mkutano wa wakuu wa nchi. Aidha, mkutano wa Baraza la Mawaziri umetanguliwa na mkutano Wataalam ulifanyika tarehe 22-23 Februari na mkutano wa Makatibu Wakuu ulifanyika tarehe 24 Februari.

Tarehe 1 Januari 2019, Rais wa Rwanda Mhe. Paul Kagame alikabidhiwa Uenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki katika Mkutano wa wakuu wa jumuiya hiyo jijini Arusha Tanzania.

Katika hatua nyingine, Prof. Kabudi ameelezea kuhusu ziara ya kikazi aliyoifanya nchini Ufaransa kuanzia tarehe 16 mpaka 21 Februari 2021, kufuatia mwaliko wa Mhe. Jean-Yves Le Drian, Waziri anayeshughulikia Masuala ya Ulaya na Mambo ya Nje wa Ufaransa na kuelezea mafanikio makubwa ya ziara hiyo.

“Pamoja na mambo mengine niliweza kukutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa Serikali ya Ufaransa, Umoja wa Wafanyabiashara wa Ufaransa (MEDEF), Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO), Uongozi wa Kampuni ya Total, Kundi la Maseneta wa Bunge la Ufaransa ambao ni Marafiki wa Tanzania, Uongozi wa Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD), Wadau wa Utalii pamoja na kuzungumza na Watanzania wanaoishi nchini Ufaransa,” Amesema Prof. Kabudi.

Aidha, kupitia ziara hiyo, Ufaransa imeeleza kuwa itaendelea kuhamasisha Makampuni yake kuja kuwekeza Tanzania pamoja na kuhamasisha watalii kuja kuwekeza Tanzania, kuiunga mkono Tanzania katika masuala mbalimbali kwenye ngazi ya Umoja wa Mataifa.

Mengine ni kuwa Ufaransa kupitia Shirika lake la Maendeleo la AFD itaendelea kufadhili miradi mbalimbali ya maendeleao hapa nchini hususan kwenye sekta ya maji, elimu, nishati, miundombinu, utalii, ulinzi na usalama;na Ufaransa kuwa tayari kushirikiana na Tanzania kwenye masuala mbalimbali yanayohusu ulinzi na Usalama.

Mafanikio mengine ni pamoja na kukubaliana kuanza mara moja mchakato wa kuifanya lugha ya Kiswahili kuwa miongoni mwa lugha rasmi zinazotumika kwenye Umoja wa Mataifa. Nilimweleza mafanikio yaliyopatikana kwenye lugha ya Kiswahili ikiwa ni pamoja na kuwa miongoni mwa lugha 10 zinazozungumzwa zaidi barani Afrika pamoja na kutumika kama lugha rasmi kwenye Umoja wa Afrika (AU) na SADC;

“Tulikubaliana kuanza mchakato ili kuwa na siku rasmi ya kuadhimisha lugha ya Kiswahili duniani kila mwaka. Nilipendekeza tarehe 7 Julai kila mwaka kwa kuzingatia kuwa tarehe hiyo ndio kilizaliwa Chama cha TANU. TANU ilikifanya Kiswahili kuwa lugha rasmi ya kupigania uhuru wa Tanganyika wakati huo. Tumeona ni jambo jema kuienzi tarehe hiyo muhimu kwenye historia ya nchi yetu,” Amesema Prof. Kabudi

Kupitia ziara hiyo, Prof. Kabudi aliweza kuyakaribisha Makampuni ya Ufaransa kuja kuwekeza nchini hususan kwenye sekta ya viwanda, kilimo, nishati, maji, elimu, miundombinu, uvuvi na utalii. Makampuni hayo yalionesha kuridhika na hatua mbalimbali zilizochukuliwa na Serikali katika kuboresha mazingira ya uwekezaji na ushiriki wa sekta binafsi katika uchumi wa Tanzania.

“Baadhi ya Makampuni makubwa yaliyoshiriki majadiliano hayo ni pamoja na Bureau Veritas; Mitsubishi II; Biolore Transport and Logistics; Eutelsat Company; Artelia Company; Catering International Services-CIS; Systra Company; Transder Group; Credit Agricole Corporate and Investment Bank; Air Bus; na Bouyegues Construction. Mengi ya makampuni haya tayari yamefanya uwekezaji mkubwa nchini katika maeneo mbalimbali,” Amesema Prof. Kabudi.

Aidha, makampuni hayo yameonesha utayari wa kutekeleza miradi hapa nchini kwa kutumia fedha kutoka Serikali ya Ufaransa zitakazotolewa kama mkopo wenye masharti nafuu. Tumeyakaribisha Makampuni hayo kuja nchini ili kukutana na wataalam wetu kwa ajili ya majadiliano.

Prof. Kabudi ameelea kuwa Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD) kwa kushirikiana na Serikali ya Tanzania ipo katika hatua za mwisho za kukamilisha majadiliano ya miradi ya kimkakati kwa Tanzania katika sekta ya maji safi na usafi wa mazingira, nishati na miundombinu ambapo tayari jumla ya fedha Euro milioni 791.70 tayari zimeshatengwa kwa ajili ya miradi hiyo.

Fedha hizo zitaelekezwa katika baadhi ya miradi ambayo ni mradi wa ujenzi wa awamu ya tano ya mwendokasi BRT Phase 5 (Euro milioni 150), mradi wa Maji safi na Usafi wa Mazingira mkoani Shinyanga (Euro milioni 70), ujenzi wa bwawa la kuzalisha umeme la Kakono (Euro milioni 100), mradi wa kuzalisha umeme kwa kutumia jua chini ya TANESCO (Euro milioni 130) na mradi wa kuunganisha umeme Tanzania na Uganda (Euro milioni 100).

Katika hatua nyingine, Prof. Kabudi amewasihi watanzania kuheshimu katiba na kuacha mara moja tabia ya kusambaza taarifa za uongo.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) akiwaonesha waandishi wa habari (hawapo pichani) aina za cocoa zinazozalishwa Tanzania na kuuzwa nchini Ufaransa jijini Dar es Salaam.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) akiongea na waandishi wa habari (hawapo pichani) jijini Dar es Salaam.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) akiwasomea waandishi wa habari (hawapo pichani) moja ya kifungu cha katiba kuhusu mipaka ya haki na Uhuru na hifadhi kwa haki na wajibu jijini Dar es Salaam

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...