Waziri, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Ummy Mwalimu akimueleza jambo Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Pauline Gekul (wapili kulia) walipokutana katika kikao cha Wavuvi na Naibu Waziri huyo kilichofanyika Mkoani Tanga mapema leo Februari 27, 2021. Lengo la kikao hicho ni kusikiliza kero za Wavuvi wa Mkoani Tanga.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Pauline Gekul (katikati) akiangalia Ng’ombe waliopelekwa katika Mnada wa Nderema kwa ajili ya kuuzwa. Naibu Waziri alitembelea mnada huo uliopo Katika Halmashauri ya Mji, Handeni, Mkoani Tanga leo Februari 27, 2021 kwa lengo la kukagua shughuli zinazofanyika Mnadani hapo.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Pauline Gekul akikagua risiti aliyopewa mfanyabiashara aliyenunua Ng’ombe katika Mnada wa Nderema uliopo katika Halmashauri ya Mji, Handeni, Mkoani Tanga leo Februari 21, 2021. Naibu Waziri alitembelea mnada huo kukagua shughuli zinazoendelea katika mnada huo.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Pauline Gekul ( wanne kutoka kulia) akiangalia bidhaa mbalimbali za maziwa zinazozalishwa na  Kampuni ya Tanga Fresh alipotembelea kukagua shughuli za Kiwanda hicho kilichopo Mkoani Tanga mapema leo Februari 27, 2021.

****************************************

Na Mbaraka Kambona, Handeni

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Pauline Gekul ameipa  Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) wiki moja kueleza namna walivyotekeleza maagizo aliyoyatoa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki ya kuwachukulia hatua wale wote waliokiuka mkataba wa umiliki wa vitalu katika ranchi hizo.

Gekul alitoa agizo hilo alipotembelea kukagua shughuli za Ranchi ya Mzeri iliyopo katika Halmashauri ya Mji, Handeni Februari 27, 2021.

Alisema kuwa Waziri Ndaki alishatoa maelekezo kwa Kampuni hiyo kuwa mpaka itakapofika Februari 15 wawe wameshachukua hatua kwa walioshindwa kuendeleza vitalu walivyopangishwa ikiwemo kuwanyang’anya vitalu hivyo.

“Ndugu zangu Mheshimiwa Waziri alishatoa maelekezo kuhusu waliokiuka mkataba, leo ni Februari 27 hatujapata taarifa yoyote, natoa wiki moja tupate taarifa ya utekelezaji, kauli ilishatolewa tunataka utekelezaji, vinginevyo tutaona NARCO hamtoshi,” alisema Gekul

Aliongeza kwa kusema kuwa kwa muda mrefu kumekuwa hakuna ufuatiliaji wa kina kuhusu ranchi hizo na watu kugeuza kichaka na Serikali imeendelea kupoteza mapato yake jambo ambalo hawataruhusu liendelee kutokea.

Gekul alisema wale ambao wameshaonesha nia ya kuanza kulipa wanaweza kuvumiliwa lakini waeleze wanampango gani na deni watamaliza lini, lakini ambao mpaka sasa hawajafanya lolote watafutwe na wachukuliwe hatua.

Aidha, Gekul aliwata NARCO kuhakikisha wanaongeza uzalishaji wa Ng’ombe wa Nyama na Maziwa ili kukidhi mahitaji ya Viwanda na kuuza nje ya nchi.

“Tunataka wawekezaji watakaofuga kibiashara katika ranchi zetu, huku hatutaki kufuga kama maonesho, tunataka ufugaji kwenye hizi ranchi uwe wa tija ili mazao yaende yakachakatwe kwa wingi katika viwanda vyetu,” alifafanua Gekul

Alisema kuwa serikali imepunguza gharama za ukodishaji wa vitalu na sasa ni shilingi 3500 kwa heka moja, hivyo aliwahamasisha wawekezaji ambao wanania ya kufuga kisasa kutumia fursa hiyo kuendesha ufugaji wa kisasa katika ranchi hizo ili kuongeza tija katika uzalishaji na kuongeza pato la taifa.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...