Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania(TANESCO) Dk.Tito Mwinuka akizungumza mbele ya waandishi wa habari leo Februari 26,2021 Mjini Morogoro wakati akifungua semina iliyoandaliwa na Shirika hilo kwa wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari.

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano TANESCO Johari Kachwamba akitoa maelezo kwa wahariri.

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania(TANESCO) Dk.Tito Mwinuka akifafanua jambo kwa wahariri kutoka vyombo mbalimbali vya habari nchini.

Baadhi ya wahariri wakiwa makini kufuatilia majadiliano yaliyokuwa yakiendelea wakati wa semina hiyo inayoendelea Mjini Morogoro
Mhariri wa TBC  Eshe Muhidini akiwa makini kufuatilia majadiliano yaliyokuwa yakiendelea kwenye semina hiyo.


Mmoja ya wahariri kutoka gazeti la Mwananchi Lilian Timbuka akiuliza swali wakati wa semina hiyo.


matukio mbalimbali katika picha wakati wa semina hiyo ambayo imeandaliwa na TANESCO kwa wahariri wa vyombo vya habari nchini.

Na Said Mwishehe, Michuzi TV

SHIRIKA la Umeme Tanzania(TANESCO) limefafanua hatua kwa hatua kuhusu hali ya umeme nchini huku ikielezea sababu ambazo zimekuwa zikisababisha kufungulia maji kwenye mabwawa ya kuzalisha umeme nchini.

Pia imetaja vyanzo vyake vinne vya kuzalisha umeme ambavyo ndivyo kwa sasa vinategemewa na Shirika hilo huku likitumia nafasi hiyo kuelezea mikakati yake ikiwemo ya kuzima mitambo ya kuzalisha umeme inayotumia mafuta.

Akizungumza leo Februari 26,2021, mbele ya wahariri wa vyombo vya habari nchini, Meneja Mwandamizi wa Uzalishaji Umeme kutoka Shirika la Umeme Tanzania(TANESCO)Mhandisi Stephen Manda ameeleza kwa kina kuhusu hali ya umeme nchini na kwamba kuna ziada ya umeme megawati 400.

"Niseme kwamba hali ya mabwawa yetu ni nzuri na hali ya ufuaji umeme ni nzuri.Kwa ujumla mabwawa yetu yana maji ya kutosha,"amesema Mhandisi Manda wakati anatoa ufafanuzi kwa wahariri hao walioko kwenye semina iliyoandaliwa na TANESCO ili kuelezea mipango, mikakati pamoja na miradi inayoendelea kutekelezwa kwa sasa.

Vipi kuhusu kufungulia maji kwenye mabwawa?

Mhandisi Manda amesema kuhusu kufungulia maji kimsingi sio tu suala la TANESCO kuamua bali linaamriwa na hali halisi ya hewa hasa kwa kuzingatia mabadiliko ya hali ya hewa kwa mfano kukiwa na mvua nyingi mabwawa yatajaa maji kuliko inavyotakiwa, hivyo lazima watayafungulia.

Aidha amesema miundombinu yao imesanifiwa kwamba maji yanakiwango cha juu kabisa ambacho kinatakiwa kuhifadhiwa lakini yanapozidi wayanafungulia kwa kuyaruhusu yapite."Kwa waliofika Bwawa la Julius Nyerere kuna maeneo saba ya kuhurusu maji kupita, kwa hiyo tunafungua tu pale maji yanapozidi.

"Pia tunafungulia maji ili kulinda miundombinu na wakati tunayafungua tunayafungulia kwa udhibiti ili yasilete madhara.Na suala hili la kuyafungulia maji katika mabwawa yetu hutokea mara chache sana huenda ikatokea ndani ya kipindi cha miaka mitano au miaka 10 kulingana na hali ya mvua kwa wakati husika.

Amesisitiza kwa hiyo hali ya umeme nchini ni nzuri na maji yanaingia vizuri na kwamba  kwa sasa hawajaanza kufungulia maji lakini kama yataongezeka basi watafungulia."Kwa bwawa la Mtera tumebakiza sentimeta nne tu maji yatazidi, hivyo tutaangalia namna ya kuyadhibiti kama yataongezeka."

VIPI KUHUSU HALI HALISI YA UMEME?

Mhandisi Manda amesema umeme uliopo ni wa kutosha na kwamba gridi yao uwezo wake ni kuzalisha megawati 1,604.81 kwa siku wakati mahitaji ya juu kabisa ni megawati 1,180.53, hivyo kuna ziada ya umeme wa megawati 424.28.

"Pamoja na ziada hiyo ambayo tunayo bado tunaona haitoshi na ndio maana Serikali inaendelea na kutekeleza mradi mkubwa wa umeme kwenye bwawa la Mwalimu Nyerere ili kuwa na umeme wa kutosha kabisa nchini.

"Malengo yetu mpaka mwaka 2025 tuwe na kiwango cha chini cha megawati 5000 ili kitakapopanda na kuwa na matumizi ya megawati 1,800 kama matumizi yatakuwepo basi tuwe na ziada ya umeme wa kutosha na ikiwezekana tuuze katika nchi nyingine.

HIVI NDIVYO VYANZO VYA UMEME TANESCO

Mhandisi Manda amesema vyanzo ambavyo vinategemewa katika uzalishaji umeme ni chanzo cha maji ambacho uzalishaji wake ni asilimia 36, gesi asilia  asilimia 56,mafuta asilimia 7 pamoja na chanzo cha Tungamotaka(Biomass) kwa asilimia 1.

JE KUNA MKAKATI WA KUZIMA MITAMBO YA MAFUTA?

Amesema TANESCO ina mikakati ambapo ametoa mfano kuna mikoa mitatu ya Kigoma, Katavi na Rukwa ambayo bado haijaunganishwa na gridi ya taifa, hivyo inatumia umeme unatokana na mafuta.

"Na mategemeo yetu kutokana na mpango kazi ifikapo Aprili 2022,mikoa hiyo iwe imeunganishwa kwenye gridi ya Taifa na kwa sasa tunaendelea kujenga na ujenzi wa miundombinu ya usafirishaji umeme kutoka Tabora kwenda Kigoma kupitia Mrambo, Kauliua, Nguruka na Kidawe na vile vile tunatoa umeme kutoka Tabora kwenda Mpanda."

Mhandisi Manda amesema lengo kubwa ni kuhakikisha hii mitambo inayotumia mafuta inazimwa na kuokoa fedha nyingi za shirika.

JE BADO WATEJA WANALALAMIKA VITU VYAO KUUNGUA?

Akizungumzia hilo amesema kimsingi TANESCO imeboresha huduma zake katika maeneo yote nchini na hasa miundombinu ya usambazaji umeme ambao umefanyika kwa kiwango kikubwa,hivyo malalamiko yamepungua kwa kiwango kikubwa.

"Lengo la TANESCO tunataka mteja asikose umeme hata kwa sekunde na tunafahamu tuko kila mahali, lakini umeme unaweza kukatika kutokana sababu ya miundombinu, kuna maeneo watu wanachoma moto na kusababisha nguzo kuanguka na kusababisha umeme kukatika hivyo tunaomba ushirikiano wa wananchi.

"Pale unapoona kuna nguzo imeanguka au mti umelalia nguzo basi tupewe taarifa ili tuweze kushughulikia. 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...