WANANCHI Wilayani Lushoto wameishukuru Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dk John Magufuli kwa kuwarejeshea shughuli za uzalishaji katika kiwanda cha Mponde Tea Estate kilichopo kata ya Mponde, Wilayani Lushoto.

Shukrani hizo wamezitoa wakati wa ziara ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama alipofanya ziara kiwanda hapo ikiwa ni maagizo yaliyotolewa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa kuwa kiwanda hicho kianze kazi.

Waziri Mhagama amesema habari hizo njema za Serikali kwa wananchi hao kuwa hivi sasa ni kuwa Serikali yao imeamua kufufua kiwanda hicho ili wakulima wa chai waendelee kulima zao hilo la chai litakaloleta manufaa kwa wakazi wa Bumbuli na Wilaya ya Lushoto kwa Ujumla.

“Serikali imeamua kurejesha matumaini kwa wakazi wa Bumbuli na Wilaya ya Lushoto kwa kuanzisha shughuli za uzalishaji katika kiwanda cha Mponde Tea Estate ili kuhakikisha kilimo cha zao la chai kinaleta tija na kusaidia wakulima wa zao waliopo katika maeneo haya wananufaika zaidi,” alisema Mhagama

Alieleza kuwa, Serikali inatambua changamoto zilizokuwa zikiwakabili wakazi wa eneo hilo waliokuwa wakijihusisha na kilimo cha Chai, hivyo Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli imedhamiria kuanzisha shughuli za uzalishaji katika kiwanda hicho ili kuwezesha wanabumbuli na Lusho kwa ujumla kuongeza uzalishaji wa zao hilo kwa kuwa wanasoko la hukakika katika kiwanda hicho.

Aliongeza kuwa, Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya Mwaka 2020 – 2025 imeweka zao la Chai kuwa moja wapo ya zao la kimkakati na hivyo uzalishaji wa zao hilo kwa sasa hapa nchini ni zaidi ya tani 37,000 lakini Serikali imejipanga kuongeza zaidi uzalishaji wa zao hilo ifikapo 2025 uzalishaji kufikia tani zaidi ya 60,000.

Sambamba na hayo Waziri Mhagama alieleza kuwa Kikosi kazi kipo tayari kwa ajili ya kuhakikisha kiwanda kinaanza shughuli za uzalishaji ambapo timu ya kwanza itahusisha mafundi wabobezi ambao watahusika na kuboresha mitambo ya kiwanda hicho ili kianze uzalishaji haraka huku wakiwa na mkakati wa kujenga kiwanda kipya katika eneo hilo, timu ya pili itakuwa ikiangalia masuala ya utawala ambayo itakuwa na jukumu la kusimamia shughuli za kiwanda hicho, huku timu ya mwisho ikiwa na jukumu la kuwawezesha wakulima kuongeza tija ya uzalishaji wa zao hilo la chai.

“Katika ziara hii nimeambatana na wataalam kutoka maeneo mbalimbali ikiwemo TIRDO, Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) na Benki ya Kilimo kwa lengo la kuhakikisha kiwanda hiki kinaanza kuzalisha na kuwanufaisha wakulima wa chai katika wilaya ya Lushoto na wakazi wa mponde,” alisema Mhagama

Aidha, Waziri Mhagama amewasisitiza wakulima wa zao hilo la chai katika Halmashauri ya Bumbuli na Wilaya ya Lushoto kwa ujumla kutatua migogoro iliyopo ndani ya AMCOS zao ili wafufue mashamba yao kwa kuwa hivi sasa wamepata sehemu ya uhakikaka ya kupeleka zao la chai ambalo litachakatwa.

Kwa Upande Wake, Mkuu wa Wilaya ya Lushoto, January Lugangika alieleza kuwa Kata 18 zilizopo katika wilaya hiyo zinalima zao la chai na asilimia kubwa ya wakulima wa zao hilo wanamatumaini makubwa na kiwanda hicho katika kuwainua kiuchumi kutokana na ajira watakazo zipata kiwandani hapo pamoja na kuuza malighafi hiyo ya zao la chai.

Naye, Mbunge wa Bumbuli, January Makamba amewataka wananchi hao kuchangamkia fursa ya kuzalisha zao la chai kwa wingi kwa kuwa Serikali yao imeamua kuanzisha uzalishaji katika kiwanda cha Mponde Tea Estate.

“Migogoro iliyojitokeza katika kiwanda hiki hapo awali ilichangia kudhorotesha uchumi wa wakazi wa maeneo haya kwasababu wananchi wengi waliacha kulima zao la chai baada ya kiwanda hicho kufungwa ila kuanzishwa shughuli za uzalishaji katika kiwanda hicho itahamasisha wakulima wengi kulima zao la chai na kunufaika kiuchumi,” Amesema Makamba

Mmoja wa wakazi wa eneo hilo Bw. Juma Msilimu amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kwa kurejesha matumaini kwa wananchi hususan wakulima wanaojishughulisha na kilimo cha zao la chai wa halmashauri ya Bumbuli na Wilaya ya Lushoto kwa ujumla kutokana na uwepo wa kiwanda hicho cha Mponde Tea Estate 

 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...