Kiongozi wa Wakulima Kijiji cha Kijungu, Machita Mgurangu akilazimishwa na Askari Polisi kuingia ndani ya gari la polisi baada ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene, kuagiza viongozi wa Kitongoji na Kijiji cha Kijungu, Wilaya ya Kiteto, Mkoani Manyara, wakamatwe kwa kushawishi wananchi kufanya vurugu na kuvamia maeneo ambayo yametengwa kwa shughuli za mifugo. Picha Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene (kushoto), akizungumza na Wananchi wa Kitongoji cha Miriongima, Kijiji cha Kijungu, Wilaya ya Kiteto, Mkoani Manyara, leo, wakati alipofika kijijini hapo kufuatilia masuala ya usalama kuhusiana na mgogoro wa wakulima na wafugaji unaoendelea, ambapo ameagiza viongozi wa vijiji wakamatwe kwa kuwashawishi wananchi kufanya vurugu na kuvamia maeneo ambayo yametengwa kwa shughuli za mifugo. Picha Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.

Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Joseph Mkirikiti akimuonyesha Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene (kushoto), mashamba yaliyolimwa na wakulima katika eneo la Amei ambalo limetengwa kwa shughuli za mifugo. Picha Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene (kushoto), akisalimiana na Askari na Maafisa wa Polisi wa Kituo cha Polisi cha Wilaya ya Kiteto, Mkoani Manyara, leo, wakati alipofika katika kituo hicho kuangalia utendaji kazi na pia kufuatilia masuala ya usalama kuhusiana na mgogoro wa wakulima na wafugaji unaoendelea Wilayani humo. Picha Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene (kulia), akimsikiliza Mwenyekiti wa Kijiji cha Amei, Ngoida Senkwa, wakati alipokuwa anazungumza masuala ya Wafugaji katika Mkutano uliofanyika katika Kijiji cha Kijungu, Wilayani Kiteto, leo, hata hivyo, Waziri huyo aliagiza viongozi wa Kijiji cha Kijungu wakamatwe kwa kuwashawishi wananchi kufanya vurugu na kuvamia maeneo ambayo yametengwa kwa shughuli za mifugo. Picha Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene (kushoto), akisalimiana na Mbunge wa Kiteto, Ole Lataika pamoja na viongozi mbalimbali wa Wialaya ya Kiteto wakati alipokuwa anawasili Wilayani humo kufuatilia masuala ya usalama kuhusiana na mgogoro wa wakulima na wafugaji unaoendelea. Picha Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.

*******************************************

Na Mwandishi Wetu, MOHA, Kiteto

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene ameamuru kukamatwa na kuwekwa mahabusu viongozi wa vijiji vya Miriongima na Kijungu Wilayani Kiteto kwa kosa la kushawishi wananchi kufanya vurugu na kuvamia eneo lililotengwa na Serikali kwa shughuli za mifugo.

Viongozi hao ambao pia wapo upande wa wakulima, wanadaiwa kuchukua rushwa kwa kuuza mashamba ambayo yapo maeneo ya wafugaji na kusababisha kuibuka kwa migogoro kati ya wakulima na wafugaji katika vijiji vya Kijungu na Amei.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara na Wananchi wa Kitongoji cha Miriongima, Kijiji cha Kijungu, Wilaya ya Kiteto, Mkoani Manyara, leo, Waziri Simbachawene alisema viongozi hao wa vijiji ndio wanaochochea migogoro ambayo inaendelea kwasababu wanawadanganya wananchi na kupelekea kuvamia maeneo ambayo yametengwa kwa shughuli za mifugo kwa kufanya kilimo.

 “Nimekuja kwasababu ya uvunjifu wa amani, nimekutana na viongozi wenu wa Wilaya na Mkoa, pia nimetembelea Kijiji cha Amei, na nyie hapa nimewasikiliza, kwa wale ambao mlienda kulima kule ardhi ya kijiji cha Amei, mkiamini kwamba viongozi hawa wa kijiji cha Kijungu ni wakweli, sasa muelewe kuanzia leo kwamba wamewadanganya ile ardhi sio yao kwasababu shamba hilo la Jumuiya lilishakufa siku nyingi na vijiji vilishaanzishwa, Mwenyekiti wa Kitongoji hiki, na Mwenyekiti wa Kijiji hiki wanatakiwa kuchukuliwa hatua,” alisema Simbachawene.

Aliongeza kuwa; “….kwasababu kama viongozi hawa wangekuwa na madai ya msingi, Mkuu wa Wilaya ungeyajua, Mkuu wa Mkoa ungeyajua, Mkurugenzi angeyajua, Mwenyekiti wa Halmashauri angeyajua, lakini dai la mkologanyo la mpaka haliwezi likaja leo wakati kumetokea hilo, niwaambieni wale ambao mlidanganywa, mkaawaamini hawa, na mkaenda kufanya kule kilimo, mlifanya kwa hiari yenu, na hasara nmi yenu, poleni, kwenye ukweli lazima tuseme ukweli.”

Waziri huyo alisisitiza kuwa, haiwezekani Mwenyekiti wa Kijiji cha Kijungu kutokujua kuwa kuna Kijiji cha Amei, na kijiji hicho kilianzishwa tangu mwaka 1993, viongozi hao ni wachonganishi, na pia wameshindwa hata kukaa na Mwenyekiti wa Amei kuzungumza suala hilo ambalo lipo kisheria.

Waziri Simbachawene aliambatana na viongozi wa mbalimbali wa Wilaya na Mkoa, ambao ni Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa Wilaya pamoja na Kamati yake ya Usalama ya Wilaya, Mbunge wa Jimbo la Kiteto, pamoja na viongozi wa halmshauri ya Wilaya hiyo.

Aidha, Waziri Simbachawene kwa niaba ya Serikali aliagiza uongozi wa Wilaya na Mkoa, kuhakikisha viongozi wa vijiji wanaosababisha migogoro wanakamatwa na kuchukluliwa maelezo kwa kuwa imebainika migogoro mingi ndani ya Wiklaya ya Kiteto, ya kuuza maeneo ambayo tayari yana mipango bora ya matumizi ya ardhi katika Wilaya hiyo, yanasababishwa na viongozi wa Vijiji na Kata.   

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa, Joseph Mkirikiti, alisema katika kijiji cha Amei, kuna wakulima wakubwa ambao wamewaweka wafanyakazi katika mashamba hayo, na endapo Mkuu wa Mkoa pamoja na viongozi wa Wilaya wakienda katika mashamba hayo, wakulima hao wakubwa hawaonekani zaidi ya wanaofanyia kazi.

“Mheshimiwa Waziri kuna watu wakubwa, hawapo zaidi ya watano, mmoja anahekari mia tano, mwingine hekari 2000, mwingine hekari 3000, hawa watu wamelima kule, ukienda kule mashambani hukutani nao, unakutana na watendaji kazi na kuwakamata huwezi, utawaonea, na hatuwezi tatua tatizo, bado tukasisitiza hawa watu waje ofisini ili tuzungumze lakini hawataki kuja,” alisema Mkirikiti.

 Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Kiteto, Ole Lataika, alisema njia pekee ya kuluhisha tatizo hili kati ya Wakulima na Wafugaji ni kusimamia sheria, na ndio njia pekee ya kumaliza suala kwasababu mkulima ni muhimu na mfugaji ni muhimu katika maendeleo.

“Sheria peke yake ndio itatunusuru tukisimamia bila kumuonea mtu yeyote, mkulima ni muhimu na mfugaji ni muhimu, na matumizi bora ya ardhi ndio njia pekee ambayo tumejiwekea, kwamba mkulima atalima hapa na mfugaji atafuga hapa na wale walio na mamlaka wasimamie bila kupindisha hata hatua moja, tukifanya hivyo mambo yote yatakuwa shwari, na mambo yanayoendelea kule yanakuzwa tu, kwa kata mbili, tatu ndio iwe Kiteto nzima sio salama, kuna maeneo mengine wapo wakulima na wagugaji usikii haya mambo hata kidogo,” alisema Lataika.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...