Na Amiri Kilagalila, Njombe
WAKULIMA wa zao la mahindi jimbo la Ludewa mkoani Njombe wameiomba serikali kushughulikia bei ya zao la mahindi kwa kuwa wamekuwa wakipata shida kutafuta soko la zao hilo huku wakiuza kwa bei ya kutupwa kwa shilingi 4000 mpaka 5000 kwa debe moja hatua inayosababisha mahindi kuozea majumbani kwa kukosa soko.

Wamewasilisha ombi hilo katika vikao tofauti vilivyofanyika baina ya makundi mbali mbali na mbunge wa Jimbo hilo Joseph Kamonga wakati akikusanya maoni ya wananchi wake kabla ya kuelekea katika vikao vya bunge vinavyotarajia kuanza karibuni.

Shegh Haruna Rahim ni imamu wa msikiti wa wilaya ya Ludewa na mkulima wilayani humo pamoja na Tafuteni Mwasonya ni mchungaji wa kanisa la KKKT jimbo la Ludewa ambao pia wanajishughulisha na kilimo,wamesema ni miaka kadhaa sasa wamekosa zao la mahindi hivyo wanatoa rai kwa serikali kufungua soko ili kuwasaidia wakulima.

“Tunalima mahindi lakini tunakosa soko lakini pia ule utaratibu wa serikali kununua mahindi tulikuwa tunatembea sana na wakulima walikuwa wanalima kweli kweli lakini kwa sasa tunalima lakini hatuna kwa kuuzia”alisema Tafuteni Mwasonya

“Nakushukuru hata wewe mbunge umeliona hilo pia tunaomba uendelee kulifanyia kazi maana mwisho wa siku mtu akiona kilimo hakina tija hatoweza kulima tena kwasababu tunatumia ghalama kubwa sana lakini soko limekuwa ni gumu sana”alisema Haruna Rahim

Bonifasi Faru ni mkulima na mfanyabiashara mkazi wa kilima hewa wilayani Ludewa,amesema wamekuwa wakitoka na mahindi mashambani lakini wamekuwa wakiuzia mahindi majumbani hivyo amemuomba mbunge wa Ludewa kushughulikia tatizo hilo ikiwa ni pamoja na kusogeza benki ya wakulima katika maeneo yao.

Kwa upande wake mbunge wa jimbo la Ludewa wakili Joseph Kamonga amesema serikali itaendelea kushughulikia tatizo hilo huku akiona namna ya kutafuta wawekezaji kwa ajili ya viwanda vya kusindika unga katika jimbo lake.

Vile vile amesema ameiomba wizara ya kilimo kuingilia kati wazalishaji wa mbolea ili iweze kushuka bei kwa kuwa wakulima wamekuwa wakishindwa kumudu ghalama za pembejeo.

“Lakini vile vile wananchi wanaweka mbolea kwenye mazao lakini hawapati matokeo vizuri niliomba wizara ilete vifaa vya kupimia udongo nashukuru serikali walisema wataleta vifaa kila halmashauri nchini na hili la pembejeo watalifanyia kazi.”alisema Kamonga
Mbunge wa jimbo la Ludewa mkoani Njombe,Joseph Kamonga akizungumza na wafanyabiashara pamoja na wakulima jimboni mwake ili kupata maoni atakayokwenda nayo bungeni huku akiahidi kushughulikia swala la bei ya mahindi.
Baadhi ya wafanyabiashara na wakulima wilayani Ludewa wakimsikiliza mbunge wao pamoja na kuwasilisha hoja kwa ajili ya maendeleo ya jimbo hilo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...