Shirika lisilo la kiserikali la CAMFED Tanzania linalo lenga kuwawezesha watoto wa kike wanaoishi katika mazingira hatarishi kwa kuwapatia ufadhili wa mahitaji muhimu ya shule limezindua rasmi mpango huo katika Wilaya ya Chamwino na kuifanya Wilaya hiyo kuwa miongoni mwa Wilaya 33 hapa nchini zitakazoendelea kunufaika na shirika hilo.

Mapema akizindua program ya mradi huo Afisa Tarafa Itiso ndugu Remidius Emmanuel (Aliyemwakilishi Mkuu wa Wilaya ya Chamwino Mhe.Vumilia Nyamoga ) alipongeza Shirika la CAMFED kwa kazi nzuri wanayoifanya katika nchi ya Tanzania na kusaidia vipaumbele vya Serikali kama ilivyoainishwa katika Mpango wa Maendeleo wa Sekta ya Elimu 2017/18-2020/21, ikiwa ni pamoja na kuwepo na usawa na ushiriki wa wanafunzi shuleni; kuboresha matokeo ya kujifunza na mazingira ya kujifunzia kwa watoto; na elimu kwa ajili ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi ambayo na kuhusisha program stahiki za maendeleo ya ujuzi kwaajili ya kujifuza, uwezeshwaji binafsi na ajira kwa vijana.
"Nimesikia kuwa tangu kuanzishwa kwake mpaka kufikia mwaka 2020, CAMFED kwa kushirikiana na Serikali mmeweza kuwafikia jumla ya wanafunzi wa kike 54,622 kwa ufadhili katika ngazi ya shule za sekondari wanaotoka katika mazingira magumu lakini furaha yangu kubwa ni kusikia kuwa katika Mpango mkakati wenu wa Miaka Mitano Ijayo (2020-2025) Wilaya yetu ya Chamwino inakua ni moja ya Wilaya zitakazonufaika na miradi ya CAMFED. Hii ni habari njema na faraja kubwa kwetu kwakua sasa wasichana wanaotoka kwenye mazingira magumu katika Wilaya ya Chamwino watafikiwa na ufadhili huu" Remidius 

Kupitia Mpango Mkakati huo, Ufadhili huu unalenga kuwafikia jumla ya wasichana 828,906 katika mikoa 9 na wilaya 33 nchini wakiwemo wasichana 1, 000 kutoka shule 27 za Serikali Wilayani Chamwino.
Kwa upande wake Mkuu wa Idara ya Miradi Taasisi ya CAMFED Bi. Nasikiwa Duke alitaja dhumuni la tukio hilo kuwa ni hatua muhimu ya uzinduzi wa mradi huo katika Wilaya ya Chamwino na kwamba mradi huo unalenga kusaidia watoto wa kike wanaotoka mazingira hatarishi kuwawezesha kupata mahitaji ya msingi kwa muda wote wa masomo yao. 

Alizitaja baadhi ya changamoto zinazowakabili watoto wanaotoka katika mazingira hatarishi kuwa ni pamoja na hali ngumu ya kiuchumi inayopelekea kushindwa kumudu mahitaji ya msingi ya mwanafunzi mfano vitabu na sare za shule pamoja na mahitaji ya muhimu kwa mwanafunzi, lakini wapo wanaotembea umbali mrefu kuja shuleni na wengine kukosa chakula, mazingira haya huwaweka karibu na vishawishi ambavyo hupoteza ndoto za maisha yao. 
"Tafsiri ya mtoto anaetoka katika mazingira hatarishi ni ile iliyotolewa na Wizara ya Afya, na mchakato wa kuwapata wanafunzi hao unaanzia shuleni na CAMFED tunafanya kazi kwa kushirikiana na Maafisa ustawi wa jamii na Idara za Elimu Msingi na Sekondari hatua ambayo hupelekea kuwapata watoto wenye sifa na vigezo husika" Bi. Nasikiwa

Uzinduzi huo uliofanyika katika Ukumbi wa Serikali ya Kijiji Chamwino Ikulu (Chamwino, Mkoani Dodoma) na kuhudhuriwa na makundi mbalimbali ikiwa ni pamoja na uwakilishi kutoka ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino, Idara ya Maendeleo ya Jamii na Afisa Elimu ngazi ya Mkoa, na Wakuu wa Idara ya Elimu Msingi na Sekondari Wilaya ya Chamwino, Wakuu wa Shule za Sekondari, uwakilishi wa Wanafunzi wa kike na ujumbe ulioambatana na Shirika hilo la CAMFED.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...