Charles James, Michuzi TV

WAZIRI wa Katiba na Sheria, Dk Mwigulu Nchemba amesema Serikali ya awamu ya tano itaendelea kulinda kwa nguvu za Mtoto na kwamba haitomvumilia mtu yeyote ambaye atamfanyia ukatili au udhalilishaji mtoto mdogo.

Kauli hiyo ameitoa leo jijini Dodoma wakati akizindua mpango mkakati wa pili wa maboresho endelevu ya haki ya mtoto nchini ya mwaka 2020 hadi 2025 yenye lengo la kutokomeza ukatili dhidi ya watoto.

Waziri Nchemba pia amemuagiza Katibu Mkuu wa Wizara hiyo kuhakikisha kuwa wanaupitia mpango huo na kuufanyia maboresho kwa kuutafsiri kwa lugha ya kiswahili ili uweze kuwafikia watu wengi zaidi.

Dk Nchemba amesema uzinduzi wa mpango huo ni nia ya serikali katika kupambana na ukatili kwa Watoto na kuimarisha haki ya mtoto na kutaka mpango huo utafsiriwe kwa lugha adhimu ya Kiswahili ili kila mmoja aweze kuuelewa mpango huo.

" Huu mpango wa kwanza uliotekelezwa kuanzia mwaka 2012 hadi 2017 kuna mazuri yamefanyika lakini tumekuja na mpango huu ambao umeboreshwa zaidi na hii ni nia serikali kuhakikisha inalinda haki ya mtoto,

Nitoe maagizo kwa Katibu Mkuu kuhakikisha mpango huu utafsiriwe kwa lugha ya Kiswahili sote tunajua hii ni lugha ya ukombozi kwa nchi yetu hivyo ni vema mpango huo utafsiriwe kwa lugha ambayo kila mmoja wetu ataielewa wakati ya kuitekeleza,” Amesema Dkt Nchemba.

Amesema mpango huo umelenga zaidi katika kuongeza uelewa wa haki ya mtoto katika jamii kwa Watoto na wadau mbalimbali, kuimarisha mfumo wa utoaji haki kwa mtoto, kuimarisha mfumo wa ulinzi na usalama wa mtoto, kuboresha sera na sheria, kuimarisha uratibu na ufuatiliaji wa utekelezaji wa mpango mkakati huu.

Amesema Wizara ya katiba na sheria kwa kushirikiana na jukwaa la haki mtoto itaendelea kuratibu na kufuatilia mwenendo na utekelezaji wa mkakati huu kwa kushirikana na Wizara nyingine zinazotekeleza mpango huo.

Ametoa wito kwa wadau na jamii mbalimbali kwa ujumla kushiriki kikamilifu katika kutekeleza mpango mkakati huo ili Watoto waweze kulindwa na kufurahia upatikanaji wa haki kwa wakati kwa kuwa haki ya mtoto ni  mtambuka.

Waziri Nchemba amezitaka taasisi, mashirika, wadau na jamii kwa ujumla wakati wa kutekeleza mpango huo kuangalia upande wa pili kwa kumuangalia mtoto huyo kwa Maisha yake ya baadaye na badala yake wajue kutofautisha kuvunja haki ya mtoto na maandalizi ya mtoto kwa Maisha yake ya baadaye.

Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria Prof Sifuni Mchome, amesema katika kulinda haki ya mtoto Wizara imeandaa na kuratibu na kuutekeleza mpango huo wa pili ambapo wamefanya marekebisho mbalimbali ya sheria yote ni katika kulinda hali ya mtoto.

Jitihada nyingine ametaja kuwa ni kuongeza makahama zinazosikiliza haki za Watoto hadi kufikia mahakama 130 na kuwapa mafunzo maafisa 638 wa mahakama waliojengewa uwezo wa kusikiliza mashauri yanayohusu kesi za ukatili dhidi ya Watoto, na mawakili wa serikali na mawakili wa kujitegemea walijengewa uwezo wa kuendesha kesi kama hizo.

Amesema kesi mbalimbali za ukatili dhidi ya Watoto 63,023 zimesikilizwa na kuwapa haki sawa hata watoto wanaotoka katika kaya maskini ambapo walikuwa hawana uwezo wa kuwa na wakili waliweza kusaidiwa ili kuweza kupata haki yao.

Nae Mwakilishi mkazi wa Unicef hapa nchini, Shalini Baragua ameipongeza Serikali ya Tanzania kwa kuendelea kupambana kuhakikisha haki ya mtoto inalindwa katika ngazi zote mijini na vijijini.

Amesema ulinzi wa mtoto ni suala mtambuka hivyo ni wajibu wa kila mwanajamii kuhakikisha anakuwa mlinzi wa Watoto ili kujenga kizazi imara kwa miaka ijayo na kwa maendeleo ya taifa kwa ujumla.







 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...