Na Mwandishi Maalum – Dar es Salaam
JUMLA ya watu 561 wamepimwa viashiria vya magonjwa ya moyo bila malipo katika upimaji maalum uliofanywa na wataalamu wa magonjwa ya moyo wanawake wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).

Upimaji huo ulioenda sambamba na utoaji wa matibabu pamoja na kupewa rufaa kwa wale waliokutwa na matatizo ulifanyika kwa muda wa siku mbili katika viwanja vya Mbagala Zakheem vilivyopo wilayani Temeke ulikuwa ni maadhimisho ya siku ya wanawake Duniani tarehe 8, Machi 2021.

Akizungumza na waandishi wa habari hizi leo katika viwanja vya Mbagala Zakheem Mwenyekiti wa Wanawake wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete ambaye pia ni daktari bingwa wa usingizi na wagonjwa mahututi Anjela Muhozya alisema katika upimaji huo pia walitoa elimu ya lishe bora kwa afya bora ya Moyo.

Dkt. Anjela alisema kati ya watu 561 waliowapima asilimia 80 walikutwa na shinikizo la juu la damu kati ya hawa asilimia 50 walikuwa wanajijua kuwa na tatizo lakini hawakuweza kuendelea na huduma za matibabu kutokana na sababu mbalimbali za maisha, asilimia 30 hawakuwa wanajijua kabisa kama wanatatizo hilo hawa walianzishiwa matibabu.

Waliokutwa na matatizo asilimia 40 waliweza kukamilisha huduma ya matibabu katika viwanja hivyo hii ikiwa ni pamoja na kupewa dawa na ushauri na asilimia 20 walipewa rufaa ya kwenda kutibiwa katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete na Hospitali ya Temeke.

“Kati ya watu tuliowapima asilimia 10 hawakuwa na tatizo lolote la kiafya ila uzito wao ulikuwa mkubwa kitu ambacho ni hatari kwa afya ya moyo. Hawa tumewapa ushauri wa kubadili mfumo wa maisha katika ulaji wao wa vyakula pamoja kufanya mazoezi mara kwa mara”, alisema Dkt. Anjela.

Mkuu wa wilaya ya Temeke Godwin Gondwe aliwashukuru wataalamu wa JKCI kwa moyo wao wa upendo wa kuwafikiria wananchi wanyonge na kwenda kuwapa huduma ya upimaji na matibabu ya moyo bila malipo yoyote yale.

“Ninawashukuru sana kwa upendo wenu wa kuwafuata wananchi wanyonge na kuwapa huduma ya matibabu ya kibingwa ya moyo kama tunavyofahamu matitabu haya yanagharama. Kwa kuwafuata kwenu wananchi hawa wameweza kuokoa fedha ambazo wangelipia hospitali na kwenda kuzitumia katika matumizi yao ya kila siku”.

“Pia Afisa Ustawi wa jamii ameweza kuwasikiliza watu wenye shida za kijamii na kuwapa maelekezo ya jinsi gani wataweza kufika JKCI na kupata matibabu. Hii itawasaidia kutoogopa kufika pale kwa ajili ya kutibiwa kwa kuwa hawana uwezo wa kulipia gharama za matibabu”.

Gondwe alisema wilaya yake itaendelea kushirikiana na JKCI katika kuhakikisha wananchi wanyonge wanafikiwa na wataalamu wa taasisi hiyo na kuwaomba wananchi wa Temeke kutumia fursa hiyo ya upimaji wa afya zao bila malipo.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi alisema amefika katika viwanja vya Mbagala Zakheem kwa ajili ya kuwaunga mkono wanawake wa Taasisi hiyo kwa kufanya upimaji kwa wananchi.

“Kama mnavyoona tunafanya upimaji kwa wanawake na wanaume na wale ambao wamekutwa na matatizo wameanzishiwa matibabu kwa kupewa dawa na wengine watakuja JKCI kwa ajili ya matibabu ya kibingwa”.

“Taasisi yetu itaendelea kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanafikiwa na huduma za matibabu ya kibingwa pamoja na kupata elimu ya magonjwa hayo ambayo siyo magonjwa ya kuambukiza na kama mtu atakuwa na uelewa nayo ataweza kuyaepuka”, alisisitiza Prof. Janabi.

Naye Musa Kitimla ambaye ni mkazi wa Mbagala Kibondemaji alisema alisikia katika redio kuna huduma za upimaji wa moyo ambao utafanyika kwa muda wa siku mbili katika viwanja vya Mbagala Zakheem akaona ni muhimu kufika hapo kwa ajili ya kupima afya yake.

“Ninamshukuru Mungu nimefika hapa na kupata huduma mbalimbali za kupima afya na majibu yangu yameonekana sina tatizo lolote lile. Nitaendelea kuichunga afya yangu ili iendelee kuwa salama. Ninawasihi wananchi wenzangu wakisikia mahali kuna upimaji wa aina hii waende kwani licha ya kupima afya zao watapata ushauri pia”, alisema Kitimla.

Katika upimaji huo wananchi walipimwa urefu, uzito, shinikizo la damu (BP), sukari, Virusi vya Ukimwi na kupewa ushauri wa lishe bora. Kwa wale waliokutwa na matatizo ya moyo wamepewa rufaa ya kwenda kutibiwa katika Taasisi hiyo na Hospitali ya Temeke ili waweze kufanyiwa uchunguzi zaidi na kupatiwa matibabu.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...