Baadhi ya wakazi wa kijiji cha Nasomba katika kata ya Nalasi Mashariki wakiwa katika foleni ya kuchota maji ya bomba hii ikiwa ni mara ya kwanza kijiji hicho kupata maji ya Bomba tangu nchi ilipopata Uhuru mwaka 1961, kwenye mradi wa maji uilotekelezwa na Serikali kupitiaWakala wa usambazaji maji vijijini Ruwasa wilaya ya Tunduru. Picha na Muhidin Amri,Ruvuma.
====== ======= =========
TAKRIBANI watu 13,279 wa vijiji viwili vya Nasomba kata ya Nalas
Mashariki na Mbesa kata ya Mbesa wilayani Tunduru, wameanza kunufaika
na miradi mikubwa ya maji iliyogharimu kiasi cha shilingi milioni
253,117,473 zilizotolewa na Serikali kupitia wizara ya maji.
Meneja wa wakala wa maji vijijini na usafi wa mazingira Ruwasa wilaya ya
Tunduru Primy Damas alisema,miradi hiyo yote imekamilika kwa zaidi ya
asilimia 100 na na wananchi wameanza kupata huduma ya maji safi na
salama kwenye maeneo yao.
Damas alisema, mradi wa maji kijiji cha Nasomba umetekelezwa kwa
gharama ya shilingi milioni 150,554,761 zilizotolewa na Benki ya Dunia
ambapo zaidi ya wakazi 3,500 wamenufaika,ulianza kujengwa mwezi mei
2020 na kukamilika Desemba 2020 kwa kuwatumia mafundi wadogo(local
fundi).
Alisema, katika mradi huo kazi zilizopangwa kufanyika na zilizofanyika
ni kujenga tenki la juu la ujazo wa lita 50,000,nyumba ya
mitambo,ununuzi wa mabomba zenye ukubwa tofauti za umbali wa mita 3,200
na viungio vyake.
Damas alisema, kazi zingine zilizofanyika ni ununuzi na ufungaji wa
nishati na mfumo wa umeme wa jenereta,ununuzi na ufungaji wa pampu kwa
ajili ya kisima,uchimbaji mitaro,ulazaji mabomba na ufikiaji mitaro na
kujenga vituo 8 vya kuchotea maji.
Aidha, mradi wa maji Mbesa ulitengewa shilingi milioni 102,562,712
ambazo zinaendelea kutumika kwa ajili ya kuwaondolea kero ya maji
takribani wakazi wapatao 9779 wa kijiji hicho.
Alisema, kukamilika kwa miradi miwili ya Nasomba na Mbesa na ile
inayoendelea kutekelezwa na wakala wa maji vijijini na usafi wa
mazingira Ruwasa kwa ujumla inalenga kuhakikisha huduma ya maji inafika
karibu na wananchi,kuchochea shughuli mbalimbali za maendeleo na kumtua
mama ndoo kichwani.
Alisema, katika bajeti ya mwaka huu wizara ya maji imeipatia Ruwasa
wilaya ya Tunduru kiasi cha shilingi bilioni 2,582,124,451.2 kwa ajili
ya kukamilisha na kujenga miradi katika maeneo mbalimbali wilayani
humo.
Kwa mujibu wa Damas fedha za mfuko wa P4R shilingi ni 1,366,865,340,
mfuko wa PbR -111 shilingi 209,347,963,mfuko wa PbR IV shilingi
337,174,313, na mfuko wa maji wa Taifa shilingi 668,736,835.20.
Amewataka wananchi kutunza miradi hiyo, kuchangia huduma na kutumia
maji ya bomba kwa shughuli mbalimbali, badala ya kuendelea na tabia ya
kwenda mtoni au kutumia visima vya asili ambavyo hakuna maji safi na
salama kwa ajili ya matumizi ya binadamu.
Diwani wa kata ya Nalasi Mashariki Mohamed Mlehani alisema, katika kata
ya Nalas kuna vijiji vinne na kijiji cha Nasomba ndiyo kijiji cha kwanza
kupata maji ya Bomba yaliyoletwa na Ruwasa.
Alisema, kijiji cha Nasomba kulikuwa na shida kubwa ya maji ambapo
wananchi wake walilazimika kutumia umbali mrefu kutembea umbali wa km 3
hadi mto Ruvuma na km 5 hadi mto Luhuwingu kuchota maji kwa matumizi
yao ya kila siku.
Mlehani alieleza kuwa,vijiji vilivyobaki vina maji ya kupitia visima
vifupi na virefu vilivyochimbwa na taasisi mbalimbali za dini na
Halmshauri,hata hivyo bado yanayopatikana bado hayatoshelezi kulingana
na idadi kubwa ya watu.
Mkazi wa kijiji hicho Ali Halifa ameishukuru serikali kupitia wizara ya
maji kutekeleza mradi wa maji katika kijiji hicho ambao umemaliza shida
na mateso ya muda mrefu waliyopata wananchi kutokana na ukosefu wa
maji safi na salama.
Alisema, akina mama ndiyo waathirika zaidi wa changamoto ya maji kwakuwa
walilazimika kuamka saa 10 usiku kwenda kuchota maji mto Ruvuma na
kwenye visima vya asili licha maji hayo kutokuwa safi na salama hasa
wakati wa masika.
Katika hatua nyingine,mkazi wa kijiji cha Nasomba Hawa Said(67)
amepoteza maisha akiwa katika foleni ya kusubiri kuchota maji katika
moja ya vituo vya kuchotea maji kijijini hapo.
Hawa,alipoteza maisha kwa kile kinachodaiwa ni mstuko baada ya
kushuhudia kwa mara ya kwanza maji ya bomba yakitoka katika kijiji
hicho ambacho hakijawahi kupata maji safi na salama tangu uhuru wa
Tanganyika na hatimaye Tanzania mwaka 1961, badala yake wananchi
walitumia maji ya mto maarufu wa Ruvuma unaopatikana umbali wa km 3.
Mashuhuda ya tukio hilo akiwemo Diwani wa kata ya Nalas Mashariki
Mohamed Mlehani walisema,kabla ya kupoteza maisha Hawa alianguka na
kupoteza fahamu akiwa katika foleni na wananchi wengine ndipo
alipokimbizwa katika zahanati ya Nasomba kwa ajili ya kupatiwa matibabu
kabla ya kufikwa na umauti.
Mlehani alisema, marehemu alipata mstuko kutokana na furaha kubwa
aliyonayo mara baada ya kushuhudia maji ya bomba,katika mradi
uliotekelezwa na wakala wa maji na usafi wa mazingira Ruwasa wilaya ya
Tunduru.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...