Serikali
ya Tanzania itaendelea kutekeleza ujenzi na ukamilishaji wa miradi
mbalimbali ya kimkakati ikiwemo ile iliyopo katika mikoa inayopakana na
nchi jirani ili kuharakisha maendeleo ya maeneo hayo.
Hayo
yamesemwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Prof. Palamagamba John Kabudi, alipowaongoza Wajumbe wa mkutano wa
sita wa tume ya pamoja ya kudumu kati ya Tanzania na Burundi kutembelea
miradi mbalimbali ya kimkakati inayotekelezwa na Serikali katika mkoa wa
Kigoma.
Miradi
iliyotembelewa ni pamoja na Eneo Maalum la Uwekezaji wa Kigoma (Kigoma
Special Economic Zone-KiSEZ); Uwanja wa Ndege wa Kigoma, Bandari Kavu
ya Katosho na Bandari ya Kigoma pamoja na Kituo cha Pamoja cha Kutoa
huduma Mpakani (OSBP) kinachotarajiwa kujengwa katika eneo la Manyovu
mkoani Kigoma.
Akiwa
kwenye eneo Maalum la Uwekezaji, Prof. Kabudi na Wajumbe wengine
walijionea uwekezaji mkubwa uliofanywa kwenye eneo hilo na Kampuni
ijulikanayo kama Next Gen Solar wa kuzalisha umeme wa jua wa megawati
tano ambao utaanza kusambazwa rasmi kwa wakazi wa Kigoma mwezi Aprili
2021. Upatikanaji wa nishati hiyo ya umeme unatarajiwa kuwanufaisha
wakazi wa mkoa huo kiuchumi.
Kadhalika
Mhe. Prof. Kabudi na Wajumbe wengine walipata fursa ya kutembelea
kampuni ya Third Man Limited inayozalisha Asali ijulikanayo kama Upendo
(Upendo Honey) ambayo nayo imewekeza kwenye eneo hilo maalum la KiSEZ.
Katika maelezo yake kwa Mawaziri, Mkurugenzi wa Kampuni hiyo Bw. Alex
Scovic alisema kuwa Kampuni yake ambayo inachakata asali inayozalishwa
bila kutumia kemikali (organic) inanunua asali hiyo kutoka kwa wafugaji
wa nyuki zaidi ya 3,000 waliopo Kigoma na mikoa jirani kama Tabora,
Katavi, na Rukwa na baadaye kuiuza asali hiyo nje nchi hususan nchini
Marekani.
“Kampuni
yetu ni ya kwanza kuwekeza kwenye eneo hili. Tunazalisha Asali safi
isiyo na kemikali ambayo ina soko kubwa nje ya nchi hususan nchini
Marekani. Biadhaa zetu tunazitangaza kuwa zimetoka Tanzania” alisema.
Pia
alijulisha kuwa, Kampuni yake imeajiri zaidi ya vijana 60 wa kitanzania
na kwamba mbali na kuchakata asali, kampuni hiyo inazalisha nta ambayo
huuzwa nchini Ujerumani ambao huitumia kwa ajili ya kutengeneza
vipodozi. Kampuni ya upendo huzalisha zaidi ya tani 4,000 za asali kwa mwaka.
Katika
ziara yao kwenye eneo la Bandari Kavu la Kitosho, Mawaziri na Viongozi
wengine walijulishwa kuwa eneo hilo limeanzishwa maalum kwa ajili ya
kurahisisha usafirishaji na uhifadhi wa mizigo na bidhaa mbalimbali
zinazokwenda Burundi kutokea Bandari za Tanzania. Tayari eneo hilo
limepata mzabuni atakayeanza ujenzi mwaka huu. Pia
Mawaziri hao walitembelea Bandari ya Kigoma na kupata fursa ya kujionea
meli kongwe na ya kihistoria ya MV Liemba ambayo ina miaka 108 tangu
itengenezwe, MV Mwongozo na MV Sangara ambazo zote zitaanza kufanyiwa
ukarabati ili kuziwezesha kuendelea kutoa huduma kwa wananchi wa Kigoma
na kutoka nchi jirani.
Wakiendelea
na ziara ujumbe huo ulitembelea Uwanja wa Ndege wa Kigoma ambapo
ulipata maelezo kutoka kwa Meneja wa TANROAD wa Mkoa wa Kigoma, Mhandisi
Narcis Choma kuwa, mradi huo unalenga kupanua na kukarabati maeneo
mbalimbali ya Uwanja huo ikiwa ni pamoja na kuongeza urefu wa barabara
ya kuruka na kutua ndege ambayo awali ilikuwa na urefu wa mita 1800 na
sasa mita 1,300 zitaongezwa ili kuwezesha ndege kubwa kutua. Pia mradi
unalenga kujenga jengo la abiria, maegesho ya ndege, usimikaji wa taa
na mitambo ya kuongozea ndege, ujenzi wa jengo la kuongozea ndege,
maegesho ya magari pamoja na uzio wa usalama.
Mhe.
Prof. Kabudi pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje wa Burundi, Mhe. Balozi
Albert Shingiro walihitimisha ziara yao kwa kutembelea eneo
kitakapojengwa Kituo cha Kutoa Huduma kwa Pamoja Mpakani (OSBP) cha
Manyovu na Mugina kwa upande wa Burundi. Wakiwa Manyovu waliweza
kutembelea maeneo ambayo vituo hivyo vitajengwa kwa upande wa Tanzania
na upande wa Burundi pamoja na kupokea taarifa ya mradi huo ambapo
walijulishwa kwamba tayari usanifu wa ujenzi wa kituo hicho cha Manyovu
ambacho kitakuwa cha aina yake umeanza na utakamilishwa mwishoni mwa
mwezi Machi 2021.
Akitoa
hotuba kuhitimisha ziara kwenye miradi hiyo, Prof. Kabudi alisema
Tanzania inawekeza kwenye miradi hiyo ili kurahisisha ufanyaji biashara
na uwekezaji kati ya Tanzania na nchi mbalimbalii inazopakana nazo
ikiwemo Burundi. Kwa upande wake, Mhe. Balozi Shingiro alipongeza
jitihada hizo za Tanzania na kuahidi kutumia fursa za miradi hiyo ambayo
mingi inalenga kuimarisha ushirikiano baina ya Tanzania na Burundi.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...