Na Lillian Shirima, Habari MAELEZO
SIKU ya Wanawake Duniani inaadhimishwa Tarehe 8 Machi ya kila mwaka ambapo kwa mwaka huu 2021 maadhimisho haya hapa nchini yanafanyika katika ngazi ya mkoa kwa kushirikiana na wadau mbalimbali nchini.

Serikali kupitia Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imesema, yapo mambo mengi ya kujivunia yaliyofanyika hapa nchini na mengine yanaonekana kwa macho hususan jitihada za kuhakikisha kunakuwepo na usawa wa kijinsia katika jamii.

Kama ilivyoainishwa katika Kaulimbiu ya Mwaka 2021 ‘ Wanawake Katika Uongozi: Chachu Kufikia Usawa’; Serikali na Watanzania kwa ujumla tumekuwa mstari wa mbele kuhakikisha kwamba Wanawake wanapata haki sawa kama ilivyo kwa Wanaume.

Katika mahojiano yake na Idara ya Habari MAELEZO, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini kutoka katika Wizara hiyo, Prudence Costatine amesema, ulingo wa Maendeleo ya Wanawake (Beijing) ni moja ya chachu iliyoleta mafanikio mengi katika kuwawezesha Wanawake, kisiasa, kiuchumi na kijamii ambapo wameshuhudiwa wanawake wengi wakishika nyadhifa mbalimbali Serikalini.

„Wanawake wameshika nyadhifa kubwa ndani ya Serikali, Taasisi, Idara na Mashirika ya Umma pamoja na Sekta Binafsi. Haya yote ni mafanikio yaliyopatikana kutokana mapambano ya kupigania haki za mwanamke ndani na nje ya nchi ya Tanzania”, amesema Costantine

Ameongeza kuwa, kufuatia hali hiyo, Tanzania kama nchi imeshuhudia nafasi ya uongozi wa ngazi za juu serikalini ikishikwa Mhe. Samia Suluhu Hassan ambaye ni Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kuongezeka kwa idadi ya Mawaziri katika Serikali, kupata Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Anne Makinda(Mstaafu), Naibu Spika wa Bunge Dkt. Tulia Ackson, Wabunge, Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Majaji na Wakuu wa Taasisi mbalimbali za Serikali na ndani ya sekta binafsi.

Aidha, amesema Tanzania inaendelea kujivunia mengi katika sekta ya elimu ikiwemo ongezeko la udahiri kwa wanafunzi katika ngazi ya elimu ya awali na elimu ya msingi ambapo kwa sasa uwiano ni 1:1 ambapo kumekuwa na nafasi sawa katika kuandikishwa kujiunga darasa la kwanza pamoja na ongezeko la wanafunzi wa kike wanaojiunga na elimu ya juu ikilinganishwa na hali ilivyokuwa hapo awali.

Mafanikio katika sekta ya elimu yameijengea jamii uwezo wa kutoa taarifa mbalimbali kuhusu vitendo vya unyanyasaji dhidi ya wanawake na watoto na hivyo Serikali kufuatilia kwa ukaribu na kutafuta mbinu za kukabiliana vitendo hivyo.

Ametoa mfano wa kuwepo kwa mkakati wa kitaifa wa kutokomeza vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto (MTAKUWWA) ambao unalenga kuhakikisha vitendo vya ukatili vinapungua kwa asilimia 50 ifikapo mwaka 2022. Pia, wanawake wamewezeshwa kupata mafunzo kwa ajili ya kuwajengea uelewa kuhusu masuala ya ujasiriamali na namna ya kuboresha bidhaa wanazozizalisha kwa kutumia vifungashio vinavyokidhi matakwa ya soko la ndani na nje ya mipaka ya Tanzania.

Baadhi ya Wanawake wajasiriamali wamepata fursa ya kuunganishwa na wafanyabiashara na taasisi za kimataifa ikiwa ni njia mojawapo ya kuwajengea uwezo ambapo wameweza kunufaika na utaratibu wa mikopo kutoka halmashauri chini ya utaratibu wa asilimia nne (4) kwa wanawake, asilimia nne (4) kwa vijana na asilimia mbili (2) kwa wenye ulemavu.

Akieleza zaidi, Contantine amesema kumekuwa na makongamano mbalimbali katika ngazi ya kitaifa na ngazi ya mikoa ambapo wanawake na wataalam wa nyanja tofauti wamekuwa wakiwasilisha mada kuhusu namna ya kuwawezesha kiuchumi na kijamii.

Amebainisha kuwa makongamano hayo yamekuwa yakifanyika katika mikoa mbalimbali ikiwemo Mbeya, Singida, Arusha, Katavi na Simiyu na Dodoma kwakuwa lengo la serikali ni kuhakikisha makongamano hayo yanafanyika katika mikoa yote Tanzania Bara na kuleta matokeo chanya

Maadhimisho ya siku ya wanawake duniani yalianza mwaka 1911, kufuatia maandamano ya Wanawake wafanyakazi katika Sekta ya Viwanda nchini Marekani waliokuwa wakipinga mazingira duni ya kazi na vitendo vya unyanyasaji katika ajira ikiwemo kulipwa mshahara mdogo kwa kazi sawa na ile ya wanaume.

Mwaka 1945 Umoja wa Mataifa ulipitisha Azimio la Nchi Wanachama kuadhimisha siku hiyo ambapo nchini Tanzania siku ya Wanawake Duniani ilianza kuadhimishwa kitaifa kuanzia mwaka 1997.

Mwaka 2005 Serikali ilielekeza maadhimisho haya yafanyike kila baada ya miaka mitano (5) ili kutoa fursa kwa Serikali na wadau kufanya tathmini ya hatua mbalimbali za usawa wa kijinsia na uwezeshaji wanawake. Kwa kuzingatia tamko hilo, Serikali ilielekeza kuwa katika miaka mingine, maadhimisho haya yatafanyika Kimkoa ambapo kila Mkoa utaandaa utaratibu wao kulingana na mazingira yao.

Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto inatoa wito kwa kila mwanajamii kutimiza wajibu wake, kuhakikisha changamoto zinazojitokeza zinaondoka na kwamba minyororo ya ubaguzi wa kijinsia inakatwa ili kuijenga dunia yenye kizazi cha usawa.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...