Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam 

 KATIKA kuadhimisha siku ya Wanawake Duniani leo Machi 8, Ubalozi wa Uswisi (Switzerland)  kwa kushirikiana na Mfuko wa Kuendeleza Sekta ya Fedha Tanzania (FSDT), watazindua utafiti wa Huduma jumuishi za fedha kwa Vijana wa Vijijini katika hafla itakayofanyika kwa njia ya mtandao itakayofanyika saa 8;00 mchana. Utafiti huo unalenga kusambaza maarifa ya kina kuhusu tabia na changamoto za vijana wa vijijini nchini Tanzania hususani wasichana,wenye umri wa miaka kati ya 16 na 24 katika masuala ya fedha.

Taarifa ya FinScope Tanzania ya mwaka 2017 ilibainisha kuwa wanawake na wanaume wa vijijini wenye umri kuazia miaka 16 hadi 24 waliokadiliwa kufikia  takriban watu milioni 4.4 walikuwa sehemu ya idadi ya watu waliotengwa katika huduma za fedha, huku asilimia 45 wakiwa hawajachukua huduma yoyote ya fedha  rasmi au isiyo rasmi.

Utafiti wa Fedha jumuishi kwa Vijana wa Vijijini unaonyesha wasifu halisi wa vijana wa vijijini ili kuwezesha ufumbuzi/ubunifu wa bidhaa/huduma zinazolenga kundi hili la soko linalojitokeza. Inachunguza zaidi mahitaji, mtamanio na hali ya sasa ya kiuchumi ya vijana wa vijijini, na jinsi mawasiliano ya sasa na mikakati ya watoa huduma za fedha kuingia sokoni, mipango ya uwezeshaji vijana na sera mbalimbali zinavyowaakisi.

“Mfuko wa Kuendeleza sekta ya Fedha Tanzania (FSDT) walibainisha kuwa Vijana wa Vijijini ni kundi muhimu sana katika kuleta mabadiliko kupitia huduma jumuishi za fedha, hivyo ushirikiano baina yake na Ubalozi wa Uswisi umewasilisha fursa nzuri kuimarisha uelewa wa ndani wa kundi hili”, alisema Bwana Sosthenes Kewe, Mkurugenzi Mtendaji wa FSDT

Utafiti huu unataka kutarifu mikakati ya maendeleo ya uchumi kwa vijana wa vijijini, huduma za fedha na mikakati inayolenga kuongeza ajira kwa vijana wa vijijini kwa kujiajiri kupitia huduma za fedha jumuishi zilizoboreshwa. Utafiti wa Vijana ulitumia jicho la jinsia katika  taarifa nzima kubainisha changamoto na fursa mahususi zilizopo kwa ajili ya mwanamke wa vijijini.   

“Kuongeza huduma jumuishi za fedha kwa vijana  vijijini ni changamoto kubwa – na kuongeza huduma jumuishi za fedha kwa vijana wadogo wa kike vijijini ina umuhimu wa kipekee kwani hawajanufaika kiusawa. Utafiti huu unachunguza kiini cha tofautiza usawa  wa kijinsia unaozuia kuwajengea uwezo wanawake”, alisema Balozi wa Uswisi Didier Chassot. “Upatikanaji na matumizi ya  bidhaa na huduma bora za fedha ni muhimu kwa ukuaji wa  uchumi jumuishi na katika kupunguza umasikini”.   

Tukio hili litasambaza ufahamu unaoweza kufanyiwa kazi kutokana na utafiti uliolenga kutatua changamoto mbalimbali zinazolikumba  kundi lengwa la vijana. Kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Wanawake, tukio hilo litazingatia hasa wasichana. Utafiti wa Fedha jumuishi kwa Vijana Vijijini ulifanywa na taasisi ya  IPSOS kwa kushirikiana na Fundacion Capital.

Uswisi imekuwa ikiunga mkono miradi ya pande mbili na ile ya kikanda nchini Tanzania tangu mwanzoni mwa miaka ya 1960. Mwaka 1981, Tanzania ikawa nchi ya kipaumbele kwa misaada rasmi ya maendeleo kutoka nchi ya Uswisi na inaendelea kupokea takriban dola za Marekani milioni 22 kila mwaka. Mpango wa Ushirikiano wa Uswisi nchini Tanzania 2021 - 24 unalenga kuwawezesha vijana, hasa wasichana masikini, kuendelea kijamii na kiuchumi kupitia matokeo matatu mtambuka ya kisekta: (i) Kuimarisha taasisi za serikali, (ii) Kukuza nafasi za uraia na (iii) Kuboresha maisha ya vijana. Mwaka 2021 inatimia miaka 40 ya ushirikiano wa maendeleo baina ya Uswisi na Tanzania.

Mfuko wa Kuendeleza sekta ya Fedha Tanzania (FSDT) ni taasisi inayo jihusisha na ujenzi wa masoko wezeshi kwa kusaidia kutatua vikwazo na changamoto zilizoko sokoni na kuchagiza ukuaji wa sekta ya fedha inayolenga  kupunguza hali ya umaskini wa watu na kipato. FSDT imejikita katika tasnia kuu nne (4), yaani Wanawake, Vijana waishio Vijijini,biashara na ujasiriamali na wakulima wadogo na wakati waliopo vijijini.

FSDT inatumia wigo mpana wa nyenzo, miundombinu na utaalamu wa kifedha kama mikopo nafuu, udhamini na misaada ya kifedha au ruzuku katika kuchochea ubunifu miongoni mwa Watoa Huduma za Fedha kwa ajili ya kuendeleza sekta ya fedha na mifumo yake. Kwa kutumia nafasi yake ya ushawishi na kitovu cha mawazo mapya/mbadala katika huduma jumuishi za fedha, FSDT inasimama kama muwezeshaji katika sekta ya fedha kwa kutumia muunganiko wa mbinu na utaalamu wa kuitisha mijadala, uzengezi na kufadhili majadiliano yanayogusa wadau mbalimbali ikiwa ni pamoja na kufanya tafiti mbalimbali na kuchochea shughuli za ubunifu katika sekta ya fedha.

Kutoa matokeo ya tafiti na kuzalisha machapisho juu ya sekta ya fedha ni moja ya nguzo muhimu katika kazi za FSDT zinazoiwezesha taasisi kuelewa kwa kina hali ya Huduma za Kifedha Jumuishi katika nchi yetu na kusaidia utoaji wa maamuzi unaozingatia Ushahidi wa kitafiti kwa wasimamizi wa sekta,na watunga sera na mwisho wahusika wenyewe, yaani  watoa huduma za kifedha. Ushahidi huu wa kitafiti pia ndio chachu na hutumika katika kubuni na kutengeneza miradi au shughuli zinazokidhi mahitaji halisi ya sekta ya fedha.

 

 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...