Na Paschal Dotto-MAELEZO
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amekula kiapo Machi 19, 2021, baada ya aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano, Hayati Dkt. John Pombe Magufuli kufariki Dunia Machi 17, 2021, Jijini Dar es Salaam. 
 
Rais Samia, amesema kuwa taifa limepoteza kiongozi shupavu na mzalendo aliyeipenda nchi yake na kujali watu wake katika kutekeleza mapinduzi makubwa ya uchumi wa wananchi wa Tanzania.

 “Tumepoteza kiongozi shupavu, madhubuti, mwenye maono, mpenda maendeleo, mwana mwema wa Bara la Afrika na mwanamapinduzi wa kweli, Mhe. Magufuli alikuwa chachu ya maendeleo kwa nchi yetu”, Mhe. Samia. 

 Amebainisha  kuwa Hayati, Rais. Magufuli aliweza kuibadili taswira ya Tanzania kwa kumtegemea Mungu katika mipango na mikakati ikiwemo utekelezaji wa miradi mikubwa na  wakati wa uhai wake alifanya naye kazi pamoja na kujifunza mambo mengi.

 Ameongeza kuwa katika kipindi chote alichofanya kazi na  Hayati, Magufuli alikuwa akimuelekeza kwa vitendo namna anavyotaka nchi iende, nini kifanyike na alimfundisha mengi, kumlea na kumuandaa vya kutosha.

Aidha, Rais Samia amewaomba Watanzania kushikamana, kuwa na moyo wa subira na  kujenga umoja katika kipindi hiki kigumu cha kuondokewa na mpendwa wao Hayati, Rais John Pombe Magufuli na amewahakikishia kuwa nchi iko imara.

“Niwaombe Watanzania tuwe na moyo wa subira, tujenge umoja na mshikamo katika kipindi hiki kigumu, niwahakikishie kuwa tuko imara na sisi viongozi tumejipanga vizuri kuendeleza pale mwenzetu alipoishia hakuna jambo litakaloharibika”, Rais Samia.

Akitangaza  ratiba ya kumuaga amesema kuwa  Hayati, Rais Magufuli ataanza kuagwa Machi 20 ambapo Ibada ya kumuombea itafanyika katika kanisa la Mtakatifu Peter Oysterbay  na baadaye mwili utapelekwa katika Uwanja wa Uhuru kwa viongozi kuuaga. Machi 21 Wakazi wa Dar es Salaam watapata nafasi ya kumuaga mpendwa wao katika Uwanja wa Uhuru, Machi 22  Wakazi wa Dodoma watamuaga,  Machi 23 wakazi wa  Mwanza watapata nafasi ya kumuaga mpendwa wao na  Machi 24 Hayati Rais Magufuli ataagwa Mjini Chato ambapo Machi 25, 2021 atazikwa nyumbani kwake Chato.

Rais Samia ametoa rambirambi kwa familia ya  mjane wa Hayati, Rais Magufuli, Mama Janeth Magufuli, watoto, ndugu na jamaa kwa  kuondokewa na mpendwa wao na  taifa linaungana nao katika kipindi hiki kigumu cha msiba mzito na amewataka wawe na subira.

Pia ametoa rambirambi kwa Watanzania wote kwa kuondokewa na kipenzi chao, Hayati, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli kwani Watanzania hawakutarajia jambo hilo.

“Natoa rambirambi kwa wananchi wote wa Tanzania kwa pigo hili kubwa,  ni msiba mzito ambao hatukutarajia, sote tunafahamu jinsi Rais Magufuli alivyoipenda nchi, alivyowapenda Watanzania na kujitoa kwa watu wake kwa dhamira ya dhati na nia njema ya kuibadilisha tasirwa ya nchi yake.”Rais Samia.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...