Na. Shukrani Kawogo, Njombe.

Wananchi wa kata ya Makonde wilayani Ludewa mkoani Njombe wameishukuru serikali kwa kuwaboreshea kituo cha afya na kuwa cha kisasa ambacho kipo katika hatua za mwisho za ujenzi wake kinachogharimu kiasi cha shilingi milioni 700 ambapo milioni 500 kwaajili ya ujenzi wa majengo matano na milioni 200 kwaajili ya ununuzi wa vifaa tiba.

Pongezi hizo wamezitoa baada ya mbunge wa jimbo la Ludewa Joseph Kamonga kufanya ziara katika kata za ukanda wa mwambao ambazo ni Lifuma, Lumbila, Kilondo,ikiwemo na kata hiyo ya Makonde akiwa ameambatana na kamati ya siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa lengo la kusikiliza changamoto mbalimbali zinazowakabili wakazi wa ukanda huo na kusema kuwa kituo hicho kinategemewa na wakazi zaidi ya 2000 wa kata hiyo pamoja na wananchi wengine kutoka kata za jirani.

Ruben Jonas ni mmoja wa wakazi wa kata hiyo amesema kuwa kituo hicho kikikamilika kitakuwa ni msaada kwao kwani kitawapunguzia kufanya safari kwenda katika hospitali ya wilaya kutibiwa ambapo hospitali hiyo ipo mbali na ukizingatia mazingira ya usafiri si rafiki.

Amesema kwa sasa wanapata tabu kwani wanatumia gharama kubwa kusafiri kwenda hospitali ya wilaya na muda mwingine wamekuwa wakikutana na dhoruba ziwani kitu ambacho ni hatari kwa maisha yao.

Aidha kwa upande wa mganga mfawidhi wa kituo hicho cha afya David Mwaka ameiomba serikali kupitia mbunge huyo kuwasaidia boti ya kubebea wagonjwa ambayo itawarahisishia kuwasafirisha pindi wanapohitajika kupelekwa katika hospitali ya wilaya.

sambamba na ombi hilo la boti pia ameomba kuongezewa watumishi wa afya kwakuwa kituo hicho kinahitaji watumishi 36 na kwa sasa kuna watumishi sita ambapo kuna mganga mmoja, muuguzi mmoja pamoja na wahudumu wanne na kupelekea kuwepo upungufu wa watumishi 30.

"Kutokana na uhaba huu wa watumishi inatulazimu kufanya kazi katika mazingira magumu kwani kituo cha afya kinapaswa kuwa wazi masaa 24 hivyo tumekuwa tukipeana zamu na watumishi wenzangu ili kuhudumu mchana na usu ili wananchi wasekose huduma" Alisema Mwaka.

Naye diwani wa kata hiyo Crispin Mwkasungura amesema majengo hayo yakikamilika yatakuwa msaada mkubwa kwa wananchi wa tarafa nzima ya mwambao kwani kitakuwa kinatoa huduma za upasuaji hasa kwa wajawazito ambazo kwa sasa hazipatikani.

Amesema kwa sasa huduma hizo za upasuaji wanazifuata katika hospitali ya wilaya au wanalazimika kwenda matema mkoani Mbeya ili kupata huduma hizo kitu ambacho kinawafanya watumie gharama kubwa za usafiri na huduma nyinginezo.

Ameongeza kuwa pamoja na changamoto hizo za kituo hicho cha afya pia wanakabiliwa na uhaba wa walimu, miundombinu ya barabara, maji, uboreshaji uvuvi wa kisasa katika ukanda wote wa mwambao, umeme pamoja na huduma ya mawasiliano ya simu.

Kwa upande wa mbunge wa jimbo hilo Joseph Kamonga amesema changamoto zote amezipokea na baadhi ya changamoto hizo tayari ameshaanza kuzifanyia kazi kwa kuzitafutia ufumbuzi.

Amesema kuhusu kuwepo kituo cha meli katika kata hiyo tayari ameshaanza kuwasilisha ombi hilo katika mamlaka husika na ataendelea kufuatilia mpaka atakapofanikisha suala hilo huku kuhusiana na watumishi amesema ataendelea kuikumbusha serikali kuleta watumishi hao katika sekta mbalimbali zenye mapungufu.

Pia amesema katika kukamilisha ujenzi wa vituo mbalimbali vya afya atakuwa sambamba nao katika kushirikiana nao kwani wananchi wamekuwa wakijitoa sana katika ujenzi huo hivyo jasho la wananchi halipaswi kupotea bure.

Sanjari na hayo pia mbunge huyo aliweza kutembelea shamba darasa la mihogo katika kata ya Lifuma ambalo limeandaliwa kwa mbegu alizowasaidia wananchi hao wa mwambao pamoja na tarafa ya masasi ambazo zina sifa ya kuzalisha kwa muda mfupi ukilinganisha na mbegu ambazo wanazitumia sasa ambazo wanavuna baada ya mwaka mmoja hadi miwili.

Kamonga alifurahishwa na shamba hilo kwani mbegu hizo zilikuwa zimechipua vizuri ambazo alizitoa Butihama na kuwaletea wananchi hao ambapo ameahidi kuendelea kuleta mbegu nyingine zaidi katika msimu ujao wa mvua.

Baadhi ya majengo ya kituo cha afya cha Makonde
Mbunge wa jimbo la Ludewa Joseph Kamonga (kushoto) akiwa na baadhi ya viongozi wa chama cha Mapinduzi anayefuata ni Katibu CCM wa wilaya hiyo, mwenyekiti wa CCM wilaya Stanley Kolimba pamoja na mwenyekiti wa UWT wilaya ya Ludewa.

 Mbunge wa jimbo la Ludewa Joseph Kamonga(mwenye shati jeupe) akiongea na wananchi wa kata ya Makonde wakati akikagua kituo cha afya cha kata hiyo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...