Na Mwandishi wetu, Mirerani

Wanawake wachimbaji wa madini ya Tanzanite wa Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, wameiomba Serikali kuwaruhusu waingie ndani ya migodi yao wanayoichimba.

Wanawake hao wachimbaji wametoa ombi hilo kwenye semina ya ya uchimbaji madini iliyofanyika jana mji mdogo wa Mirerani na kuandaliwa na shirika la mazingira na haki za wanawake la Envirocare.

Mmoja kati ya wanawake wanaomiliki mgodi wa madini Stella Shayo amesema wanawake pia wana haki ya kuingia kwenye migodi yao pindi wakiwa wanaichimba.

"Tunapaswa kupata ruhusa ya kuingia katika migodi yetu tunayochimba kwani hakuna tatizo lolote pindi wanawake wakizamia migodini kwani wapo waliowahi kufanya hivyo," amesema Shayo.

Mmoja kati ya watoa mada Dk Curtis Msosa amesema hakuna ubaya kwa wanawake kuruhusiwa kuingia mgodini kwani mmiliki mmoja Pili Hussein alishawahi kuingia mgodini na hakudhurika.

"Pia wapo waandishi wa habari wanawake walishawahi kuingia ndani ya mgodi wa madini ya Tanzanite na hakupata tatizo lolote lile pindi wakiwa mgodini," amesema Dk Msosa.

Hata hivyo, ofisa mazingira wa Tume ya madini, Nelusigwe Mwakatobe amesema hakuna sheria ya madini inayokataza wanawake kuingia katika migodi wanaochimba.

Mwakatobe amesema wanawake hao wanapaswa kuingia ndani ya migodi ambayo ni imara na yenye usalama ili isitokee ajali pindi wakiingia mgodini.

Mjumbe wa chama cha wanawake wachimbaji madini nchini (Tawoma) Rachel Njau amesema miongoni mwa changamoto zinazowakabili wanawake hao ni kulipia leseni ambayo wanachangia na wanaume.

"Unakuta kwenye zile mita 50 kwa 50 kuna migodi hata minne ya watu tofauti hivyo wanawake huwa ndiyo wanalipa ada ya leseni badala ya kulipa wote kwa pamoja," amesema Njau.

Meneja mradi wa shirika la kutetea haki za wanawake na mazingira (Envirocare) Amos Mbwambo amesema wamefanya mafunzo kama hayo kwenye mikoa ya Shinyanga na Mbeya.

Mbwambo amesema lengo la mradi huo wa miaka miwili ni kushirikisha jinsia zote mbili ili ziweze kumiliki rasilimali zilizopo na kuwainua kiuchumi wanawake katika madini.
 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...