Na Mwandishi Wetu, MOHA, Dodoma.
WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene, ametoa wiki mbili Kituo cha Polisi kihamishiwe katika mji mdogo wa Mtera illi wananchi zaidi ya elfu kumi wanaoishi katika Kata ya Mtera, Wilayani Mpwapwa waweze kupata huduma kwa ukaribu.

Kituo hicho ambacho kipo nje ya mji kwa umbali wa zaidi ya kilomita tano kutoka katika Mji wa Mtera ambapo ipo barabara kuu ya Dodoma kwenda Iringa, wananchi hao wamekuwa wakiteseka kwa miaka mingi kutokana na umbali wa kituo hicho wanapoenda kituoni hapo.

Waziri Simbachawene ambaye alikuwa katika ziara katika Kata hiyo, iliyopo Jimboni kwake Kibakwe, baada ya kupokea malalamiko mbalimbali ya wananchi, alifika katika Kituo hicho kilichopo katika eneo la Mtera ‘Camp’ na kuona umbali huo na pori kubwa lililopo barabarani wakati unapoelekea kituoni hapo, na akaona kuna umuhimu mkubwa wa Kituo hicho kuhamishwa.

Akizungumza na mamia ya wananchi katika Mkutano wa hadhara uliofanyika katika Mji huo wa Mtera, Simbachawene alisema baada ya kwenda kukikagua kituo hicho amekiona kipo porini kama wananchi wanavyosema, hivyo amesema kuna umuhimu mkubwa kituo hicho kuhamishwa.

“Kazi ya Jeshi la Polisi ni kulinda raia na mali zao, kituo kipo porini, na uhalifu mwingi unatokea barabarani, wahamiaji haramu polisi wenyewe wanawakamatia hapa barabarani, wezi, wahalifu, wapiga dili na majambazi wote wanakamatiwa huku wanakoishi watu, kituo kipo mbali kabisa, porini kwasababu kilikuwa ni kambi waliorithi wakati wa ujenzi wa kituo cha Mtera zamani wakawekwa kule, hivyo Polisi wakabaki kule,” alisema Simbachawene.

Aliongeza kuwa; “Lakini hata usalama wao ni hatari sana, kwasababu nguvu ya polisi ni wananchi wake, kwasababu jeshi hili ni la usalama wa raia, polisi wakizidiwa wanawaomba wananchi muwasaidie, hivi wakivamiwa kule watasaidiwa na nani, si mtakuta wamekufa wote, na wenyewe wapo wangapi, watano, sijui sita, kule ni porini, kimsingi busara zote zinataka tufikirie upya, kituo kile kinatakiwa kihame kije huku barabarani, uamuzi wangu ni kwamba kituo kile cha polisi ndani ya siku kumi na nne kiwe kimehamia hapa barabarani.”

Hata hivyo, Waziri Simbachawene baada ya mkutano wa hadhara, alikubaliana na viongozi wa kata hiyo kuyachukua majengo yaliyokuwa Zahanati ya zamani ya Mtera yatumike kwa ajili ya Kituo cha polisi hicho pamoja na nyumba ya Zahanati hiyo ilitumike kwa ajili ya makazi ya Mkuu wa Kituo hicho.

Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Mtera, Robert Maulya alisema kituo cha Polisi Mtera kilijengwa muda mrefu, na kilijengwa kwasababu maalumu na kwasasa kule kumekuwa porini hakuna watu zaidi ya kuwepo kwa kituo hicho pekee, hivyo kinapaswa kuhamishiwa mahali ambapo kuna wananchi kwasababu kwenda kituoni pale ni gharama pia kutokana na umbali.

“Wewe ni Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Polisi wapo chini yako, tunacho kituo cha polisi ambacho kimejengwa muda mrefu, na kule kilijengwa kjwa ajili ya kazi maalumu ya ujenzi wa daraja, lakini leo kule kumekuwa pori na polisi kazi zao ni kulinda raia na mali zao, sasa kule walipo, raia hawapo na mali hazipo, kwahiyo tunaomba kituo hiki kisogee hapa kijijini ili polisi hawa waweze kufanya kazi yao,” alisema Maulya.

Pia Maulya alimshukuru Rais Dkt. John Magufuli kwa kutoa shilingi milioni 700 mwaka jana kwa ajili ya kuanzisha mradi wa maji katika Kata hiyo ambapo mpaka sasa tayari mabomba yamesambazwa kupeleka maji katika nyumba za wananchi.

Aidha, Waziri Simbachawene ametoa milioni kumi kwa ajili ya kusaidia ukarabati wa hosteli ya wanafunzi wa kike wa kidato cha tano na sita katika shule ya sekondari ya Mtera ambayo inatarajiwa kuanza kuchukua wanafunzi hao kuanzia mwakani.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...