Waziri wa Madini Doto Biteko akizungumza na Wanahabari  wakati  akifunga Mkutano wa Saba wa Mawaziri wa Nchi za Afrika Zinazozalisha Madini ya Almasi (ADPA) uliofanyika  kwa Njia ya Video tarehe 8 Aprili, 2021 Jijini Dodoma

   Waziri wa Madini Doto Biteko na baadhi ya Wataalam wa Madini waliohudhuria Mkutano wa Saba wa Mawaziri wa Nchi za Afrika Zinazozalisha Madini ya Almasi (ADPA) kwa Njia ya Video uliofanyika  tarehe 8 Aprili, 2021 Jijini Dodoma

    Picha ya pamoja ya Waziri wa Madini Doto Biteko (Katikati), Naibu Waziri wa Madini Prof. Shukrani Manya (Kushoto) na Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini Prof. Simon Msanjila (kulia) wakati wakifuatilia Mkutano wa Saba wa Mawaziri wa Nchi za Afrika Zinazozalisha Madini ya Almasi (ADPA) uliofanyika  kwa Njia ya Video tarehe 8 Aprili, 2021 Jijini Dodoma

Asteria Muhozya na Steven Nyamiti, Dodoma

Kiswahili kimekubalika kuwa moja ya Lugha ya Mawasiliano zitakazotumika katika Umoja wa nchi Zinazozalisha Madini ya Almasi Afrika na hivyo kuongeza idadi ya lugha zilizokuwa zikitumika awali  katika umoja  huo za  Kiingereza, Kireno na Kifaransa.

 Hayo yamesemwa  Aprili 8, na Waziri wa Madini Doto Biteko wakati akifunga Mkutano wa 7  wa Mawaziri wa nchi zinazozalisha Madini ya Almasi Afrika  ( African Diamond Producers Association- ADPA) uliofanyika kwa njia ya Video Conference na kutanguliwa na Mkutano wa  Wataalam wa jumuiya hiyo ambapo Tanzania ilikuwa mwenyeji wa mkutano huo.

Aidha, Tanzania imekabidhiwa  Uenyekiti wa Jumuiya hiyo nafasi ambayo itadumu nayo kwa kipindi cha miaka 2 ikipokea kutoka kwa nchi ya Jamhuri ya  Namibia ambayo ilikuwa Mwenyekiti kwa muda wa mwaka mmoja. Pia, nchi ya Zimbabwe imekubalika kuwa Makamu Mwenyekiti na inatarajia kuwa mwenyeji wa mkutano  wa 8.

Akieleza kuhusu yaliyojadiliwa na kukubaliwa katika mkutano huo, Waziri Biteko amesema kuwa mkutano huo umekubaliana kuwa Kamati Tendaji ya umoja huo kupitia upya mifumo ya kiutendaji  ya umoja huo ndani ya kipindi cha miezi sita  na kutoa mrejesho.

Aidha, Waziri Biteko ametumia fursa ya Uenyekiti wa jumuiya hiyo  kuzisisitiza nchi wanachama kutumia masoko ya madini yaliyoanzishwa maeneo mbalimbali nchini, akilenga kuzifanya nchi wanachama kuyatumia masoko hayo kufanya biashara ya madini  ili manufaa ya madini hayo yaendelee kubaki Afrika na kwa wanachi wenyewe.

Awali, Waziri Biteko amewaeleza mawaziri walioshiriki mkutano huo kuhusu mafanikio yaliyopatikana katika Sekta ya Madini kufuatia Marekebisho yaliyofanywa kwenye Sheria ya Madini ambayo pamoja na mambo mengine, yalipelekea kuanzishwa kwa masoko ya madini katika mikoa mbalimbali nchini ambapo hadi sasa, Tanzania ina jumla ya Masoko ya Madini 39 na Vituo vya Ununuzi wa Madini 41.

Naye, Waziri wa Madini na Nishati wa Jamhuri ya Namibia, Tom Alweendo wa nchi ambayo imemaliza uenyekiti wake, ameutaka umoja huo kupata viongozi shupavu wa kamati tendaji watakaosaidia kuweka msukumo katika utekelezaji wa malengo ya jumuiya hiyo.

 Ameongeza kuwa, kama wanachama ni lazima  wachochee na kuweka mikakati ya kupigania maslahi ya Afrika kwa madini ya Almasi ikiwemo kuzitaka  nchi hizo  kuhakikisha zinalipa  michango yao kwa mujibu wa sheria.

Pia, Ametumia fursa hiyo kuelezea yale ambayo yalifanywa na nchi hiyo wakati ikishikilia kiti cha Uenyekiti na kueleza kuwa, pamoja na kipindi chake kukabiliwa na changamoto za janga la ugonjwa wa Corona, ilifanikiwa kuunda kamati ya uendeshaji ya jumuiya hiyo.

Mkutano wa 7 wa Mawaziri wa Nchi zinazozalisha madini ya Almasi Afrika, umehudhuriwa na nchi zote 19 wanachama wa umoja huo zikiwemo  Nchi za Angola, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Afrika Kusini, Namibia, Tanzania, Zimbabwe, Cameroon, Afrika ya Kati, Ghana, Togo, Guinea na Sierra Leone. Nchi waangalizi zilizoshiriki ni Algeria, Jamhuri ya Congo, Cote D’ivore, Gabon, Liberia, Mali na Mauritania pia zimeshiriki.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...