Naibu Waziri Ofisi ya Rais  Menejimenti ya Utumishi na Utawala Bora, Deo Ndejembi akizungumza na viongozi wa Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi CCM na Wajumbe wa Kamati ya Maendeleo ya Kata za Manchali na Chilonwa zilizopo jimboni kwake Chamwino, jijini Dodoma.

Charles James, Michuzi TV

ELIMU kwanza! Mbunge wa Jimbo la Chamwino mkoani Dodoma ambaye pia ni Naibu Waziri Ofisi ya Rais  Menejimenti ya Utumishi na Utawala Bora, Deo Ndejembi amesema kipaumbele chake kwa sasa ndani ya Jimbo lake ni elimu na kwamba amepanga kutokomeza zero kwa wanafunzi wanaomaliza kidato cha nne.

Naibu Waziri Ndejembi ametoa kauli hiyo leo alipokua akizungumza na viongozi wa Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi CCM na Wajumbe wa Kamati ya Maendeleo ya Kata za Manchali na Chilonwa zilizopo jimboni kwake Chamwino ambapo amefanikisha upatikanaji wa Sh Milioni 35 na mifuko 150 ya saruji kwa ajili ya sekta ya elimu kwenye Kata hizo mbili.

Akiwa katika kata ya Manchali, Ndejembi amesema tayari kiasi cha Sh Milioni 35 zimeshaingia kwenye akaunti ya Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino kwa ajili ya ujenzi wa jengo la Maabara huku Milioni tano zingine zikiwa zikiwa ni kwa ajili ya ujenzi wa jengo la Hosteli kwa wanafunzi wa shule hiyo.
Katika kata ya Chilonwa, Naibu Waziri Ndejembi amefanikisha upatikanaji wa Sh Milioni 50 za kujenga Zahanati huku pia akichangia mifuko 150 ya saruji kwa ajili ya ujenzi wa Shule ya Sekondari Mapinduzi.

Amesema katika kukuza kiwango cha elimu jimboni hapo amepanga kuanzisha makambi ya elimu kwa shule zote zilizopo jimboni kwake ifikapo mwezi Julai mwaka huu ili kuwaandaa wanafunzi hao kikamilifu kwa ajili ya mitihani yao ya kumaliza kidato cha nne.

" Mimi nitaanzisha makambi ya elimu Julai lengo langu ni kutokomeza zero kwa watoto wetu kwa sababu haziwasaidii, ili tuondoe zero ni kuweka walimu wetu na wanafunzi karibu ili waweze kufundishana, suala la chakula nitagharamia mimi Mbunge wao, ni lazima tuwe na kizazi cha vijana wasomi ambao watakua msaada mkubwa kwa familia zao na Taifa letu kwa ujumla.

Kuwaweka wanafunzi sehemu moja na walimu wao kwa miezi mitatu wananolewa nina uhakika tutaondoa zero kabisa, Dunia ya sasa hivi na Tanzania yetu tunahitaji watu wasomi kwa ajili ya kuwawezesha kuingia kwenye ushindani wa ajira na Biashara kwa ujumla, niwahakikishie nitalibeba hilo Mbunge wenu," Amesema Ndejembi.

Amesema katika kukamilisha mpango huo anaangalia namna nzuri ya kuyaweka makambi hayo kama ni kitarafa au kikanda ambapo wanafunzi wote watakaa sehemu moja huku akiahidi kuwapa walimu motisha.

" Hii ni kwa ajili ya maslahi ya watoto wetu na Jimbo letu, tutatoa motisha kwa walimu maana tutawaomba waongeze muda wa ufundishaji, niwaombe wazazi tuungane pamoja ili kuzalisha akina Mama Samia wengine ambao watatoka katika Jimbo la Chamwino, tuzalisha wakina Ndejembi wengine ambao kesho ndio watakua msaada kwetu," Amesema Naibu Waziri Ndejembi.

Ndejembi amesema katika mwaka wake huu wa kwanza akiwa Mbunge wa Chamwino ni kuhakikisha wanafunzi wanafaulu kwa kiwango kikubwa huku pia akikamilisha miundombinu ya elimu kwa maana ya Madarasa, Hosteli na Maabara ili kurahisisha ufundishaji kwani pia miundombinu bora ya elimu huongeza kiwango cha ufaulu.

Ndejembi pia amewaomba wananchi wa kata hizo mbili na Jimbo la Chamwino kwa ujumla kufanya kazi kwa bidii wakiendelea kumpa ushirikiano Rais Mama Samia Suluhu Hassan kwani ni kiongozi mzuri ambaye uzoefu wake alionao na busara ya uongozi iliyopo ndani yake kwa pamoja itailetea mafanikio makubwa ya kimaendeleo Tanzania.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...