Charles James, Michuzi TV

SERIKALI imewaagiza maafisa elimu kata kuhakikisha wanasimamia fedha na miradi yote ya  elimu katika  shule za msingi na sekondari ili ikamilike kwa wakati na kuleta manufaa kwa jamii na Taifa kwa ujumla.

Hayo yamesemwa leo jijini Dodoma na Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tamisemi, David Silinde wakati akifungua kikao cha maafisa elimu kata nchini(UMEKTA).

“Kuhusu usimamizi wa fedha na miradi ya elimu, kila Afisa Elimu kata asimamie miradi na fedha zote za serikali ndani ya kata yake kwa shule zote za msingi na sekondari.

Baadhi yenu mnazembea kwenye usimamizi na kuisababishia Serikali hasara na kutokuonekana kwa thamani ya fedha kwenye baadhi ya miradi inayotekelezwa katika Kata zetu,” Amesema Silinde.

Silinde amesema  imebainika kuwa baadhi ya walimu wamekuwa na mikopo mingi kupita kiasi hali inayopelekea kukosa utulivu kazini na kusababisha utendaji kazi usioridhishi hivyo kila Afisa Elimu kata ametakiwa kuhakikisha, walimu wanaelimishwa juu ya madhara ya mikopo hiyo.

Amesisitiza maafisa elimu kata wanatakiwa kusimamia  kikamilifu ufundishaji na ujifunzaji wa wanafunzi katika Shule za Msingi na Sekondari kwa kuwa imebainika kuwa baadhi ya Maafisa Elimu kata hawasimamii shule za Sekondari.

“Kila Afisa Elimu Kata afanye tathmini ya maendeleo ya taaluma kwenye kata yake ili kubaini changamoto zinazokwamisha utoaji wa elimu bora ndani ya kata husika na kuzitafutia ufumbuzi kwa kushirikisha jamii na viongozi wa kata husika,” Amesema Naibu Waziri Silinde.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu TAMISEMI Gerald Mweli amesema  Serikali imewawezesha maafisa elimu kata kwa  kuwapa nyenzo ya usafiri pamoja na posho ya kuwasaidia kutekeleza majukumu yao.

Amesema hata hivyo, baadhi wamekuwa hawatimizi majukumu yeo ipasavyo ikiwemo kutokufika kwenye shule kwa muda mrefu.

“Tutakuwa na usimamizi wa karibu kuona kuwa, mnatekeleza majukumu yenu, na pale ambapo itabainika kuwa na udhaifu au uzembe, hatua kali za kisheria na kiutumishi zitachukuliwa dhidi ya wahusika,” Amesema Mweli.

Mweli ameongeza kuwa ili kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia kwenye Shule za Msingi na Sekondari, Serikali kwa kushirikiana na Wadau mbalimbali, Washirika wa Maendeleo na jamii imejenga vyumba vya madarasa kwenye shule za msingi na hivyo kuongezeka kutoka 115,665 mwaka 2015 hadi kufikia 136,292 mwaka 2020.

“Wakati huo huo, idadi ya shule za msingi imeongezeka kutoka 16,899 mwaka 2015 hadi 17,804 mwaka 2020 na shule za Sekondari kutoka 4,708 mwaka 2015 hadi 5,330 mwaka 2020,” Amesema Mweli.

Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tamisemi, David Silinde 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...