Charles James, Michuzi TV

WAZIRI wa Elimu Sayansi na Teknolojia, Prof Joyce Ndalichako amezionya Halmashauri zote nchini ambazo zimekua na tabia ya kufanya udanganyifu kwenye uandikishwaji wa wanafunzi ambao wanamaliza Darasa la Saba.

Prof Ndalichako ametoa kauli hiyo leo jijini Dodoma alipokua akizindua mkutano wa Baraza la Wafanyakazi la Wizara hiyo ambapo amewataka watumishi wote wa Wizara kuzingatia weledi na kuacha kutumia lugha za ubabe wanapowahudumia wateja wao.

Akizungumzia suala la udanganyifu wa wanafunzi wanaoandikishwa kwa ajili ya mitihai ya kumaliza Darasa la Saba, Prof Ndalichako amesema amepata taarifa ya halmashauri ambazo zimeondoa majina ya wanafunzi wanaotakiwa kufanya mitihani hiyo kwa kuepuka kwamba watafeli na kuziletea sifa mbaya halmashauri hizo.

Ametoa onyo kwa maafisa elimu wa halmashauri hizo na walimu wakuu kwenye shule ambazo zimeondoa majina ya wanafunzi hao kuacha mara moja na wale watakaokaidi hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.

" Nimepata taarifa kutoka kwa raia mwema kuhusu hii tabia kwenye Halmashauri nchini ambapo kwa makusudi kabisa maafisa elimu na walimu wakuu wanaondoa majina ya wanafunzi wenye uwezo mdogo kwa kuepuka kwamba watafeli na halmashauri zao kuonekana zinafanya vibaya, wanachokifanya wanawarudisha hao wanafunzi darasa la sita.

Nitoe onyo kwa maafisa elimu wote kuacha mara moja tabia hiyo na wale wote waliofanya udanganyifu huo majina yao ntayapeleka Tamisemi ili wachukuliwe hatua maana Tamisemi ndio wanahusika nao," Amesema Prof Ndalichako.

Amesema serikali imeamua kuwekeza kwenye elimu kwa kutoa elimu bila malipo hivyo kitendo cha kuwaondoa wanafunzi hao ni kuchongesha serikali na wananchi kwani hao wanafunzi wanaorudishwa nyuma bila mpango wa serikali wanakua hawapo kwenye hesabu ya elimu bila malipo.

" Unajua serikali tunatenga fedha nyingi kwenye Sera hii ya elimu bila malipo, hawa maafisa elimu na walimu wakuu wanavyowarudisha nyuma hawa wanafunzi wakati serikali ishatenga bajeti yao inaajua wanamaliza matokeo yake mwaka unaofuata idadi ya wanafunzi inaongezeka nje ya kiasi kilichopangwa," Amesema Prof Ndalichako.

Waziri Ndalichako amewatoa hofu pia watumishi wote wenye sifa za kupandishwa madaraja kuwa watapandishwa kwani tayari Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dk Leonard Akwilapo ameshapeleka taarifa zao Ofisi ya Rais Utumishi.

" Niwaombe mfanye kazi kwa bidii ili kuipa sifa zaidi wizara yetu, Rais Mama Samia ameendelea kutuamini ndio maana mnaona timu yote Mimi, Katibu Mkuu na Naibu Katibu Mkuu wote tumerudishwa hajatubadilisha, hiyo maana yake anatuamini sana, twendeni tukafanye kazi kwa weledi kwa kufuata taratibu na sheria zetu na watakaofanya vizuri basi tunawapandisha madaraja maana inakua ni haki yao, mtu akifanya vizuri lazima apewe haki yake.

Nisisitize tena nidhamu makazini hasa kuwa waungwana na wastaarabu kwa wananchi wetu, haiwezekani mtu amefunga safari amefuata huduma toka asubuhi hadi jioni yupo tu na bado unamwambia arudi kesho, huu siyo uungwana ni kuwagombanisha wananchi na serikali yao, tabia hii sitaki kuiona nachotaka ni utii, ufanisi na utendaji kazi uliotukuka," Amesema Prof Ndalichako.

WAZIRI wa Elimu Sayansi na Teknolojia, Prof Joyce Ndalichako

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...