Watendaji wa Sekta za serikali, wametakiwa kuwajibika ipasavyo, hasa katika kusimamia makusanyo ya fedha katika maeneo yao, kwa lengo la kuzidisha uharaka katika kutengeneza miradi ya maendeleo.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla, ametoa kauli hiyo alipokutana na Uongozi wa Shirikia la Bandari la Zanzibar, Ofisini kwake Vuga, ikiwa ni katika utaratibu alioupanga kuonana na viongozi wa taasisi mbali mbali za Serikali.

Mheshimiwa Hemed alisema kwamba, ni wajibu kwa watumishi kuhakikisha mapato yanaongezeka, ili serikali iweze kuongeza kasi ya kuleta maendeleo kwa maslahi ya wananchi.

Alieleza kuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mheshimiwa Dr Hussein Ali Mwinyi, wakati akiomba ridhaa ya wazanzibar aliweza kuonana na makundi mbali mbali, na kuahidi mengi, hivyo ni vyema kwa watendaji kuongeza kasi Zaidi kwa vile wao ndio watekelezaji wa aliyoyahidi Rais Mwinyi.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliendelea kuwasihi viongozi hao kuendelea kutatua changamoto mbali mbali zinazowakabili katika maeneo yao ya kazi, na zile wasizoziweza ni vyema wakaziwasilisha katika mamlaka ya juu, ili kuzifikisha sehemu husika.

Aliwasihi kuwa Bandari ni eneo linalotoa huduma kwa jamii, hivyo ni vyema watendaji wake kuwa na utayari na ufanisi katika majukumu yao, ili lengo na azma ya Serikali ya Awamu ya Nane iweze kufikiwa.

Mh. Hemed amefurahishwa na mafanikio yanayoaendelea kupatikana katika shirika la Bandari, na kueleza kwamba Serikali haitegemei kuona mabaya yoyote yanaweza kujitokeza katika eneo hilo, kwa kuwa wameweza kuonesha uwezo mzuri wa kazi zao.

Mheshimiwa Hemed aliwanasihi watendaji hao kuzidisha juhudi zaidi ya kazi zao, kwani jamii ina uhitaji mkubwa wa eneo hilo, hivyo wasisite kuomba ushauri kwa Serikali kwa lengo la kukuza ufanisi wao.

Kwa upande wake Waziri wa Miundombinu, Mawasiliano na usafirishaji Mheshimiwa Rahma Kassim Ali amesema, Wizara kwa kushirikiana na Shirika hilo wamejitahidi kutatua changamoto zinazowakabili, na nyingi wanazitatua kwa hatua ya awali, ingawa zipo changamoto zinazowapa vikwazo na watazifikisha sehemu husika, kwa ajili ya maelekezo zaidi.

Kwa upande wake mkurugenzi wa Shirika la Bandari Zanzibar Nd. Nahaat Mohamed Mahfoudh amemueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba, Shirika limepata mafanikio makubwa kwa muda mchache, akitolea mfano makusanyo ya mwezi Machi yaliyofikia Shilingi za Kitanzania Bilioni 3.6 na faida Shilingi 2.2 Bilioni.

Ndugu Nahaat alisema uingiaji wa meli katika Bandari hiyo, kwa sasa unachukuwa siku Tatu hadi Nne ambapo awali ilikuwa ikichukua siku 14.

Aidha alieleza kwamba licha ya changamoto ya janga la corona duniani, pamoja na mfumko wa bei, bado shirika linaendelea kuzidisha mapato.

Wakati huo huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla, amekutana na Uongozi wa Mamlaka ya Uwekezaji Vitega Uchumi Zanzibar (ZIPA) Ofisini kwake Vuga,na amewasihi watendaji hao kuwajibika katika majukumu yao, wakizingatia kuwa taasisi hiyo ni muhimu kwa kukuza uchumi wa Nchi.

Nae Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Kazi, Uchumi na Uwekezaji Mheshimiwa Mudrik Ramadhan Soraga, amesema Mamlaka hiyo ni kitovu cha uwekezaji Nchini, na kueleza kuwa moja ya jukumu lao ni kuwatambua wawekezaji wote wanaowekeza nchini.

Mheshimiwa Soraga amemueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba, miongoni mwa mafanikio yaliyofikiwa ni pamoja na kuanzishwa kwa Kituo Jumuishi {One Stop Center} kinachomrahisishia muwekezaji kupata cheti cha kumtambua ndani ya siku saba.

Waziri Soraga awasihi wazaliwa kutumia fursa ya uwekezaji nchini kwao na kuondoa dhana ya uwekezaji kuwahusu wageni kutoka nje ya Tanzania.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...