Na Teresia Mhagama, Dodoma

Timu ya Serikali ya Majadiliano ya Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki imekamilisha majadiliano ya mradi huo na kukabidhi Taarifa kwa Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani ikiwa ni ishara ya kuendelea na hatua zaidi ya utekelezaji wa mradi husika.

Taarifa hiyo ilikabidhiwa tarehe 19 Aprili, 2021 na Katibu wa Timu hiyo ambaye ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Leonard Masanja ambapo viongozi mbalimbali wa Wizara na Taasisi walihudhuria wakiwemo Naibu Waziri wa Nishati, Wakili Stephen Byabato, Naibu Katibu Mkuu, Kheri Mahimbali, Kamishna wa Petroli na Gesi, Adam Zuberi na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania,(TPDC), Dkt.James Mataragio.

Akizungumza mara baada ya kukabidhiwa Taarifa hiyo, Waziri wa Nishati, alieleza kuwa, majadiliano ya mradi huo yamefanyika kwa takribani miaka mitatu kutokana na ukubwa wa kazi husika na kukamilika kwake kunafungua ukurasa mpya wa kuanza kufanya kazi.

Alisema kuwa, taarifa hiyo inajumuisha masuala mbalimbali ambayo yatapelekea nchi kufaidika na mradi huo ikiwemo masula ya  kikodi, tozo za Serikali, ushiriki wa watanzania katika mradi, fidia, mikataba, bima na masuala ya ardhi.

Pamoja na kuipongeza Timu hiyo ya Majadiliano, Dkt.Kalemani alieleza kuwa jumla ya shilingi bilioni 28.8 zitalipwa kwa watanzania ambao watapisha mradi huo baada ya tathmini kukamilika hivyo ametoa wito kwa wananchi kupisha maeneo ya mradi mara watakapolipwa fidia ili mradi husika utekelezwe kama ilivyopangwa.

Aliongeza kuwa, katika mradi huo yatajengwa makambi 16 pamoja na eneo la kulainisha na kuunganisha vyuma vitakavyotumika kwenye ujenzi ambapo wananchi wataopisha maeneo hayo pia watalipwa fidia.

Dkt.Kalemani alisema kuwa, katika Bandari ya Tanga, kutajengwa matenki makubwa Matano ambapo mafuta yatakuwa yanashushwa na kazi inayofuata ni kutwaa eneo na kuanza ujenzi baada ya fidia kukamilika.

Kuhusu suala la ajira, Dkt.Kalemani alisema kuwa, jumla ya watanzania 10,000 hadi 15,000 wataajiriwa wakati wa ujenzi wa bomba hilo, na Serikali itahakikisha kuwa watanzania wanaajiriwa kwa zaidi ya asilimia 80 na katika taaluma ambazo watanzania hawana ndipo wataajiriwa watu wa nje ya nchi.

Vilevile alisisitiza watanzania kujiandaa na fursa zitakazotokana na mradi huo ikiwemo utoaji wa huduma mbalimbali kama ulinzi, vifaa vya ujenzi, chakula na usafiri kwa kuwa hatua za ujenzi zitaanza wakati wowote kuanzia sasa.

Alieleza kuwa, Timu maalum itaundwa kwa ajili ya kusimamia mradi huo ambao utajengwa kwa muda wa miaka mitatu na utapita katika mikoa Nane, Wilaya 24 na vijiji zaidi ya 124 hivyo ni watanzania wengi wataguswa na mradi huo na hivyo kufaidika nao.

Aidha, alisema Serikali itafaidika na masuala mbalimbali kutokana mradi huo kwani Bomba hilo la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki litapitisha takriban mapipa 216,000 ya mafuta kwa siku ambapo kila pipa litalipiwa Dola za Marekani 12.77.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Leonard Masanja ambaye pia ni Katibu wa Timu ya Serikali ya Majadiliano ya Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki, (kushoto) akikabidhi taarifa ya majadiliano ya mradi huo kwa Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (kulia).Kulia ni Naibu Waziri wa Nishati, Wakili Stephen Byabato.

Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (katikati) akizungumza mara baada ya kukabidhiwa taarifa ya majadiliano ya mradi wa Bomba la Afrika Mashariki. Kulia kwake ni Naibu Waziri wa Nishati, Wakili Stephen Byabato na kushoto ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Leonard Masanja ambaye pia ni Katibu wa Timu ya Serikali ya Majadiliano ya Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki.

 

Watendaji mbalimbali kutoka Wizara ya Nishati pamoja na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), wakiwa katika mkutano na Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani ambao ulihusu makabidhiano ya taarifa ya mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Kheri Mahimbali (kushoto) na Kamishna wa Gesi na Petroli, Adam Zuberi wakiwa katika mkutano na Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani ambao ulihusu makabidhiano ya taarifa ya mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki.

 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...