Charles James, Michuzi TV

NI zaidi ya Kimbunga Jobo! Ndivyo unavyoweza kuelezea baada ya Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Dodoma, Mariam Ditopile kuzoa wanachama 38 wa vyama vya upinzani kutoka Chadema, ACT Wazalendo, NCCR-Mageuzi na ADA Tadea leo katika kata ya Buhigwe iliyopo wilayani Buhigwe Kigoma.

Wanachama hao wamerudisha kadi zao hizo wakieleza kutoridhishwa na uongozi wao wakuu akiwemo Freeman Mbowe wa Chadema na Zito Kabwe wa ACT Wazalendo.

Mbunge Ditopile amefanikiwa kuwarudisha wapinzani hao CCM na kupokea kadi zao alipokutana na wananchi na vijana wa Bodaboda katika kituo chao maarufu cha Buhigwe alipofika kumuombea kura mgombea Ubunge wa Jimbo la Buhigwe CCM, Kavejuru Felix.

Akizungumza na wananchi hao, Ditopile amesema Serikali inayoongozwa na CCM imefanikiwa kufanya maendeleo makubwa kwenye Mkoa wa Kigoma na hata Wilaya ya Buhigwe na bado kazi ya kuwaletea maendeleo inazidi kufanyika huku akiwatolea mfano ujenzi wa miundombinu ya barabara unaofanywa na serikali pamoja na uletwaji wa nishati ya umeme ambao kabla haukuepo.

“ Hii ni historia hapa Buhigwe na kitendo cha wanachama 38 wa upinzani tena wakiongozwa na Bodaboda kurejea CCM leo inaonesha dhahiri namna ambavyo Chama chetu kinakubalika kwa wananchi, tuwaahidi tu kwamba tutaendelea kuitunza imani yenu hii kwetu.

Salamu zimewafikia hao wanaopita kudanganya wananchi kwamba wanakubalika, mmewaonesha kwamba Wananchi wa Buhigwe siyo wajinga na wala hawadanganyiki na siasa uchwara za yule Mbunge wa upinzani tuliyemstaafisha pale Kigoma Mjini, mmempa heshima Rais Samia na Makamu wa Rais Dk Mpango ambaye ni mtoto wa nyumbani,” Amesema Ditopile.

Awali kabla ya kuwapokea wanachama hao, Mbunge Ditopile alisikiliza changamoto zao ikiwemo ya jezi za mpira ambapo amewaahidi kuwaletea seti mbili za jezi pamoja na mipira mitatu ili waweze kushiriki mashindano mbalimbali bila changamoto za vifaa.

Aidha Ditopile aliambatana na Mkuu wa Upelelezi wa Wilaya SP Deogratius Challe ambaye alijibu changamoto ya bodaboda kukamatwa kiholela ambapo alimuahidi Mbunge Ditopile na wananchi hao kuwa watashughulikia changamoto hizo ili zisijitokeze tena.

“ Changamoto yenu ya jezi nimeipokea hilo liko chini ya uwezo wangu ninaahidi nitawaletea lengo likiwa kukuza michezo na wananchi pia kufanya mazoezi kama sehemu ya kujiweka fiti kiafya,” Amesema Ditopile.

Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Dodoma, Mariam Ditopile akiwa ameshika kadi za vyama mbalimbali vya upinzani zilizorudishwa na wanachama wa vyama hivyo mbele yake leo wilayani Buhigwe Kigoma. Wanachama hao wameomba kurudi CCM.
Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Dodoma, Mariam Ditopile akipokea kadi za wanachama wa upinzani walioomba kurejea CCM leo.
Vijana wa Bodaboda wakimsikiliza Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Dodoma, Mariam Ditopile. Mbunge huyo amekutana na vijana hao katika Kata ya Buhigwe wilayani Buhigwe Kigoma.
Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Dodoma, Mariam Ditopile akiwa na Mkuu wa Upelelezi wa Wilaya ya Buhigwe, SP Deogratius Challe walipokutana na vijana wa Bodaboda wa kata ya Buhigwe kusikiliza na kutatua changamoto zao.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...