Waziri wa Kilimo Mhe Prof Adolf Mkenda akisisitiza jambo wakati akizungumza na waandishi wa habari Ofisini kwake Jijini Dodoma tarehe 13 Mei 2021.

Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Dodoma


Hadi kufikia tarehe 04 Machi, 2021 Serikali imefanikiwa kudhibiti makundi yote ya nzige wa jangwa yaliyoingia nchini na uchunguzi umeendelea kufanyika hadi tarehe 13 Aprili, 2021 ambapo haujabaini uwepo wa nzige au tunutu walianguliwa na hakuna uharibifu uliofanywa na nzige hao kwenye mazao ya kilimo.

Katika taarifa ya Waziri wa Kilimo Mhe Prof Adolf Mkenda wakati akizungumza na waandishi wa habari Ofisini kwake Jijini Dodoma tarehe 13 Mei 2021 amebainisha kuwa Kati ya tarehe 14 Januari, 2021 na 24 Februari, 2020 Tanzania ilipata uvamizi wa Nzige wa Jangwa waliotokea nchi jirani ya Kenya na kuingia katika Wilaya nane (8) za Mwanga, Siha na Moshi (Kilimanjaro), Simanjiro (Manyara); Longido, Monduli na Ngorongoro (Arusha); na Lushoto (Tanga).

Waziri Mkenda amesema kuwa kati ya Wiaya hizo, nzige walikuwa wakihama kutoka kwenye maeneo waliokuingia na kulala maeneo mbalimbali ya Wilaya nne (4) Siha (Kilimanjaro), Simanjiro (Manyara); Longido na Monduli (Arusha) wakitanda kwenye eneo la jumla ya hekta 6,441

Kuhusu Nzige Wekundu, Waziri Mkenda amesema kuwa wapo katika mazalio ya asili ya yaliyopo katika Bonde la Mto Malagarasi (Wilaya ya Kigoma na Kaliua), Mbuga za IKuu/Katavi (Wilaya ya Mpanda), Mbuga za Wembere (Wilaya ya Igunga) na Mbuga za Ziwa Rukwa (Wilaya ya Sumbawanga). Aidha, kuna Mazalio madogo (auxiliary breeding area) yaliyoko kwenye Mbuga ya Bahi (Wilaya ya Bahi) ambapo Wizara ya Kilimo kila mwaka hufanya tathmini ya Nzige Wekundu kwenye mazalio kwa kuangalia uwepo wao na kuwadhibit endapo wameongezeka.

Katika msimu wa mwaka 2020/2021 wataalamu wa Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na Shirika la Kudhibiti Nzige Wekundu la Kati na Kusini mwa Afrika (International Red Locust Control Organization for Central and Southern Africa – IRLCO-CSA) wamefanya uchunguzi katika maeneo yote ya mazalio ya nzige wekundu kuanzia tarehe 15 Februari, 2021 hadi 29 Aprili, 2021 na kubaini kuwa hakuna tishio la uwepo wa nzige hao.

Kama ilivyo kwenye udhibiti wa nzige, Wizara ya Kilimo imeweka kipaumbele katika udhibiti wa visumbufu hivyo vywa kwelea kwelea kwa kuwa wanaweza kusababisha upotevu wa mazao endapo hawadhibitiwa mapema.  

Kuhusu udhibiti wa kwelea kwelea, Prof Mkenda amesema kuwa kazi hiyo ilianza tarehe 17 Novemba, 2020 na imeendelea hadi sasa katika Wilaya 22 kwenye mikoa 12 ya Kilimanjaro (Mwanga, Moshi), Arusha (Wilaya ya Meru), Manyara (Simanjiro na Babati), Dodoma (Chamwino, Bahi, Kondoa, Dodoma Jiji), Singida (Singida Vijijini, Itigi, Mkalama), Morogoro (Kilosa na Mvomero), Iringa (Iringa Vijijini), Mbeya (Mbarali), Geita (Geita Vijijini), Mwanza (Sengerema na Kwimba) na Shinyanga (Kishapu na Shinyanga Vijijini) na Pwani (Chalinze).

Ameeleza kuwa kudhibiti kwelea hao katika maeneo mapya yaliyoripotiwa katika Mkoa wa Tabora na Simiyu na maeneo ambako wameshadhibiti lakini makundi mapya ya kwelea yameanza kujitokeza kutokana na kuanguliwa kwa makinda hususani katika Wilaya ya Mbarali (Mbeya), Babati (Manyara), Kishapu (Shinyanga).

Kiwavijeshi vamizi (Fall Armyworm- FAW) ni kisumbufu kigeni ambacho kimeendelea kuripotiwa katika nchi mbalimbali duniani. Nchini Tanzania kisumbufu hiki kilionekana kwa mara ya kwanza mwezi Machi, 2017 kikishambulia mazao ya mahindi katika Wilaya ya Nkasi Mkoani Rukwa. Kisumbufu hiki ni tishio kwa usalama wa chakula, lishe na uchumi wa nchi kutokana na uwezo wake wa kushambulia hadi aina 80 ya mazao yakiwemo mahindi, mtama, uwele, mpunga, shairi, ngano, miwa na kuleta uharibifu wa mazao hadi kufikia asilimia 100 kama hatadhibitiwa mapema na kikamilifu.

Mbele ya Waandishi wa habari Mhe Prof Mkenda amesema kuwa Wizara imesambaza mitego ya kunasa nondo wa kiwavijeshi vamizi 289 katika mikoa ya Rukwa (24); Songwe (30); Mbeya (18); Shinyanga (09); Arusha (11); Mwanza (10); Manyara (07); Kilimanjaro (07); Kagera (09); Katavi (13); Mara (10); Simiyu (12); Geita (08); Morogoro (09); Njombe (07); Iringa (26); Ruvuma (20), Tanga (07), Pwani (06), Tabora (09), Lindi (07), Mtwara (07), Dodoma (06), Singida (07) na Kigoma (10). Vile vile Wizara imesambaza lita 9,900 za kiuatilifu aina ya Duduma katika Wilaya za Hai (Lita 2,500), Mbogwe (Lita 2,000), Dodoma Jiji (Lita 1,000), Iramba (lita 1,000), Kilindi (Lita 2,000), Mkoa wa Mara Lita 300, Simanjiro Lita 500, Bahi (Lta 100), Morogoro lita 500.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...