Na Mwandishi wetu, Mirerani


WADAU wa madini ya Tanzanite wa Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, wamewapongeza wabunge kwa kukemea kitendo cha upekuzi wa kuvuliwa nguo unavyofanyika kwenye lango la ukuta unaozunguka migodi ya madini hayo.

Mkazi wa Mirerani Obeid Sarakikya amesema wabunge wamewatetea wananchi ipasavyo kwani siyo vizuri na pia ni uvunjifu wa haki za binadamu kuwavua nguo watu wakati wa kuwapekua.

Sarakikya amesema alimsikia mbunge wa jimbo la Simanjiro Christopher Ole Sendeka akipiga kelele dhidi ya upekuzi huo kwani ni udhalilishaji mkubwa usio na chembe ya utu wa kibinadamu.

"Mbunge wa vijana Taifa Asia Halamga na Joseph Musukuma nao wamelia na wadau wa madini juu ya upekuzi wa kuvuliwa nguo kwa wadau wa madini ya Tanzanite, tunawashukuru sana," amesema.

Katibu wa chama cha wachimbaji madini mkoani Manyara (Marema) Tawi la Mirerani Rachel Njau amesema anamuomba Waziri Mkuu Kassim Majaliwa atimize ahadi aliyoitoa Bungeni kuwa watanunua mashine ya upekuzi kuliko kuwavua nguo na kuwadhalilisha watu.

Njau amesema kauli ya Waziri wa ulinzi Elias Kwandikwa inapaswa kukanushwa kwani watu wanavuliwa nguo siku zote na siyo wakihisiwa wakiwa na madini kama alivyosema Bungeni.

"Mbunge wa viti maalum wa Mkoa wa Arusha Catherine Magige alielezea vizuri juu ya udhalilishaji unaofanyika Mirerani unasababisha wananchi wengine kutopanda mlimani kwa hofu ya kuvuliwa nguo, tunawapongeza wabunge wetu kwa kutetea," amesema Njau.

Mdau mwingine Mashaka Jororo amesema wananchi wanaichukia Serikali yao kwa vitendo vya udhalilishaji unaofanyika Mirerani hivyo wanunue vifaa vya upekuzi na siyo kuwavua nguo.

Jororo amesema kitendo cha kuwavua nguo wananchi kinapaswa kupigwa vita hivyo anawapongeza wabunge kwa kuwatetea Bungeni.

Mdau mwingine Sokota Mbuya amesema wabunge wameonyesha kuwa wanajali maslahi ya wananchi wao kwa kukemea kitendo cha askari kuwavua nguo wakati wa upekuzi.

"Tunawapongeza wabunge wote akiwemo Ole Sendeka, Musukuma, Asia na Magige ambao kwa namna moja au nyingine wamekemea vikali kitendo hicho," amesema.

Waziri wa Madini Dotto Biteko akizungumza na wachimbaji madini ya Tanzanite wa Mji mdogo wa Mirerani, Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, alipotembelea eneo hilo hivi karibuni.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...