Na Mathew Kwembe, Mtwara
TIMU ya soka ya wasichana ya mkoa wa Mwanza imeyaanza mashindano ya mwaka huu ya UMISSETA kwa kutoa onyo kwa timu nyingine zinazoshiriki michezo hiyo baada ya kuifunga timu ya mkoa wa Kagera magoli 3-0.

Magoli ya Mwanza yalifungwa na Aaliyah Fikiri magoli mawili na Hadija Petro goli moja.

Nyota wa mchezo huo alikuwa ni kiungo mshambuliaji wa Mwanza Sharifa Hamidu ambaye ndiye alikuwa akisababisha mashambulizi dhidi ya Kagera na mara kwa mara kutibua mipango yao.

Akizungumza mara baada ya mchezo huo Kocha wa Mwanza Mwalimu Michael Otieno amesema mchezo wa leo ulikuwa mgumu kwa timu yake mwanzoni baada ya Kagera kucheza pasi fupifupi lakini baada ya vijana wake kuanza kucheza pasi ndefu ndefu waliweza kuwamudu Kagera.

Mwalimu Otieno ambaye anafundisha shule ya sekondari ya Alliance ya jijini Mwanza amesema amejigamba kulibeba tena kombe hilo kwani anajivunia kuwa na kikosi kilichojaa wachezaji mahiri ambapo wanafunzi 9 wanaounda kikosi hicho wanatoka katika shule hiyo ya mpira.

Matokeo ya michezo mingine iliyochezwa leo kwa soka wasichana, timu za Rukwa na Mbeya zilitoka suluhu ya bila kufungana, Tabora imeifunga Mara 2-1, Mtwara na Kilimanjaro 0-0, Arusha na Manyara 0-0, Iringa imeibugiza Songwe 5-1, Dar es salaam imeichapa Katavi 3-0, Singida na Simiyu 1-1 na Ruvuma dhidi Lindi 0-1.

Matokeo ya mpira wa wavu wavulana Unguja dhidi ya Pwani 3-0, Njombe dhidi ya Ruvuma 3-0, Songwe imefungwa na Shinyanga seti 0-3 na kwa wasichana mpira wa wavu Morogoro imefungwa na Mbeya seti 0-3.

Mpira wa mikono wasichana Unguja dhidi ya Tanga 10-13, Mwana dhidi ya Iringa 17-8, na Morogoro dhidi ya Geita 14-9, Mara dhidi ya Njombe 22-4 na kwa upande wa mpira wa mikono wavulana Dar es salaam dhidi ya Simiyu 26-12, Tabora dhidi ya Manyara 24-7, na Pwani dhidi ya Kigoma 22-20.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...