Wafanyakazi wa BRAC Tanzania Serengeti wakiwa katika picha ya pamoja.
Katibu Tawala Wilaya ya Serengeti Cosmas Qamara akizungumza na wananchi wa wilaya hiyo wakati wa uzinduzi wa tawi la Shirika la BRAC Tanzania lililozinduliwa Wilayani humo.



SHIRIKA la BRAC limezindua rasmi tawi lake katika wilaya ya Serengeti, ikiendelea na dhamira yake ya kurahisisha upatikanaji wa huduma za kifedha nchini Tanzania. 

Tawi hilo lililopo katika mji wa Mugumu lilizinduliwa rasmi na Katibu Tawala wa Wilaya ya Serengeti Cosmas Qamara na kuwapongeza shirika la BRAC linalotanua wigo katika kutoa huduma jumuishi za kifedha kwa njia ambayo ni rahisi, kupitia bidhaa zilizoundwa kukidhi mahitaji ya wateja wake. 

Qamara akizungumza katika tukio hilo lililohudhuriwa na Watendaji wa Serikali za Mitaa ya mji wa Mugumu, pamoja na viongozi wa vikundi vya mikopo ya akina mama alitoa pongezi zake kwa shirika kwa kuifikia wilaya ya Serengeti kwa huduma za mikopo na hivyo kurahisisha upatikanaji wa fedha kwa wakinamama wanaojishughulisha na shughuli mbali mbali mbali za uchumi. 

"Nawapongeza BRAC kwa hatua hii na ninafarijika kuona nia yenu ya kuwanyanyua wanawake kiuchumi. Napenda kuwashauri wakinamama wanaopata fursa hii waitumie vizuri kwa kutumia mikopo kwa shughuli husika na kurejesha mikopo yako kwa uaminifu ili na wengine waweze kupata,"

"Vile vile ningependa kushauri shirika lifikirie kuleta mikopo ya wakulima ili na wakina baba nao wapate fursa ya kuendeleza shughuli zao za kilimo. Serengeti ni wilaya yenye shughuli nyingi za kilimo na wakulima hawa pia wanahitaji huduma za kifedha,” aliongeza Katibu Tawala huyo.

Kwa upande wake, Meneja wa Mkoa wa BRAC Tanzania Finance Ltd Eunice David alisema kuwa BRAC imejipanga kusaidia shughuli za kiuchumi za wakazi wa wilaya ya Serengeti kupitia mikopo midogo midogo yenye masharti nafuu hususani kwa wanawake ambao ndio lengo kuu la shirika hilo. 

"Wanawake ndio uti wa mgongo wa taifa letu na hivyo tumejikita katika kuwawezesha wanawake waweze kujikomboa kiuchumi. Huduma ya mikopo ya vikundi isiyokuwa na dhamana ndio bidhaa yetu kuu na imeundwa mahsusi kwa wanawake wajasiriamali na wakulima kwa sababu tunaelewa changamoto za wanawake katika kupata huduma za kifedha. Ni matumaini yetu kuwa kupitia mikopo hii wanawake wa wilaya ya Serengeti wataweza kuwekeza katika shughuli zao za kiuchumi na hivyo kutimiza malengo yao kijamii na kiuchumi."  

Mkoani Mara BRAC ilianza operesheni mwaka 2008 katika mji wa Musoma ambako kuna matawi mawili, matawi mengine yapo katika wilaya za Tarime, Bunda na kuongezeka kwa tawi jipya la wilaya ya Serengeti, kutakuwa na jumla ya matawi matano katika mkoa huu uliopo katika kanda ya ziwa. 

Amesema BRAC inajivunia kuwa na matawi 155 ambayo yapo katika wilaya 83 kati ya mikoa 23 kati ya 26 ya Tanzania Bara na Zanzibar na inajivunia kuwa mshirika mkubwa kwa wanawake kwani asilimia 97 ya wateja wake nchini ni wanawake wanaojishughulisha na biashara ndogo ndogo, wakulima na wafugaji. 

"Pamoja na mkopo usio na dhamana kupitia vikundi vya kinamama, BRAC pia hutoa huduma za mikopo binafsi kwa wajasiriamali wa kati ulio wa dhamana kwa wateja wanawake na wanaume.Dhamira ya BRAC ni kutoa huduma mbalimbali za kifedha kwa watu wanaoishi katika mazingira magumu kiuchumi, hasa wanawake wanaoishi vijijini na maeneo ambayo upatikanaji wa huduma za kifedha ni mgumu,"

Ameongeza kuwa, Lengo kuu ni kuweza kuwapatia fursa za kujiajiri, kujenga nidhamu ya matumizi ya kifedha, na kuendeleza ndoto zao za ujasiriamali.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...