Charles James, Michuzi TV

AMEONESHA uwezo! Ni kauli ya Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Dodoma, Mariam Ditopile akizungumzia siku 100 za Rais Samia Suluhu Hassan akimtaja kama Rais mchapakazi, hodari, jasiri,mwenye busara na mlezi kwa viongozi walio chini yake.

Akizungumza na mwandishi wetu jijini Dodoma, Ditopile amesema kwa kipindi cha miezi mitatu ya uongozi wake mpaka Sasa Rais Samia ameonesha kuwa ni kiongozi shupavu, mwenye msimamo na uwezo wa kuiletea Tanzania maendeleo makubwa.

Amesema kupitia bajeti ya Serikali ya mwaka wa Fedha 2021/22 imeonesha jinsi gani Uongozi wa Rais Samia umejipanga kuacha alama katika kuwatumikia watanzania.

Ditopile ameongeza kuwa uso wa Rais Samia unaonesha ni jinsi gani alivyo na upendo asiye mbaguzi ambapo amesema hayo ameyadhihirisha wazi mara kadhaa ambapo amekua akisema wapo watanzania wenye uwezo kwenye vyama vingine tofauti na CCM ambao atawateua.

Katika kulidhihirisha hilo, Ditopile amesema ndio maana Rais Samia alimteua aliyekua Mgombea Urais mwaka 2020 kupitia Chama Cha ADC, Queen Sendiga kuwa Mkuu wa Mkoa wa Iringa.

" Rais Samia ndani ya siku zake 100 ofisini tayari tumemuona rangi yake, hana ubaguzi na wala siyo Rais anaeangalia vyama, ndio maana pia aliwakaribisha wapinzania na hata tuliona Chadema wakikiri kuwa barua yao ya kuomba kuonana na Rais imekubaliwa na wanasubiri kupangiwa tarehe," Amesema Ditopile.

Akizungumzia Ujasiri na Ushupavu wa Rais Samia, Mbunge Ditopile amesema hilo lilijionesha siku tatu tu baada ya kuapishwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kauli yake aliyoitoa Machi 22 katika Uwanja wa Jamhuri wakati wa shughuli ya kuaga mwili wa aliyekua Rais Dk John Magufuli.

" Wote ni mashuhuda ile siku Dk Magufuli anaagwa pale Jamhuri Dodoma, Rais Samia alitoa kauli ya kishupavu sana ambapo alisema, "Niwaambieni anayeongea hapa ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye Jinsia yake ni Mwanamke" 

Kauli hiyo pekee ilitosha kuonesha kwamba Rais Samia anajiamini, siyo mtu wa kuyumbishwa, lakini pia ukiacha kauli hiyo tumeona namna ambavyo amekua mkali kwa Watendaji wabadhirifu na wasioenda na kasi yake," Amesema Ditopile.

 Ditopile amesema kupitia pia Bajeti ya Serikali ya mwaka wa Fedha 2021/22 Rais Samia ameonesha jinsi gani anajali maslahi ya wafanyakazi wa umma na binafsi nchini ambapo ameboresha maslahi yao.

" Tumeona katika bajeti hii ambayo ndio bajeti yake ya kwanza akiwa na miezi mitatu tu Mama yetu amepunguza kiwango cha chini cha kutoza kodi ya mapato ya ajira (PAYE) kutoka asilimia tisa hadi nane, hii inaonesha jinsi gani Serikali ina mpango wa kupunguza mzigo wa kodi kwa wafanyakazi, kiwango hicho kimepunguzwa kutoka asilimia 11 mwaka 2015/16 hadi asilimia nane.

Kubwa zaidi amefuta tozo ya asilimia sita iliyokua ikitozwa la ajili ya kulinda thamani ya mkopo wa elimu ya juu kwa wanufaika jambo ambalo limekua mzigo kwa watumishi wengi nchini, lakini pia siku 100 kazini tayari Rais ametenga Sh Bilioni 449 kwa ajili ya kuwapandisha vyeo watumishi 92,619, " Amesema Ditopile.

Ditopile pia amefurahishwa pia na Rais Samia kuonesha hadharani mapenzi yake kwa vijana wa Bajaji na Bodaboda ambapo amepunguza adhabu zinazotolewa kwao pindi wanapofanya makosa ya Barabarani kutoka Sh 30,000 hadi Sh 10,000 kwa kosa moja.

KUWAPA NAFASI WANAWAKE

Kw upande wa kuwainua Wanawake katika kufikia ile 50 kwa 50 kwenye usawa, Rais Samia amefanya vizuri ambapo kwa siku 100 tu akiwa kazini ameteua Makatibu Tawala 26 ambapo kati yao 12 ni Wanawake sawa na asilimia 46, lakini pia kwenye uteuzi wa Majaji 28 aliofanya ameteua Wanawake 13 sawa na asilimia 43.

" Rais Samia ametuheshimisha sana Wanawake, pamoja na kwamba tumepata Rais wa kwanza mwanamke lakini hata kwenye uteuzi ametoa fursa kwa Wanawake Sana, kwenye Muhimili wa Bunge kwa mara ya kwanza amemteua Katibu Mkuu wa Bunge wa kwanza Mwanamke, bado kwenye asilimia 36 ya Wabunge Wanawake ameteue asilimia 21 kwenye Baraza lake la Mawaziri, tunamshukuru sana," Amesema Mbunge Ditopile.

Amesema hata kwenye uteuzi mpya alioufanya hivi karibuni wa Wakuu wa Wilaya amejitahidi kuteua idadi kubwa ya maDC Wanawake lengo likiwa ni kuzidi kuongeza usawa wa kijinsia.

MIRADI YA MAENDELEO

Ditopile amesema kupitia Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2021/22 inaonesha jinsi gani Rais Samia amepanga kutekeleza miradi ya kimkakati itakayokua na tija na Taifa ikiwemo mradi wa kufua umeme wa Bwawa la Mwalimu Nyerere, ujenzi wa Reli ya Kisasa ya SGR, Ujenzi wa madaraja makubwa na madogo na mingine mingi.

" Kupitia bajeti yetu Rais Samia ametuonesha kuwa mpango wake ni kuboresha Shirika la Ndege Tanzania ATCL, Ujenzi wa Reli ya kiwango cha kimataifa kutoka Mtwara hadi Mbamba Bay, ujenzi wa Bomba la Mafuta ghafi kutoka Hoima Uganda hadi Tanga.

Lakini pia ametuhakikishia kumaliza ujenzi wa madaraja makubwa na Barabara za juu za Daraja la Kigongo-Busisi Mwanza, Tanzanite la Dar es Salaam, Interchange ya Kamata, Dar es Salaam pamoja na ununuzi wa meli za uvuvi," Amesema Ditopile.

Ditopile amesema kwa siku hizi 100 za Rais Samia zimekua zenye matokeo chanya kwa Nchi na watanzania kwa ujumla ambapo hata imani kwa wananchi juu ya kiongozi wao imekua ni kubwa na isiyo na mashaka.

Amesema pia limekua jambo la faraja na kubwa kuona Rais akitenga muda wake kuongea na makundi mbalimbali ambapo alikutana na Wazee wa Mkoa wa Dar es Salaam, akakutana na Wanawake jijini Dodoma lakini pia hivi karibuni akakutana na vijana jijini Mwanza.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...